Maadui wa Rais Samia pale anapowahudumia Watanzania

Katika saikolojia, kuna somo linaitwa “Ingratiation”. Maana yake ni mbinu za kisaikolojia ambazo mtu anaweza kuzitumia kumvuta adui upande wake. Mwanasaikolojia bingwa, Edward Jones ‘Ned’, ambaye alipata kuwa profesa wa vyuo vikuu vya Duke na Princeton, Marekani, anatajwa kama baba wa Ingratiation kutokana na kazi kubwa aliyoifanya.

Ingratiation ni mbinu ya kutoa sifa za ukweli na uongo, kumfanyia mtu vitendo vya kumvutia akuone wewe ni mwema sana kisha akuamini. Mbinu hizo za hadaa hujumuisha pia uchonganishi.

Ndani ya Ingratiation kuna tawi linaitwa flattery au adulation (blandishment), yaani kumjaza mtu upepo na sifa za kijinga, avimbe kichwa, kisha ampende anayemsifia na kumwona ni muhimu sana kwake.

Huo utoaji sifa za kupitiliza (flattery) na mbinu zote za kisaikolojia kumvuta mtu na kumhamasisha akuone wewe ni bora na unayemfaa (ingratiation), hutumiwa na jamii ya watu wenye kuitwa sycophants.

Kwa kawaida sycophants ni watu watiifu, watoa sifa nyingi na kujiona wao huwa na umuhimu kwa mhusika kuliko hata viongozi wenzake au familia yake. Sycophant anaweza kujiamini kwa mtu kuwa yeye ni wa muhimu kuliko hata mkewe au mumewe.

Sycophant ni neno lililoanza kutumika nyakati za Classic Athens, Ugiriki ya Kale, tangu Karne ya Tano Kabla ya Kristo (BC). Wakati huo Waathens hawakuwa na polisi, isipokuwa sycophants ndio walisambazwa mitaani na kufuatilia matukio ya kiusalama kisha kuwaripoti kwenye mamlaka husika.

Baada ya muda, ilikuja kubainika kuwa sycophants walikuwa wanatumia nafasi zao vibaya, kwani walikuwa wakiwazushia watu kesi na kufikishwa mahakamani. Kesi zilipofika mahakamani zilikosa uthibitisho wa kisheria.
Kilichogundulika ni kuwa sycophants waliwasingizia kesi watu ili waonekane wanafanya kazi nzuri kwenye macho ya wakuu wao.

Walitumia zaidi nafasi zao kupongeza watawala. Hata mambo yalipoonekana kwenda ndivyo sivyo, wao hawakushauri vinginevyo, isipokuwa waliitikia kila walichoambiwa. Hii ndiyo sababu sycophants wakatungiwa jina la Yes-Men, kwamba wao kila kitu waliitikia.

Sasa basi, sycophants au Yes-Men ndio huitwa wapambe kwa Kiswahili. Siku hizi wanaitwa chawa. Wapambe hutumia mbinu za kisaikolojia ili kuteka imani ya wakuu wao. Hutoa sifa na kufanya mambo tofauti kujionesha wao ndio wana mapenzi makubwa na ni watiifu hasa. Kwa kawaida binadamu hupenda sifa na kunyenyekewa. Hivyo, mtu mwenye kumnyenyekea na kumsifu, humwona wa maana.

Binadamu hupenda kusemwa vizuri. Zaidi hujisikia raha sana anaposhinda vita yoyote. Binadamu hupamba moto anapojua au anaposikia watu humsema vibaya. Kikubwa zaidi cha kutambulika ni kwamba asili ya binadamu akishamwamini mtu, kila analomwambia hulikubali kwa asilimia kubwa na kulipitisha kama ndiyo ukweli wenyewe.

Hapo ndipo palipo na mtaji wa wapambe au chawa. Kwa vile huaminika, basi hutumia mwanya huo kukuza uhasama palipo na mahitaji ya suluhu.
Katibu Mkuu wa zamani wa uliokuwa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim, mwaka 2011, alifanya mahojiano na kituo redio cha Clouds FM na kueleza jinsi wapambe huwahadaa viongozi wengi wa Afrika kinyume na ukweli, matokeo yake kuangusha tawala nyingi.

Alizungumza kuhusu wapambe alipokuwa anatoa mtazamo wake baada ya tukio la kukamatwa kisha kuuawa kikatili, aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.

Salim alisema: “Watakuwa nyuma yako wanakwambia mzee hakuna tatizo lolote, mzee unapendwa sana, mzee utavuka, mzee utashinda tu, hali inakuwa mbaya na hali halisi wanaiona lakini hawaisemi.”

Alichokifikisha Salim ni kwamba viongozi hudanganywa hali halisi. Ni ukweli kwamba silaha kuu ya wapambe ni kuzungumza maneno yenye kupendwa na wakuu wao. Chawa hutambua kuwa kumweleza masta wake maneno yenye kumuumiza au kumkatisha tamaa ni kujipunguzia alama za kupendwa. Akitokea wa kumpa maneno yenye kumpendeza, huyo atapendwa zaidi.

Huu ndio ujumbe ambao nimekusudia kuufikisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Maadui zake namba moja, hawatakuwa wapinzani wanaokosoa hadharani, bali wale wenye kujifanya wema kwake, wanamsifu na kumpamba kila uchwao. Kisha, kuwasema wengine vibaya mbele yake ili kumchonganisha.

Rais Samia ni binadamu. Kiasili, hakuna binadamu asiyefanya makosa. Kama anakuwepo mtu ambaye hamkosoi, kila siku anamsifu, huyo ni adui. Kila binadamu anahitaji kuwa na watu ambao ndiyo kioo kwake.

Wamtazame usoni na kumweleza anapokosea. Mtu ambaye anakwambia kila siku wewe ni mzuri, hafai.

Kawaida, watu wanaposifia sana, hufika wakati humaliza kila neno la sifa, lakini huhitaji kuendelea kuwa muhimu kwa wanayemsifia. Hapo ndiyo huanza maneno ya uchonganishi. Rais Samia ana Baraza la Mawaziri, lakini wapambe watamwambia kuna mawaziri wanamhujumu.

Rais, kutokana na unyeti wa nafasi yake, vilevile wajibu mkubwa anaobeba, hutakiwa kuwa na kiwango bora cha moral compass, yaani uwezo wake wa kupokea mambo, kutafsiri, kuchuja na kufanya uamuzi kwa usahihi. Moral compass husaidia kupembua taarifa sahihi na uzushi. Dawa ya chawa na maneno yao ni kiongozi kuwa na kiasi kizuri kuchuja maneno na kufanya uamuzi kwa umakini mkubwa.

Mitandaoni hadi kwenye vyombo vya habari, sauti za watu wanaomsifia Rais Samia, kuna wakati mpaka zinaogopesha. Unajiuliza, je, hawa wasifiaji hawamchoshi Rais? Usifiaji wenyewe hauna maudhui mapya, ni yaleyale ya siku zote. Lengo lao ni kutaka kuingia kwenye kitabu kizuri cha Rais Samia.

Kuna msemo wa Kiingereza “too much of a good thing”, ukiwa na maana kuwa chochote kizuri, kikipitiliza kinageuka hatari. Si jambo baya kumsifia Rais Samia, hasa anapofanya mambo mazuri, lakini sifa zinapopitiliza, inakuwa tatizo. Hivyo, maadui wa Rais Samia ni wapambe au chawa.

Unaweza kujipatia kitabu changu “Kikwete Lowassa: Urafiki, Ndoa Yao ya Kisiasa, Uadui” kwenye maduka ya TPH Bookshop na House of Wisdom, Samora Avenue, Dar es Salaam. Piga simu namba +255713355717, utafikishiwa popote. Bei ni Sh75,000.

Related Posts