Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko mahitaji ya umeme Tanzania yameongezeka kutoka asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka kutokana na kuongeza kwa mahitaji, wateja na shughuli za kiuchumi.
Amesema ongezeko hilo pia limetokana kuongezeka kwa vyanzo vya umeme vinavyotegemewa ambavyo ni maji yanayochangia asilimia 39, gesi asılıa inayochangia asilimia 56.1, mafuta asilimia 4.3 na vyanzo vingine 0.5. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Kutokana na hali hiyo ameieleza jumuiya ya wafanyabiashara wa Ujerumani na wadau wa nishati kuwa Tanzania itaendelea kutoa kipaumbele kwenye vyanzo mbadala vya nishati ikiwemo gesi, upepo, jua na vyanzo vingine mbadala vya umeme, ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme wa kutosha kwa wananchi.
Dk. Biteko ameyasema hayo jana tarehe 11 Juni 2024 alipokutana na ujumbe wa chemba ya wafanyabiashara na wadau wa sekta ya nishati kutoka Ujerumani wakiongozwa na Balozi wa shirikisho la Ujerumani nchini, Thomas Terstegen.
‘’Nipende kuwashukuru wenzetu wa Ujerumani kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwenye sekta ya nishati hususani kwenye miradi ya umeme ambapo wamekuwa wakifadhili na kutoa mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo,’’ alisema Dk. Biteko.
Alisema nishati inabeba ajenda kubwa nchini ikiwemo usalama wa nishati yenyewe, upatikanaji wa nishati na uhakika wa nishati kama ilivyoainishwa kwenye sera ya nishati ya mwaka 2015 na kuongeza kuwa serikali imejipanga kufikisha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2030.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan anatamani kuona wadau na makampuni mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya uwekezaji yanapewa fursa ili kutekeleza miradi iliyoainishwa na imekosa fedha ili kutumia fursa hiyo kuwekeza kwa pamoja na wadau wa sekta binafsi.
Kwa upande wake, Balozi wa Shirikisho la Ujerumani, Thomas Terstegen alisema Tanzania imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Ujerumani hususani kwenye sekta ya nishati na kuahidi kuendelea kufadhili utekelezaji wa miradi kwenye sekta ya nishati ili kuinua uchumi wake.
Aidha, mkutano huo ulilenga pia kutoa fursa kwa wadau wa sekta binafsi na nishati kufahamu fursa zilizoko nchini ujerumani na namna ya kuzitumia.
Ulihudhuriwa na Maren Diale Schellschmidt ambaye ni Mkuu wa Msafara kutoka chemba ya wafanyabiashara na Viwanda kutoka Afrika, wawakilishi kutoka shirikisho la watu wa Ujerumani, wawakilishi kutoka Serikalini na kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau wa sekta ya nishati.