Makundi maalumu yapewa neno INEC ikijiandaa kwa uchaguzi

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeyataka makundi maalamu, wakiwamo watu wenye ulemavu kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura, kutokana na mifumo kuboreshwa.

Tume imesema wapigakura wengi wamekuwa hawajiandikishi, wakiwamo wenye ulemavu, wajawazito na wenye watoto wachanga.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Juni 11, 2024 na Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele alipofungua mkutano wa wawakilishi wa kundi la vijana kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura.

Amesema Tume imeboresha mfumo wa uandikishaji hivyo mpigakura aliye kwenye daftari anaweza kuboresha taarifa zake kidijitali kwa kutumia simu ya kiganjani au kompyuta.

“Mpigakura anayeweza kutumia mfumo huo ni yule aliyepoteza kitambulisho cha kupigia kura au kuhama kituo, ambaye atatembelea kituo anachokusudia kujiandikishia kuchukua kadi,” amesema.

Amesema matumizi simu na kompyuta yatapunguza msururu kwenye vituo na kuharakisha uandikishaji.

Amesema kwa wale wa makundi maalumu wamewekewa mazingira rafiki ambayo hayatasababisha wakae kwenye foleni.

Akizungumzia uboreshaji wa majaribio uliofanyika Novemba 24 hadi 30, 2023 katika kata za Ikoma mkoani Mara na Ng’ambo, Mkoa wa Tabora mfumo ulionyesha ufanisi mkubwa.

 “Lengo la majaribio ilikuwa kupima uwezo wa vifaa na mifumo ya uandikishaji itakayotumika wakati huu wa uboreshaji wa daftari,” amesema.

Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura unatarajiwa kuanza Julai Mosi, 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Femina, Ruth Mlay amepongeza mabadiliko ya mfumo akitaka makundi hayo kujitokeza kujiandikisha ili kupata haki ya kuchagua viongozi.

“Mchakato huu ni muhimu ukizingati kuna mabadiliko ya mfumo na teknolojia, ombi langu kwa vijana kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kuanzia Serikali za mitaa kwa kuwa ni ngazi muhimu,” amesema Mlay.

Ibrahim Apolinary, kutoka Taasisi ya Taistudio amewataka vijana kujitokeza kujiandikisha na kupiga kura badala ya kulalamika baada ya uchaguzi.

“Kupiga kura kunafanya mtu ushiriki katika kufanya uamuzi wa kuiletea nchi maendeleo, kutoshiriki unakuwa umekosa haki kwa mujibu wa Katiba inayompa kila mtu haki ya kuchagua na kuchaguliwa,” amesema.

Mwakilishi wa Taasisi ya Open Youth Opportunity, Hussein Baswariu ameshauri Tume kuweka utaratibu, endapo mtu atapoteza kadi kuwe na namna ya kuipata badala ya kusubiri uboreshaji.

“Tumeona Tume imeboresha mfumo kwa wale walipoteza kadi au kubadilisha taarifa kwa kutumia simu au kompyuta, tungeshauri kuwe na utaratibu wa kupata kadi muda wowote ili kunapokuwa na uchaguzi mdogo waweze kushiriki,” amesema Baswariu.

Related Posts