Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amewataka askari na maofisa wa vyombo vya usalama waliopandishwa vyeo na Rais Samia Suluhu Hassan kutenda kazi kwa kufuata haki na uadilifu katika kuwahudumia wananchi.
Ameeleza hayo leo Juni 11, 2024 jijini Dar es Salaam, wakati akifungua kikao cha Tume ya Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji.
“Ni imani yangu sasa kwamba mashauri yote yaliyokuwa hayajashughulikiwa tume itayashughulikia, nendeni mkavitendee haki vyeo hivyo,” ameagiza Masauni.
Amesema haki huenda na wajibu, hivyo amewataka wakawe waadilifu na wakafanye kazi zilizokusudiwa na Rais za kuzuia na kupambana na uhalifu, akisema huko chini vilio ni vingi waende wakasikilize na kuvitafutia ufumbuzi.
Akizungumzia changamoto alizokumbana nazo wakati akifanya ziara, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema askari wengi wa Magereza walikuwa wanauliza upandishwaji wa vyeo.
“Nashukuru kuona hoja ya upandishwaji vyeo iliyoibuliwa na askari wa Jeshi la Magereza imefanyiwa kazi,” amesema Sillo.
Mkurugenzi msaidizi wa tume hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, George Mwansasu amesema idadi ya waliopandishwa vyeo, Jeshi la Polisi ni maofisa waandamizi 154, Zimamoto na Uokoaji maofisa waandamizi 11, Jeshi la Uhamiaji maofisa waandamizi 50 na Jeshi la Magereza 50.