Saa chache baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Simba Salim Mhene ‘Try Again’ kujiuzulu nafasi hiyo, mwekezaji za klabu hiyo Mohammed Dewji ‘MO’ ameibuka na mambo sita huku akitangaza kurejea kwenye nafasi hiyo.
Mapema leo jioni, Try Again alitangaza rasmi kujiuzulu nafasi hiyo, kufuatia changamoto zilizoikumba klabu hiyo ikianguka kwa matokeo kwa kushika nafasi ya tatu kwenye msimu uliomalizika.
Akitangaza muda mfupi uliopita MO ameridhia kurejea kwenye kuongoza bodi ya klabu hiyo kuhakikisha anarejesha utulivu ambao ulipotea ndani ya miaka mitatu.
Katiika taarifa yake kwa Wanasimba MO ameyataja mambo sita yaliyoikwamisha Simba yakiwemo mvurugano na makundi yaliyozalishwa na uchaguzi wa viongozi wa juu kwa upande wa wanachama.
“Tangu uchaguzi upite tumekuwa na mvurugano na makundi yaliyotokana na uchaguzi, hili limesababisha migongano mbalimbali ndani ya klabu yetu, niwaombe Wanasimba wenzangu tuvunje makundi na turudi kushirikiana kama kauli yetu inayosema Simba Nguvu Moja,”amesema MO.
Ameelezea pia namna mabadiliko ya benchi la ufundi na eneo hilo kutokuwa imara limechangia kuirudisha nyuma timu hiyo kongwe.
“Tulipoteza ubora wa kucheza mpira wetu wa ‘pira biriani’ kutokana na mabadiliko ya makocha, nitashirikiana na viongozi wenzangu kuunda benchi imara la ufundi litakaloturudishia ubora wetu.”
Tajiri huyo ameutaja pia usajili usiokidhi kiu ya Wanasimba ukichangia kuirudisha nyuma timu hiyo kutawala kwa kuchukua vikombe vya ndani ya nchi.
“Tumekuwa tukisajili wachezaji wengi ambao wameshindwa kukidhi kiu ya Wanasimba, nataka niwaambie Wanasimba tutakwenda kufanya usajili mzuri utakaorudisha ubora wa kikosi chetu.”
Ameelezea pia kitokamilika kwa mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na kwamba wanakwenda kuhakikisha hatua zilizosalia zinamalizika sambamba na kuboresha miundo mbinu ya viwanja vyao ya mazoezi vilivyopo Bunju ambapo amekiri kuwa havikidhi vigezo.
“Tutakwenda kumalizia mchakato wa mabadiliko ili kila mwanachama aweze kumiliki hisa zake, suala la tano ni miundo mbinu yetu ya eneo la viwanja nayo tutaiboresha ili iendane na hadhi ya Simba.
MO amemalizia kwa kutaja eneo la uwekezaji kwa soka la vijana na kwamba wataweka nguvu kubwa itakayozalisha vipaji kwa kuanzia chini.
Huku akisema kuwa ameongea na Try Again na amekubali kubaki kama mjumbe wa bodi upande wa mwekezaji.