Dar es Salaam. Siku moja baada ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) na baadhi ya viongozi wa dini kutoa matamko ya kuiomba Serikali iufungie mtandao wa X (zamani Twitter), baadhi ya wadau wamepinga vikali ombi hilo wakisema ni ukiukwaji wa haki ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.
Hata hivyo, Serikali kupitia, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema wameshaanza mazungumzo na kampuni ya X na mtandao wa X ili kudhibiti maudhui yake ili kulinda usalama wa mitandao na watumiaji.
Kampeni hiyo imekuja wakati kukiwa na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano yaliyowezesha uwasilishaji wa taarifa za kibiashara, siasa na masuala ya kijamii kupitia mitandao ya jamii.
Mtandao wa X pamoja na mitandao mingine imekuwa ikitumiwa na wanasiasa kufanya mijadala na kurusha matukio ya mikutano na taarifa zao, huku vyombo vya habari zikiwemo kampuni za magazeti, redio na televisheni wamekuwa wakiitumia mitandao yao kuwasiliana na wasomaji wao.
Zohra Malisa ambaye ni Mhariri wa Maudhui ya Mitandao ya Jamii wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), amesema kampuni hiyo inatumia mitandao ya jamii ikiwamo X kuwafikia wasomaji wa magazeti na tovuti zake.
“Tunatumia mitandao ya jamii kuwafikia wasomaji wetu ambao kwa sasa wengi wamehamia huko. Pia tunatumia mitandao kama jukwaa la majadiliano kwa kuwaleta pamoja watunga sera, wafanya uamuzi ili kufanya mijadala ya kitaifa,” amesema.
Amesema pia MCL inatumia mitandao hiyo kibiashara kwa kuuza maudhui na kupata gawio kutokana na mauzo hayo.
“Hayo madai kwamba X inatoa maudhui ya ngono ni ya mtu mmoja moja, lakini mitandao hii inapaswa kutumika kuleta faida zaidi,” amesema.
Mtumiaji maarufu wa X nchini anayejulikana kwa jina la Roland Malaba maarufu kwa jina la Madenge ameandika katika ukurasa wake: “Wakati nchi nyingine zikipambana kufanya internet iwe bure, nafuu sababu imekuwa ni chanzo cha mapato, maarifa, taarifa kwa dunia ya sasa, sisi tunapambana mitandao ifungwe eti haina maadili. Mtandaoni unapata ukitakacho …”
Hata hivyo, Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye alipoulizwa, amemtaka mwandishi kuuliza suala hilo Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA).
Hata hivyo, Mkurugenzi wa TCRA, Dk Jabir Bakari alipopigiwa simu jana hakupokea.
Jana Jumanne, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa UVCCM, Mohamed Kawaida alisema wamesikitishwa na baadhi ya mitandao ya kijamii inavyohimiza mapenzi ya jinsia moja.
“Tumeona kupitia Serikali yetu pendwa ya Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania mitandao yote yenye maudhui ya namna hii wameifungia sasa umefika wakati Serikali na mtandao huu nao kuufungia,” alisema.
Amesisitiza kama wataondoa maudhui yanayofundisha mapenzi ya jinsia moja wako tayari kuendelea kutumia mtandao huo lakini kabla ya yote mtandao huu unapaswa ufungiwe.
“Serikali ya Tanzania imeshawahi kufungia mitandao ya kijamii ambayo ilikuwa inajihusisha na maudhui yasiofaa, hivyo basi waufungie mtandao huu kama mitandao iliyopita,” alisema.
Mbali na UVCCM, wito huo pia umetolewa na baadhi ya viongozi wa dini akiwamo Katibu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania, Allen Siso aliyeutuhumu mtandao wa X kwa kuchochea mapenzi ya jinsia moja na kuiomba serikali kuufungia.
“Naungana na viuongozi wa Taifa hili, kukemea kwa dhati ushoga, mapenzi ya jinsia moja katika Taifa letu, kukemea ulawiti na vitendo vyote vinavyoharibu taifa letu,” amesema Siso katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Naye Sheikh Hilal Yusuf maarufu Sheikh Kipozeo amesema: “Tunaiomba Serikali iliangalie kwa kina jambo hili na itusaidie kuiufungia Twitter (X) isiendelee kufanya kazi kwa sababu inatuharibia jamii.”
Hata hivyo, maoni yamepingwa na chama cha ACT Wazalendo wakisema ni njama za Serikali katika mwendelezo wa kuzuia haki ya kupata taarifa na uhuru wa kutoa maoni.
Taarifa iliyotolewa na Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa chama hicho, Rahma Mwita imesema Serikali ya CCM imekuwa na utamaduni wa kutovumilia maoni, mitazamo na fikra tofauti zinazotolewa na wananchi kuhusu viongozi na sera zao.
“Mara zote inatumia hila za namna tofauti ili kutimiza dhamira hiyo kandamizi,” amesema.
Alitaja mbinu hizo alizoita ni kandamizi kuwa pamoja na Sheria ya Mawasiliano ya Kielekroniki na Posta ya 2010, Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Takwimu ya 2015.
“Watanzania wamekuwa wakipitia mazingira magumu kutokana na hila za Serikali kudhibiti uhuru na maoni yao dhidi ya watawala,” amesema.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Pambalu ameandika katika ukurasa wake wa X akiikosoa UVCCM.
“Kwamba UVCCM waliposikia tu mtandao unaitwa X tu wakajua utakuwa na mambo ya X (ngono). Kwa nini waliposikia mtandao unaitwa X akili yao haikuwatuma kwenye zile hesabu za darasa la saba za tafuta thamani ya X na Y? Aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo amesema wanaopiga kampeni hiyo ni maadui wa uhuru wa kujieleza wanaotumia visingizio vingi kuhalalisha dhamira yao kwa kujua kwa kutojua.
“Sera ya mtandao wa X siyo mpya na imekuwa ikieleza wazi kwamba unaweza kukubali kuangalia maudhui yoyote unayotaka,” amesema.
Ameitaka Serikali kupeleka malalamiko yake X kueleza mambo inayolalamikia na itafute suluhisho.
“Kama Serikali ina malalamiko basi iwaandikie barua iwaeleze mambo wanayotaka yarekebishwe kwa mfano maudhui yanayoharibu watoto, kwa sababu Tanzania kama nchi huru ina wajibu wa kulinda raia wake, lakini siyo kutaka ufungiwe kabisa.
“Kama Mwalimu Julius Nyerere alivyosema ukishaanza kula nyama ya mtu, hautaacha, hivyo mkishaanza kufungia mtandao mmoja, hamtaishia hapo, mtaenda Instagram, kisha Facebook, Tiktok, halafu mtahamia kwenye magazeti, redio na televisheni,” amesema.
Ameshauri Serikali kutumia jumuiya za kikanda kufikisha malalamiko yake ikiwamo (Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika), SADC Afrika Mashariki (EAC) au Umoja wa Afrika (AU).
Mdau wa vyombo vya habari, Ernest Sungura amesema juhudi zozote za kuzuia uhuru wa kujieleza zinakwenda kinyume na Katiba na maazimio ya kimataifa ya haki za binadamu.
“Uhuru wa kujieleza ndio haki ya Kikatiba unaostahili kulindwa siyo tu na Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayostahili kulindwa, bali pia matamko na maazimio ya kimataifa na kikanda na Serikali zinapaswa kuheshimu hilo,” alisema.
Mmoja wa watumiaji wa mtandao huo, Mkazi wa jijini Mwanza, Frank James amesema: “Tunachokiona tunakwenda kwenye uchaguzi, sasa isije kuwa ni mkakati wa kutaka kuufunga kwa hofu tu ya nini kitatokea kama utaachwa. Serikali isikubali kuingia mtego huu wa kuufunga kwani hautakuwa na afya.”
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alipoulizwa amesema wameshaanza mazungumzo na kampuni ya X.
“Ni kweli kwamba wiki iliyopita vyombo vya habari duniani vilitangaza kwamba mtandao wa X sasa utaruhusu maudhui ya picha za ngono kurushwa hewani.
“Bado Serikali inalitafakari jambo hili na kimsingi ilishaanza mazungumzo na wamiliki wa X kabla ya jambo hilo ili waheshimu sheria yetu ya usalama mtandaoni na kanuni za maudhui lakini bado hawajatoa ushirikiano,” amesema.
Amesema mitandao mingine hufuata maelekezo ya Serikali ili kuzuia maudhui yasiyofaa kuingia Tanzania na hivyo kuruhusu wananchi wetu kuendelea kuitumia kwa shughuli zao.
“Ni matarajio yetu hata X nao watatoa ushirikiano. Kwa sasa Serikali bado haijachukua hatua.
“Serikali haifanyi mambo kwa papara bali inatumia sheria, utaalamu na kutanguliza mbele maslahi ya jamii ya Watanzania. Ikichukua hatua itatoa taarifa kupitia mamlaka au wizara inayosimamia sekta hii,” amesema.
Mfanyabiashara na mjasiriamali, Fila Samson aliitaka Serikali kuangalia namna ya kushughulika na wanaosambaza na maudhui yasiyofaa na kuwachukulia hatua wapotoshaji badala ya kufuga mtandao mzima nchini.
Kwa sababu yeye binafsi mtandao huo ndiyo unaomfanya kuendesha maisha yake baada ya kujiwekeza na kutengeneza jina ambalo watu wamelizoea jambo linalomuwezesha kupata wateja wengi.
“Nguvu zetu ziko Twitter (X), tunakula kupitia huko ukifunga unamaanisha kuwa tutafute njia nyingine ya kutafuta hela na wateja, taani tuanze upya, ujue unapata wapi wateja, kuwezekeza kupata wateja itatuathiri haijakaa sawa,” amesema Samson ambaye hutengeneza picha mbao, saa, vikombe vyenye ujumbe mbalimbali na kuuza.
Mfanyabiashara ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kufungia mtandao wa X haiwezi kuwa suluhisho la kuzuia maudhui wanayoyapiga vita bali kutafuta namna ambayo wanaweza kushughulika nayo.
“Kufunga ni kuonyesha udhaifu mkubwa kwamba vyombo vyetu husika vimeshindwa kuchukua hatua za kudhibiti maudhui yanayolalamikiwa na hawatoshi kukaa pale, kufunga siyo suluhisho, watu wanaweza kuhamishia kitu hicho hicho katika mitandao mingine, wajitathimini,” amesema.