KOCHA na daktari wa viungo wa Yanga, Mtunisia Youssef Ammar aliyekuwa akielezwa kuwa ni kipenzi cha wachezaji wengi amesepa kimyakimya.
Sababu kubwa ikitajwa ni mkataba wake umemalizika na uongozi haukuwa tayari kumuongezea huku ikielezwa kwamba Kocha Miguel Gamondi analeta mtu wake. Ammar aliachwa Yanga na kocha aliyeondoka, Nabi Mohammed.
Moja ya sifa za hivikaribuni kwa Kocha huyo ni kumrejesha haraka kwenye ubora wake, Khalid Aucho aliyekuwa na majeraha ambayo wengi walidhani angekosa mechi zaidi ya nusu msimu.
Lakini inaelezwa kuwa FAR Rabat ya Morocco ilimrejesha nchini, Bernard Morrison aje akatibiwe kwaajili yake kwani Nabi anamuelewa zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti, mtaalamu huyo alisema amemalizana na klabu hiyo baada ya kumaliza mkataba wa kuitumikia Yanga mwisho wa msimu huu huku akikiri kufurahia mafanikio na maisha mazuri aliyoishi ndani ya timu hiyo.
Alisema ameshaondoka nchini lakini ataendelea kuyaishi maisha ya Tanzania kutokana na upendo mkubwa alioonyeshwa na mashabiki, viongozi na wachezaji wa Yanga ndani ya misimu mitatu aliyoitumikia timu hiyo.
“Nilikuwa na misimu miwili bora kutokana na mafanikio ya timu lakini najivunia kufanya kazi kwa ubora kutokana na kuwasimamia mastaa kadhaa ambao walipatwa na shida na kurudi haraka kiwanjani,” alisema na kuongeza;
“Kazi yangu ilwwikuwa ni kusimamia wachezaji hasa wale ambao wametoka kwenye matibabu na kutakiwa kurudi uwanjani haraka kwa kuwapa mazoezi ya kuwarudishia utimamu kama ilivyokuwa kwa Aucho, Mshery, Kibwana na Morrison akiwa ndani ya Yanga na hata alivyotoka alirudi kuniona kwa ajili ya huduma yangu.”
Alisema baada ya Aucho kufanyiwa upasuaji kipindi ambacho timu ilikuwa inahitaji huduma yake hakuna mtu aliyefikiria kama atarudi uwanjani kwa haraka na kuendeleza ubora alionao.
“Kwa staa huyo haikuwa kazi ngumu kwani anaipenda kazi yake alihakikisha anafuata ratiba alizopewa, hii ni kutokana na kupenda kazi anayoifanya ilinirahisishia hadi mimi kumpa mazoezi ambayo yalimrejesha haraka kiwanjani,” alisema na kuongeza;
“Pia kina Mshery, Kibwana nao hawakuniangusha, ni vijana wadogo ambao pia walipitia shida nilisafiri nao hadi Afrika Kusini kwa ajili ya upasuaji na kusimamia matibabu yao walikuwa na nidhamu ya kuuguza majeraha yao nawaona mbali kwani wana vipaji.”
Alimtaja Aucho kama staa mwenye uchu wa mafanikio. Mbali na Aucho, amewataja Abuutwalib Mshery, Kibwana Shomari, Bernard Morrison kuwa ni wachezaji ambao amefanya nao kazi kwa ubora hasa kipindi walichokuwa wanapitia hali ya majeraha.
Ammar amehudumu ndani ya Yanga kwa misimu mitatu akitwaa mataji matano tofauti, Ligi Kuu Bara (3) na mawili Kombe la Shirikisho (FA), huku akiwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo ilipocheza fainali Kombe la Shirikisho Afrika 2022/23 na msimu uliomalizika wacheza hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.