Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limemfungia promota Shomari Kimbau kujihusisha na shughuli za mchezo wa ngumi kwa kipindi cha miaka miwili.
Mbali na Kimbau, BMT pia imeifungia Taasisi ya Ukuzaji wa Mchezo wa Ngumi iitwayo Promosheni Golden Boy Boxing yenye usajili namba 72 kutojihusisha na mchezo huo kutokana na kushindwa kufuata utaratibu wa Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kufuatia taharuki iliyotokea kwa wadau wa michezo katika pambano la kimataifa kati ya Bondia Hassan Mwakinyo dhidi ya Mghana Patrick Allotey la kuwania Mkanda wa Ubingwa wa WBO katika uzani wa middle lililopangwa kufanyika Mei 31, 2024.
Uamuzi wa baraza hilo umetokana na kutoridhishwa na maelezo yaliyotolewa na Kimbau baada ya BMT kumtaka kufanya hivyo kwa njia ya maandishi huku baraza likijiridhisha kwamba promota huyo hakuwa makini.
Hata hivyo, BMT limetoa angalizo kwa mapromota wengine watakaoshindwa kutimiza wajibu wao, halitosita kuwachukulia hatua stahiki.
Pambano la Mwakinyo lilikwama kupiganwa siku husika na kuchezwa siku inayofuata ya Juni Mosi na bondia huyo Mtanzania kushinda ka TKO ya raundi ya tatu baada ya Allotey kugoma kuingia ulingoni kuanza raundi hiyo ya tatu kaa madai aliumia bega.
Matokeo hayo yalimfanya Mwakinyo kutetea mkanda huo alioutwaa mwaka jana.
Hii ni mara ya pili kwa Kimbau kuingia matatani, kwani Desemba, 2020 aliwahi kufungiwa mwaka mmoja TPBRC.