Puma Tanzania watoa gawio la bilioni 12.2 kwa Serikali

KAMPUNI ya Mafuta ya Puma Tanzania imetoa gawio la Sh. 12.2 bilioni kwa Serikali na kuahidi kuendelea kuboresha huduma zake ili kufanya vizuri zaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Puma wamekabidhi gawio hilo leo Jumanne Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan. Kampuni hiyo ni moja ya 10 zilizowasilisha gawio kwa Serikali ambazo serikali ina hisa.

Akizungumza baada ya kukabidhi gawio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania, Fatma Abdallah amesema mafanikio hayo yametokana na mazingira bora ya biashara yaliyowekwa na Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan (katikati) akipokea hundi ya gawio la Sh. 12.2 bilioni kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania, Fatma Abdallah (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo Dk. Seleman Majige (kushoto). Gawio hilo limekabidhiwa Ikulu jijini Dar es Salaam na kushuhudia na wakuu wa taasisi na mashirika mbalimbali ambayo yamehudhuria tukio hilo.

“Ametuongoza vizuri, ameweka mazingira wezeshi kwa sisi wawekezaji kufanya biashara kwa usalama na ubunifu. Pia tunamshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Dotto Biteko kwa ushirikiano wake kwa sababu wote wamekuwa ni viongozi ambao hutushauri lakini wamekuwa wakiweka mazingira bora ya uwekezaji,” amesema.

Amesema kigezo kikubwa ambacho kimewazesha kutoa gawio hilo ni kinatokana na kufanya kazi vizuri bodi chini ya Mwenyekiti Dk. Selemani Majige.

Amesema katika kuendeleza ufanisi kampuni hiyo itaendelea kutoa huduma na kuziboresha na kwamba mikakati yao ni kutoa huduma kidigitali katika kutoa huduma zao na mwaka huu wamepanga uwafikia watanzania wengi kwenye kusambaza nishati.

Pia amesema kwa kuwa Serikali imetilia mkazi matumizi ya nishati safi ya kupikia, vivyo hivyo kampuni hiyo inaunga mkono juhudi hizo za serikali ili kufikia malengo ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi kupikia ifikapo mwaka 2034.

Amesema ili kutekeleza ipasavyo mpango, kampuni hiyo itazindua kituo cha gesi kwa ajili ya kujaza kwenye magari na uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika mwaka huu.

Related Posts