Rahis, waziri wako wa fedheha anatuhujumu

Mtukufu Dk, Dk, Dk, Dk, Dk Rahis. Naambwa unazo PhD tano.
Sina tabia ya kupongeza. Hivyo, kwa taadhima, nakuomba usishangae. Mie ni fyatu. Si msifiaji wala chawa. Ndo maana sianzi kwa mashairi, mapambio, ngojera na kamba. Huwa namsifu Sir God pekee na siyo masanamu wa kuchongwa na machawa ili wapate kujaza mitumbo.

Si kazi yangu, maana mie siyo chawa wala kunguni wa kujipachika uchawa wala mwenye kupwaya kimaadili na kitaaluma. Ni msomi kuliko Mwambukuzi. Ni fyatu kuliko Tunda Lishe na Pita Msingua, mafyatu wanaosifika kayani.

Leo, nakuletea skandali ya mwishiwa Madilu Lameki Nchembuz ambaye hupenda kuitwa doktari. Niseme wazi. Anakuaibisha, kukuhujumu, kutuhujumu, kukuchonganisha, na kukuchongea kwa mafyatu wanaoshangaa kwa nini kumwacha aendelee kutia aibu na hasara kaya na hata mjengo wetu mtukutu, sorry, mtukufu.

Hafai kuwa hata mtunza choo, so to speak. Juzi iliibuliwa skandali mjengoni na Mheshimiwa Joji Mwanisongo Lee ikimkariri Nchembuz akijisifu uzwazwa na uzembe. Hata kama muda umekwisha kuelekea uchakachuaji, Mwanisongo Lee ni jembe. Ningekuwa wewe, ningemteua awe waziri wa njuluku maana ana uchungu na njuluku na wakulima wetu.

Mwanisongo Lee popote ulipo, nakupa kongole fyatu wangu. Unastahiki, kwani hukuogopa mvua wala jua. Ulicheza clip mjengoni ambapo Nchembuz anajisifu kuwasikinisha mafyatu na kuwatajirishi wakwepa kodi. Hakuna kilichoniudhi hadi nikalala njaa zaidi ya kupata kanywaji kuondoa hasira kama madame Kipaza sauti aka Spiker kushindwa kuunda kamati kumchunguza hata kumuondoa madarakani Nchembuz mbali na kuamuru takokuru imfyatue.

Kama mjengo kweli ungekuwa wa mafyatu au kuwawakilisha, hasa ikizingatiwa ndiyo wanaohujumiwa kwenye skandalii hii, ingeletewa hoja kumchunguza Nchembuz liwe somo kwa wengine. Ajabu ya maajabu, hakuna aliyeona skandali hii kama tishio kwa maisha ya kaya, hasa kiuchumi. Tatizo nini?

Ajabu! Nchembuzi alipotakiwa kujieleza, siyo kujitetea, alipiga siasa na skandali ikafia hapo! Je, zipo skandali nyingine kama hata kubwa kuliko hizi ngapi? Je, kaya imeishapoteza njuluku kiasi gani? Ni mafyatu wangapi wapiga jembe waliokwishasikinishwa?

Kama ningekuwapo mjengoni, ningekamata shilingi na kuhakikisha huyu fyatu anafyatuliwa tena bila maji. Je, mtukufu rahis, umeridhia mchezo huu mchafu? Ili iweje? Je, unapanga kufyatua japo huwa hufyatui itakiwavyo nikikumbusha skandali za akina Riz One na Janwari Joseph Marope nilizokuletea ukaminya?

Je, kwenye uchakachuaji ujao, utatujibu nini tutakapomkumbusha skandali hizi na nyingine kama vile Deep Weed, Ngorongoro n.k? Je, mhujumu uchumi huyu analipwa mamilioni, kupewa hekalu, shangingi na wese bure kwa kazi gani iwapo amejifunga mwenyewe kuwa anahujumu kaya? Mafyatu twataka jambo moja tu, kuwajibishwa Nchembuz as soon as possible.

Mafyatu, hadi leo, hatujaelewa uzwazwa na majisifu hata mantiki ya kunyamaziwa kana kwamba alichofanya Nchembuz ni haki. Je, ni ile hali ya maadili kugeuzwa madili na baadhi ya mafyatu kujigeuza au kugeuzwa machawa wengine miungu?

Je, wanaachwa kwa vile wana sifa kuu za kujisifu na kukusifia kuwa umefanya mambo makubwa kama kukopa sana na kusafiri eti kuliko hata Vasco da Gama wa Musoga. Wee! Kausha. Heri lawama za mwenye busara kuliko nyimbo za wapumbavu na wasaka tonge. Mafyatu twasema wazi. Mummy, achana na masifa na kuteua kwa sifa na ithibati.

Clip aliyocheza Mwanisongo Lee ilimvua nguo mhujumu uchumi huyu ambaye mafyatu watafurahi kama utamtema haraka maana anatia aibu na hasara. Nchembuz, doktari wa akina Philo na Sofia, sijui alipataje hiyo PhD maana, hata akiongea huoni dalili zozote za ubukuzi. Nadhani Mwambukuzi hakosei anapowaita vilaza.

Wamelaza bongo hadi njuluku za mafyatu zaibwa wakiwa wamelala. Jamaa alibanwa inakuwaje anataka kuwatoza wafa kwa ngwamba kodi ilhali matajiri wanapeta. Hakutoa jibu lolote la maana zaidi ya kukusifia na kukusingizia kama gea yake ya kuendelea kuvurunda. Wizara si mali yake ya urithi kiasi cha kuchefua na kutia kinyaa.

Kwa vile hii ni kaya ya mafyatu na wanene mpo kwa vile mafyatu tumewakasimisha na kuwaamini maulaji, lazima tuzoze hadi umfyatue na kutuletea fyatu anayefaa, tena anayeweza kuwafyatua matajiri wasiolipa kodi. Kuna fyatu mmoja wa kaya ya jirani aliwahi kusema kuwa ukiona mafyatu wenye raslimali wakijipeleka majuu kubomu na kupangwa kama wanafunzi mbele ya mkuu wa shule, ujue kuna tatizo.

Kwa kaya yetu, tatizo kubwa mafyatu wanaoloona limeota sugu ni kuteuana kwa sifa za uchawa na ukunguni. Inakuwaje fyatu mwenye PhD, tena si ya kuzawadiwa, anafanya madudu kuliko hata waliosoma ngumbaru? Sasa mafyatu tunazoza tena bila kumung’unya kuwa fyatu Nchembuz atumbuliwe haraka japo huwa unaonea kinyaa majipu usiyatumbue kama mwendaze.

Leo sirongi sana. Muhimu, nasema wazi. Mummy fyatua huyu fyatu ili mafyatu wengine chawizi watie akili. Ukimfyatua usawa huu, mafyatu tutakumwagia kura za kula hadi uzimii. Hivi leo nimekunywa gongo kiasi gani?

Related Posts