Raia wa China alipa faini Sh300,000 kukwepa kifungo

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu raia wa China, Zheng Zhiyuan (47) kulipa faini ya Sh300,000 au kwenda jela miezi 36 baada ya kutiwa hatiani katika mashitaka matatu, yakiwamo ya kuishi nchini bila kibali na kuwatishia kwa kisu maofisa wa Uhamiaji.

Zheng amehukumiwa adhabu hiyo leo Juni 12, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya baada ya kukiri mashitaka.

Mahakama pia imemuamuru mshtakiwa kurudishwa nchini China atakapomaliza kutumikia adhabu.

Baada ya Wakili wa Serikali, Grace Nyarata kumsomea mashitaka katika kesi ya jinai namba 15955 ya mwaka 2024, alikiri makosa akaomba apunguziwe adhabu.

“Mshtakiwa umetiwa hatiani kama ulivyoshtakiwa baada ya kukiri mashitaka matatu uliyoshtakiwa nayo, hivyo mahakama inakuhukumu kulipa faini ya Sh100,000 kwa kila kosa au kwenda jela miezi 12 kwa kila kosa,” amesema Hakimu Lyamuya.

Kabla ya kutoa hukumu, Hakimu Lyamuya alimuuliza mshtakiwa iwapo ana lolote la kusema ili mahakama iweze kumfikiria.

Mshtakiwa alikaa kimya, baadaye alijibu ‘i have no idea’ (sijui).

Kesi hiyo iliendeshwa kwa lugha ya Kiingereza kutokana na mshtakiwa kuieleza mahakama kwamba ndiyo anayoielewa zaidi.

Hakimu alimuhoji sababu ya yeye kuwatisha maofisa Uhamiaji kwa kutumia kisu na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:

Hakimu: Kwa nini uliwatishia maofisa Uhamiaji kwa kisu?

Mshtakiwa: Samahani sana mheshimiwa. Naomba unisamehe. Nilijua walikuwa matapeli. Naomba mahakama inipunguzie adhabu.

Baada ya majibu ya mshtakiwa, wakili Nyarata amesema upande wa mashitaka hauna kumbukumbu ya makosa ya nyuma dhidi yake. Ameiomba mahakama itoe adhabu kali.

Hakimu Lyamuya ndipo alipotoa hukumu akimtaka mshtakiwa kulipa faini hiyo au kutumikia kifungo jela.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa anadaiwa Juni 4, 2024 katika jengo la Sophia House lililopo Keko, wilayani Temeke alikutwa akiishi nchini, huku viza yake ikiwa imeisha muda tangu Desemba 26, 2023.

Anadaiwa pia kutokuwa na nyaraka yoyote inayoonyesha uhalali wake wa kuishi nchini.

Shitaka la pili, anadaiwa siku na eneo hilo, aliwazuia maofisa wa Uhamiaji wasifanye kazi zao wakati walipokwenda kufanya ufuatiliaji wa hati yake ya kusafiria katika ofisi yake na kuwatishia kuwachoma kisu.

Katika shitaka la tatu, anadaiwa siku na eneo hilo alikutwa akifanya biashara wakati akiwa hana kibali cha kuishi nchini kinyume cha sheria.

Mshtakiwa amelipa faini na kukwepa adhabu ya kwenda jela miezi 36.

Related Posts