Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema msingi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuongeza utoaji wa gawio ni uwekezaji uliofanywa katika uendeshaji wa bandari kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Katika kauli yake hiyo, Rais Samia amesema kelele zilizokuwa zinapigwa kupinga uwekezaji wa Kampuni ya DP World katika bandari ya Dar es Salaam, matokeo yake ndiyo faida inayoonekana.
Mzizi wa kauli ya Mkuu huyo wa nchi ni hatua ya TPA kuongoza katika utoaji gawio kwa mashirika ya Serikali yanayopaswa kuchangia silimia 15 katika mfuko mkuu wa hazina.
Katika gawio hilo, TPA imetoa Sh153 bilioni ikiziongoza Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) na Mamaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Sakata la uwekezaji wa sekta binafsi katika Bandari hiyo liliibua upinzani mkali na hoja zaidi zilielekezwa kwenye kasoro za masharti ya mkataba wa nchi na nchi (IGA).
Miongoni mwa kasoro hizo, ni kukosekana ukomo wa mkataba, kadhalika mashauri kati ya pande mbili iwapo zitahitalifiana yaamriwe na mahakama za nje ya Tanzania.
Rais Samia amesema hayo jijini Dar es Salaam leo, Juni 11, 2024 alipopokea gawio kutoka mashirika ya Serikali na yale ambayo yanamiliki hisa chache.
Mkuu huyo wa nchi amesema kutokana na mageuzi yaliyofanyika katika eneo hilo, anatarajia mwakani TPA itatoa gawio mara mbili ya lile la mwaka huu.
“Wale waliopiga kelele, mama kauza bahari, mama kauza bandari, mama kauza hili, mama kauza lile, mauzo yale faida yake ni hii leo,” amesema.
Hata hivyo, amesema faida hiyo ni mwanzo na kuna matarajio ya kupata faida kubwa zaidi katika mwaka ujao.
Amesisitiza kiwango kilichofikiwa na TPA ni matokeo ya mageuzi yaliyofanyika katika eneo la bandari hasa ya Dar es Salaam.
“Na mwakani tunatarajia kiwango kikubwa zaidi ya kile kisichopatikana mwaka huu, hakuna sababu kama mtaendesha na sekta binafsi iliyopo pale,” ameeleza.