Safari treni ya SGR kuanza Dar-Moro Juni 14

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetangaza kuanza kwa safari za treni ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kuanzia Ijumaa ya Juni 14, 2024.

Kuanza kwa safari hizo kunafanyika karibu wiki mbili kabla ya siku ambayo Rais Samia Suluhu Hassan atazindua rasmi safari ya treni hiyo, Juni 25, mwaka huu.

Hata hivyo, safari hizo za treni zitaanza ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya muda ambao Rais Samia Desemba 31, 2023 aliiagiza TRC kuhakikisha treni hizo zinaanza kusafirisha abiria kuanzia Julai mwaka huu.

Kwa mujibu wa TRC, mwanzo wa safari hizo ni ishara ya kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji, itakayochochea ukuaji wa uchumi wa kanda.

Hayo yalielezwa leo Jumatano Juni 12, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa wakati wa kampeni ya uzinduzi wa huduma za uendeshaji wa SGR, iliyopewa jina la “Twende tupande treni yetu, tuitunze, tuithamini.”

“Tumezindua kampeni iliyopewa jina la kuhamasisha watu wengi zaidi kusafiri kwa treni, ili wakati wa operesheni rasmi za reli ya SGR kutoka Dar es Salaam -Dodoma watu wengi zaidi waifahamu na itazinduliwa Juni 25 na Rais Samia,” amesema.

Amesema TRC imeanza na Dar es Salaam- Morogoro kama hatua ya awali zitakazowezesha kupata uzoefu na kutatua changamoto zitakazojitokeza, ili kuboresha safari zitakazoendelea.

Katika kauli yake hiyo, Kadogosa amesema nauli za treni hiyo kutoka Dar es Salaam-Dodoma, kwa daraja la uchumi ni Sh70,000, biashara Sh100,000 na daraja la kibiashara la kifalme ni Sh120,000.

“Kulingana na mahitaji ya soko la wateja, TRC imepanga kuanza na treni mbili kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na Dodoma hadi Dar es Salaam kila siku,” amesema.

Kuhusu usalama, amesema utakuwepo wa uhakika kwa kuwa vichwa vya treni hizo vimefungwa CCTV Kamera zitakazowezesha abiria kufuatiliwa akiwa ndani na wakati wa kushuka.

Ameeleza doria hiyo itafanywa katika safari yote, ili kudhibiti wale wasio waaminifu kuhatarisha usalama kwa namna yoyote.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TRC, Jamila Mbarouk ameliambia Mwananchi kuwa njia ya Dar es Salaam – Morogoro itaanza na nauli zilizotangazwa hivi karibuni na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra).

Kwa mujibu wa Latra, nauli za safari ya treni hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa watu wazima na watoto wenye umri wa zaidi ya miaka 12 ni Sh13,000 huku watoto wa chini ya miaka minne watalipa Sh6,500 kwa daraja la kawaida.

Ofisa Biashara wa TRC, Lilian Mselle amesema njia mbalimbali zitatumiwa na abiria kununua tiketi ikiwemo Gepg (control number), Visa au Master card na kupitia mitandao mbalimbali ya simu.

“Hatua hii inalenga kupunguza malipo ya fedha ya mkono kwa mkono na kuhamasisha malipo kwa njia ya mtandao. Chakula kitauzwa kwenye vituo kwa bei nafuu kwa, sababu hiyo hakuna abiria atakayeruhusiwa kuingia kwenye treni na chakula,” amesema.

Watakaoruhusiwa kuingia na vyakula ni wanawake wanaonyonyesha na vyakula hivyo vinapaswa kuwa vya watoto wenye umri wa kuanzia miezi sita hadi mwaka mmoja.

Amesema katika daraja la biashara, abiria ataruhusiwa kubeba mzigo wa kilo 20 bure.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Miyaho amesema wameamua kushirikiana na TRC kuhakikisha wanaleta mapinduzi katika sekta ya uchukuzi.

“Tumeshirikiana na TRC kwa kukusanya nauli. Tuna matumaini kwamba kila mtu ataangalia SGR kama fursa ya kuwekeza,” amesema.

Mkuu wa Mradi wa Yapi Merkezi, Mehmet Firat amesema kuanza kwa safari hizo ni historia, kwani ni mradi walioanza kujenga tangu awali.

“Tumejenga SGR kutoka Dar es Salaam-Morogoro na kila kitu kimekamilika, tunatarajia itatumika kukuza uchumi wa nchi,” amesema.

Kwa mujibu wa Mehmet, Tanzania imejenga SRG bora zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa ni hatua kubwa kwa wananchi wake na sekta binafsi kuitumia.

Related Posts