Serikali yamaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu

Dodoma. Serikali ya Tanzania imemaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Kitulo,  Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na wananchi wa kata za Ilungu, Igoma na Inyala.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dustan Kitandula ameyasema hayo leo Juni 12, 2024 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Oran Njeza.

Njeza amehoji ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya Tanapa, Kitulo, TFS na wananchi wa kata za Ilungu, Igoma na Inyala.

Akijibu swali hilo, Kitandula amesema Serikali kupitia kamati ya usalama ya Wilaya ya Rungwe na uongozi wa kata zinazopakana na Hifadhi ya Taifa Kitulo imefanya mikutano 15 kati ya Mei 17, 2023 na 9 Novemba, 2023.

“Mikutano hiyo ililenga kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi, dhana ya ujirani mwema na kuwashirikisha katika juhudi za pamoja za kutambua mipaka ya hifadhi kwa faida za hifadhi, jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Amesema kutokana na mikutano hiyo, mgogoro huu umemalizika.

Kitandula amesema katika kuendeleza mahusiano mema na jamii zinazozunguka hifadhi, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Tanapa kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mbeya imepanga kuweka vigingi kwenye mpaka wa hifadhi.

Amesema vigingi hivyo vitawekwa umbali wa kilomita 82 katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kurahisisha utambuzi wa mipaka ya hifadhi na vijiji.

Katika swali la nyongeza Njeza amesema wananchi hao wamekuwa vinara wa utunzaji mazingira na kuwa walinzi kuliko askari je, wizara haioni muhimu sasa kushirikiana na wananchi kwa kutoa misaada ya CSR (Uwajibikaji kwa Jamii) kwa ajili ya kuwashirikisha ili kuwapa motisha wa kutunza mazingira,”amesema.

Akijibu swali hilo, Kitandula amesema wizara kupitia taasisi zake wana mpango wa ujirani mwema katika maeneo yanayozunguka hifadhi zao.

“Niwaagize wataalamu wetu walioko uwandani waende katika maeneo yanayozunguka hifadhi hii wakafanye kazi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uibuaji wa miradi ya kijamii kusudi miradi hiyo iweze kupata ufadhili,” amesema.

Naye Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Francis Ndulane amehoji ni lini Serikali itamaliza mgogoro baina ya pori la akiba la Selous na Kijiji cha Mtepela.

Akijibu swali hilo, Kitandula amesema utatuzi wa migogoro ni mchakato na alivyokuwa anazungumza kuna utatuzi wa migogoro uliokuwa unaendelea.

“Namuomba mheshimiwa mbunge kuwa na subira tukamilishe kazi ili tuweze kuondokana na changamoto hii,”amesema.

Naye Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga amehoji ni lini Serikali itamaliza mgogoro baina wananchi na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro unaohusisha kitongoji cha Isera kilichopo katika Kijiji cha Ndolezi na eneo la Kimondo.?

Akijibu swali hilo, Kitandula amesema utatuzi wa migogoro ni mchakato na kuomba wabunge kutoa fursa kwa Serikali ili iweze kushughulikia migogoro hiyo na kuimaliza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbarali (CCM), Bahati Ndingo amesema mgogoro kati TFS na Kijiji cha Kapyo, Wilaya ya Mbarali ulishamalizika baada ya wataalamu wa TFS kukaa na wataalam wa halmashauri na wanakijiji.

Hata hivyo, amesema kinachosubiriwa kutoka wizarani ni barua ambayo itawaruhusu wanakijiji kuendelea na shughuli zao.

Akahoji ni lini watapata barua hiyo ili waendelee na shughuli zao?

Akijibu swali hilo, Kitandula amewaagiza uongozi wa TFS kwa haraka sana watoe barua hiyo ili wamalize jambo hilo.

Related Posts