Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Shirika la Ujerumani la GIZ na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania [JET] wameungana kwa pamoja kutoa elimu inayolenga kujenga uelewa wa pamoja kwa waandishi wa habari kuhusu changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika mafunzo yaliyofanyika leo katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Mratibu wa Mradi wa kutatua changamoto hiyo, unaotekelezwa katika katika Wilaya ya Liwale (Mkoa wa Lindi), Namtumbo na Tunduru (Mkoa wa Ruvuma), Bw. Gideon A. Mseja amesema, changamoto hiyo ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo imekuwa kubwa kwa na kusababisha madhara makubwa kwa jamii na wanyamapori.
Amesema kufuatia changamoto hiyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya doria na kujenga vituo vya askari wa wanyamapori katika maeneo ya wananchi, kuwezesha vifaa vya kuondoa tembo maeneo ya wananchi, kufuatilia miendendo ya wanyamapori, kutumia helikopta na mabomu baridi kuwaondoa tembo kwenye makazi, kuwezesha wananchi kiuchumi na kutoa elimu ya tabia ya tembo na mbinu ya kutatua migongano hiyo kwa jamii ili kujenga uhimilivu wa matukio hayo.
”Serikali imejitahidi kuhakikisha kwamba maeneo yote yenye changamoto kubwa katika wilaya 44 yanapewa kipaumbele ili kulinda Maisha na mali za wananchi” amesema Mseja
Bw.Gideon ameongeza kuwa katika hatu nyingine Serikali imeanzisha Mradi wa ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani ili kutatua migongano hiyo kwenye ukanda wa Ruvuma. Pamoja na malengo mengine, Mradi wa Kutatua Migongano Baina ya Binadamu na Wanyamapori umelenga kutoa elimu ya namna sahihi ya kuandika na kutoa habari sahihi zinazohusiana na migongano hii kwa waandishi wa habari. Shughuli hii ya kutoa elimu inatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) ambapo Kitaifa mafunzo yalizinduliwa Bagamoyo, Mkoani Pwani na sasa Mkoani Ruvuma katika Wilaya ya Tunduru.
”JET tumewakasimisha jukumu la kutekeleza sehemu ya malengo ya Mradi huu na kwa kuwa wao ni mabingwa wa habari za mazingira tunategemea matokeo makubwa na habari nyingi zenye ubora.”
Kwa Upande wake Mtaalam Mshauri wa Mradi hasa kwenye eneo la elimu ya utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa GIZ, Bi. Ana Kimambo amesema waandishi hao wanapatiwa mafunzo hayo ili wanapoenda kwenye Jamii waweze kuielimisha kwa ufasaha
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma yamehudhuriwa na Waandishi wa Habari takribani 10 kutoka vyombo mbalimbali vya habari kutoka maeneo ya mradi ikiwemo wawakilisha kutoka Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na baadhi ya Maafisa Habari wa Serikali kutoka maeneo hayo.