Simu janja kurahisisha uboreshaji daftari la kudumu wapigakura

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza utaratibu mpya wa maboresho ya Daftari la Kudumu la wapigakura ambapo mpigakura ataweza kutumia simu janja kuhamisha taarifa zake au kuhama kituo.

Akizungumza leo Juni 12,2024 na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura Mkuu wa Dawati la Tehama INEC, Stanslaus Mwita, amesema mpigakura anaweza kuanzisha mchakato mtandaoni kurahisisha uboreshaji wa daftari hilo.

Kulingana na tume hiyo, kupitia simu janja mpigakura anaweza kurekebisha au kubadili taarifa binafsi na kuhama kituo kisha atatakiwa kutembelea kituo kilicho karibu kupata kadi yake.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakara ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Naye Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakara ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, amesema uboreshaji huo utazinduliwa Julai Mosi mwaka huu mkoani Kigoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Amesema katika uboreshaji huo Teknolojia ya kumtambua mtu na kumtofautisha na mwingine (BVR) itatumika ambapo sasa imeboreshwa kwa kuwekwa programu za kisasa zaidi na kupunguzwa uzito ili ziweze kubebeka kirahisi.

“Vyombo vya habari viwafikishie wananchi taarifa sahihi na kwa wakati na kuwahamasisha wananchi wenye sifa wajitokeze kwa wingi kujiandikisha,” amesema Jaji Mwambegele.

Aidha amesema Novemba 24 hadi 30 mwaka 2023 walifanya majaribio ya uboreshaji daftari hilo katika Mikoa ya Tabora na Mara ili kupima uwezo wa vifaa na mifumo itakayotumika ambapo lilifanyika kwa mafanikio.

Hata hivyo amesema kulijitokeza changamoto kadhaa kwa baadhi ya wapigakura kusahau majina yao waliyojiandikisha awali na kuchukua muda mrefu vituoni kutokana na ugumu wa kupata taarifa zao kwa haraka.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, amesema wanatarajia kuandikisha wapigakura wapya, wanaoboresha taarifa zao, wanaohama vituo, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kuondoa taarifa za wapigakura waliopoteza sifa za kuwepo katika dafrati.

Related Posts