Ukimya wa Polisi tuhuma za  RC kumlawiti mwanafunzi gumzo

Mwanza/Dar. Ukimya wa Jeshi la Polisi uliotanda kuhusu tuhuma zinazomkabili mkuu wa mkoa mmoja wa Kanda ya Ziwa, anayetuhumiwa kumlawiti mwanafunzi umegeuka gumzo mitandao ya kijamii.

Tukio hilo limeibua mijadala maeneo mbalimbali, hususan mitandoni kuanzia juzi, baadhi ya wachangiaji kwenye mjadala huo wakilitaka Jeshi la Polisi kutoa tamko na kumfikisha mhusika kwenye vyombo vya sheria.

Mwananchi juzi na jana hadi linakwenda mitamboni, limekuwa likiwatafuta viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani, kutaka kujua hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.
Msemaji wa Jeshi Polisi, David Misime mwenye dhamana ya kulisemea jeshi hilo simu yake ilikuwa inaita bila kupokewa tangu juzi. 

Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya WhatsApp, ulionyesha kupokewa lakini hakutoa mrejesho wowote.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai hawakupatikana kupitia simu zao kuzungumzia suala hilo, hivyo hivyo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni.

Hata mkuu wa mkoa  mwenyewe anayetuhumiwa  alipotafutwa hakupatikana kujibu tuhuma dhidi yake, kuhusu tukio hilo linalodaiwa kutokea mkoani Mwanza.

Juzi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ambaye juzi alisema hakuwa na taarifa na anafuatilia, jana alipopigiwa simu hakupokea wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi.

Hata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa ambaye juzi alisema yupo kwenye msiba, jana simu yake ilipopigwa mara kadhaa,  iliita bila kupokewa.

Viongozi hao wanatafutwa kuzungumzia taarifa ambazo Mwananchi ilizipata kutoka kwa vyanzo mbalimbali kwamba mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza, baada ya mkasa huo alikwenda kutoa taarifa Jeshi la Polisi-Dawati la Jinsia na Watoto na jeshi hilo limefanya hatua kadhaa za awali za kipelelezi.

Inadaiwa baada ya kutoa taarifa Juni 3 mwaka huu na kupelekwa Hospitali ya Sekou Toure kwa uchunguzi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza lilituma taarifa za awali juu ya tukio hilo kwa DCI Kingai, ambaye hata hivyo hajasema lolote.

Ukimya huo umechochea mjadala mkubwa mitandaoni na kuhoji kwa nini jeshi hilo linasuasua kuchukua hatua.

Baadhi wamekwenda mbali zaidi na kueleza ukimya huo wa polisi, unachochea kuendelea kutendeka vitendo hivyo kwenye jamii.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kutoka vyanzo mbalimbali jijini Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam, vimedokeza uchunguzi wa suala hilo unafanywa kwa usiri mkubwa na kumekuwapo na njama za kutaka kufifisha suala hilo kimyakimya.

Jana, Mwananchi ilifika Hospitali ya Sekou Toure alipopelekwa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21 na kupata fursa ya kuzungumza na mmoja wa viongozi (jina tunalihifadhi) aliyekiri kupokelewa kwa mwanafunzi huyo na kupatiwa matibabu.

Kiongozi huyo alisema mwanafunzi huyo alipokewa Juni 3 mwaka huu. Hata hivyo, hakutaka kuzungumza kwa kina kwa kile alichokieleza taarifa za mgonjwa ni siri baina ya daktari na mgonjwa.

Katika toleo la jana la gazeti hili kupitia vyanzo vyake lilielezea jinsi mkuu huyo wa mkoa alivyokutana na binti. Lilieleza kuwa mtuhumiwa huyo alianza uhusiano na mwanafunzi huyo Januari, 2024 jijini Mwanza.

Siku hiyo walikutana katika tafrija ya siku ya kuzaliwa ambayo mtuhumiwa anatajwa ndiye alikuwa mgeni rasmi na hapo ndipo walipobadilishana namba za simu na kuanzisha uhusiano na kuendelea kuwasiliana kwa simu mara kwa mara.

Chanzo hicho kimedai siku hiyo kigogo huyo alikutana na dada huyo katika moja ya hoteli jijini Mwanza, ambapo katika hali ya kustaajabisha, alimuomba wafanye mapenzi kinyume cha maumbile, ombi ambalo dada huyo alilikataa.

Inadaiwa kigogo huyo, aliendelea kumshawishi akubali kufanya naye mapenzi kinyume cha maumbile kwa ahadi kuwa angempa maisha mazuri.

Chanzo kimoja kutoka ofisi ya kigogo huyo, kilidai siku ya tukio, mtuhumiwa alitumia kila mbinu kumshawishi mwanafunzi huyo wakutane jijini Mwanza, ambapo walikutana katika baa hiyo mashuhuri na kupata vinywaji.

“Sasa baada ya muda huyu jamaa akamuambia wakazungumze kwenye gari maana kuna mambo ya muhimu anataka kumweleza. Huko sasa jamaa ndio akashinikiza wafanye kinyume cha maumbile,” kilidokeza chanzo hicho.

Chanzo kingine kilidai kigogo huyo na gari alilolitumia vilinaswa na kamera za usalama zilizofungwa katika klabu hiyo tangu gari hiyo inaingia, kuegeshwa na kutoka usiku wa saa sita na namba za usajili zilisomeka vizuri.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, kamera zinaonyesha ilipofika saa 2:48 usiku, binti huyo alionekana akiingia katika gari hilo na saa 3:21 usiku, takribani baada ya dakika 30 kupita, mlalamikaji alionekana akitoka kwenye gari.

Saa 6:24 usiku, zinaonesha gari hilo lilionekana katika geti la kutokea likiwa eneo la mwanga mkali uliowezesha kulitambua usajili wake. Dereva wa gari hilo alikuwa amevalia kofia aina ya kapelo akitoka kwenye gari hilo kwa ajili ya kulipia ushuru wa maegesho.

Taarifa zinadai, Juni 3 mwaka huu, siku moja tangu alipofanyiwa ukatili huo, binti huyo alikwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi-dawati la jinsia na watoto, jijini Mwanza. Alisikilizwa, kisha kupelekwa moja ya hospitali kubwa jijini hapo kwa uchunguzi.

Related Posts