RAIS Samia Suluhu Hassan amesema licha ya kupigiwa kelele kuwa ameuza bandari baada ya kuruhusu wawekezaji wawili kwenye bandari ya Dar es Salaam, tayari faida imeonekana kutokana na gawio lililotolewa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akitoa pongezi maalumu kwa kampuni zilitoa gawio kwa Serikali leo Jumanne, Rais Samia amesema TPA imetoa mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi kwa serikali kwa mujibu wa sheria katika kiwango ambacho ni tofauti na mwaka jana.
Bila kutaja kiwango amesema; “mwaka jana level yenu hamkuwa hivyo ila kwa mageuzi yaliyofikiwa bandarini mmeweza kufikia kiwango hiki, mwakani tunatarajia kiwango kikubwa zaidi,” amesema.
Amesema kwa kuwa sasa katika bandari hiyo kuna wawekezaji wawili akiwamo DP World, katika mwaka ujao wataweza kuongeza kiwango zaidi.
“Waliopiga kelele, mama kauza bahari, kauza bandari mama kauza nini… mauzo yale faida yake ni hii na huu ni mwanzo, tunatarajia kupata faida kubwa zaidi kwa bandari zote kubwa,” amesema.