Dar es Salaam. Mkazi wa Mikocheni, Elizabeth Timasi (76) na wenzake wanne, wamefikishea katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kujibu mashtaka matatu, likiwamo la kuvunja duka na kuiba mali yenye thamani ya Sh892 milioni.
Mbali na Timasi ambaye ni mfanyabiashara, washtakiwa wengine ni daktari Suzan Charles (52), Neema Timasi (43), mfanyabiashara, Jonathan Masanga (76) na Emmanuel Kasonjola (40).
Wamesomewa mashtaka leo Juni 11, 2024 na Wakili wa Serikali, Violeth David mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Nabwike Mbaba.
David amedai washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 15603 ya mwaka 2024.
Katika shtaka la kwanza la kuvunja duka wanadaiwa kwa pamoja kulitenda Aprili 29, 2024 eneo la Mwenge wilayani Kinondoni.
Inadaiwa kwa nia ya kutenda kosa walivunja duka la nguo mali ya Lilian Macha.
David katika shtaka la pili la wizi amedai washtakiwa walilitenda Aprili 29, 2024 eneo la Mwenge wakiiba mali kadhaa zikiwamo suruali 238 aina ya kadeti na 247 za jeans.
Pia, wanadaiwa kuiba suruali za aina tofauti 1,468 na kaptura 334 aina ya jeans na kadeti.
Wanadai pia, kuiba nguo za ndani za kiume 859, mashati ya ofisi 1,953, suti 837, kaunda suti 234, makoti 769, masweta 759, vesti 564, taulo 48, soksi 910 na fulana 2,341.
Washtakiwa wanadaiwa kuiba jozi 82 za miwani, raba 1,407, pochi ndogo (wallet) za ngozi 82, kofia 162, viatu 915, makubadhi 289 na ndala 137.
Pia, wanadaiwa kuiba fedha tasilimu Sh70 milioni, Dola za Marekani 50,000 (Sh130.5 milioni). Thamani ya mali iliyoibwa amedai ni Sh892.82 milioni.
Katika shtaka la tatu wanadaiwa kuharibu mali kwa makusudi dukani hapo.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka walikana kuyatenda.
Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo kuomba tarehe kwa ajili ya kuwasomewa hoja za awali (PH).
Mahakama imetoa dhamana kwa washtakiwa kwa masharti kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria wenye barua kutoka Serikali za mitaa. Pia, wanatakiwa wawe na kitambulisho cha Taifa (Nida).
Kila mdhamini anatakiwa kuwasilisha fedha tasilimu Sh80 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Washtakiwa wametimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Julai 4, 2024.