Dar es Salaam. Wito wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa viongozi wa vyama vya siasa kujadili kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa umezua mvutano miongoni mwa wadau kabla ya mjadala wenyewe.
Baadhi ya vyama vya siasa vimekosoa hatua hiyo kwa kuwa wito huo haukuambatana na rasimu ya kanuni hizo ili waweze kuzipitia kabla, badala ya kwenda kukutana nazo kikaoni jijini Dodoma.
Juni 10, 2024 Tamisemi ilituma barua za mwaliko kwa vyama vya siasa kupitia Ofisi ya Msajili wa vyama hivyo, ikiwataka wenyeviti, makatibu wakuu na viongozi wa jumuiya za wanawake za vyama hivyo, kufika Dodoma Juni 15, 2024 kwa ajili ya kujadili kanuni hizo.
Baada ya kupata wito vyama vya siasa vilivyozungumza na Mwananchi – ACT Wazalendo, Chadema na NCCR-Mageuzi vikosoa mwaliko huo wa Tamisemi kwa udhaifu huo.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka wanachama wake kutoa maoni kuhusu mwaliko wa Tamisemi kwenda kwenye mkutano huo bila kutoa rasimu ya kanuni.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika kupitia mtandao wa X, imesema chama hicho kiliomba rasimu za kanuni hizo lakini hakijapewa.
“Kwa kuwa uchaguzi huu unahusu mitaa na matawi ya chama Tanganyika nzima sanjari na umma tunaowaongoza, nimeona niwaandikie ujumbe huu ili mfahamu na mtafakari kuhusu mwaliko na mchakato huu unaoendelea na mtupe maoni na ushauri wenu wa haraka juu ya hatua za kuchukua, nikizingatia kuwa chama ni wanachama, vikao na uongozi.
“Nasubiria mrejesho wenu kwa wakati nikiwatakia heri katika majukumu yenu na mapambano ya haki, uhuru, uadilifu, demokrasia na maendeleo ya watu,” ameandika Mnyika.
Naye Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini amesema kanuni hizo zimecheleweshwa na mpaka sasa vyama havijui ratiba ya uchaguzi.
“Pamoja na mchakato kutokujulikana mapema, zamani walikuwa wanatuletea rasimu ya kanuni mapema ili tuijadili pamoja na wataalamu ndani ya vyama, halafu tunapokutana tunakuwa na mapendekezo.
Wakati vyama hivyo vikilalamika kutotumiwa rasimu ya kanuni, Mkurugenzi wa Mawasiliano Serikalini wizara ya Tamisemi, Ntenghenjwa Hosea alisema rasimu hizo zimeshatumwa.
“Rasimu zimetumwa tangu jana,” amesema.
Chama cha ACT- Wazalendo kimekwenda mbele zaidi kikitangaza kusudio la kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga kuendelea na mchakato wa kuchukua maoni ya maboresho ya kanuni ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu.
Mbali na hilo, ACT Wazalendo pia kimepanga kuwasiliana na vyama vingine vya siasa kuvisihi vichukue hatua za pamoja na visiwe tayari kutoa maoni ya maboresho ya kanuni hizo kwa Tamisemi kwa madai kuwa haijapewa mamlaka hayo kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Julai 12, 2024, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema tayari wameshawasiliana na asasi za kiraia kwenda kufungua kesi.
“Bahati nzuri tumepata mrejesho mzuri kutoka kwa asasi wa kiraia, na maandalizi ya kufungua kesi hiyo yamekamilika na hivi karibuni tutafanya hivyo na ACT Wazalendo tutatoa ushirikiano na kama wakichelewa tutaenda wenyewe,” amesema Ado.
Ado amesema kufuatia hali inayoendelea na unyeti wa jambo hilo chama hicho kitawasiliana na vyama vingine makini nchini, kuona umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja ili kuzuia mchakato wa Tamisemi.
“Na tutashinikiza wajumbe wa sasa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wajiuzulu kwa sababu hawajapatikana kwa kuzingatia utaratibu ulioainishwa na sheria mpya ya Tume huru ya Uchaguzi,” alisema.
Licha ya kususia utoaji wa maoni kwa ajili ya kanuni hizo, Ado amesema watakwenda kwenye mkutano wa Tamisemi jijini Dodoma ili kuwaeleza kuwa wasimamishe mchakato huo.
“Kwa sababu ni kinyume na sheria za nchi, tutakwenda kuiuliza Tamisemi maboresho ya kanuni yanafanyika kwa mujibu wa sheria ipi,” amesema.
“Hiki kinachofanywa na Tamisemi kinavunja sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na inakuwa batili na kinyume na Katiba ya nchi,” alisema.
Hata hivyo, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ibara ya 10 (1)(c) akisema moja ya majukumu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi “ni kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za vijiji, mitaa na vitongoji Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika sheria itakayotungwa na Bunge.”
Alipoulizwa jana Jumanne, kuhusu kutungwa kwa sheria hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi alisema: “Sheria itatungwa, mchakato wake ukianza kwa mujibu wa sheria na taratibu.”