ALIYEKUWA mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole amerejea hapa nchini baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili aliousaini na kikosi cha FC Lupopo cha DR Congo alichojiunga nacho Desemba mwaka 2022 baada ya kuonyesha kiwango kizuri.
Mpole ambaye anakumbukwa zaidi kutokana na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021-2022 baada ya kufunga mabao 17, amepata nafasi ya kupiga stori na Mwanaspoti na kuelezea alivyoziingiza vitani Yanga, Simba na mipango yake mipya.
“Nimefurahi kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi kwa sababu kuna mambo mengi nimejifunza tofauti na mchezaji aliyekuwa hapa nchini, unapotoka ndipo unapojifunza mazingira ya utofauti na ulipozoea hivyo inakujenga sana kiakili,” anasema.
CONGO HUTHAMINI WACHEZAJI WAO
Mpole anasema moja ya jambo la utofauti alilokutana nalo katika nchi ya Congo ni kuona jinsi wanavyothamini wachezaji wao tofauti na wanaotoka nje, kitu ambacho ni tofauti kabisa na Tanzania kwa sababu sisi tunawapa thamani wageni zaidi.
“Wakati Tanzania tukiwapamba wachezaji wa nje katika vyombo vyetu vya Habari, kwa wenzetu Congo ni tofauti kwa sababu wanaangalia wa kwao kwanza, kuna kipindi nilifunga bao ndipo wakaanza kunizungumzia ila kiufupi wako bize na vyakwao.”
“Congo hakuna uhuru mzuri kama huku kwetu ndio maana mchezaji akitoka kule akija anatamani kubakia, mbali na hivyo ila malipo ni mazuri jambo ambalo huvutia wachezaji wengi na hutoona nyota wetu wakimiminika sana mataifa ya nje,” anasema.
Anasema, kwa sasa licha ya kwamba yupo mapumzikoni ila kuna ofa nyingi ambazo zinamfanya kutulia zaidi kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho kujua ni klabu gani ataichezea kwa msimu ujao, kwa sababu hataki kukurupuka kwanza.
Wakati Yanga ikiwa katika harakati za kukamilisha usajili wa beki wa kushoto wa FC Lupopo, Chadrack Boka, Mpole anasema mashabiki watarajie mambo makubwa kutoka kwake, kwani jamaa anajua japo tusubiri kwanza hadi atakapokuja hapa nchini.
“Nimecheza naye na namjua vizuri, ni mchezaji mzuri kwa sababu anacheza timu kubwa, watu watamuona wenyewe atakapokuja kwa sababu shida yetu Watanzania tunapenda sana kujadili vitu kabla ya kuviona hivyo watakapomuona watamuongelea zaidi.”
“Kabla ya kwenda Congo ni kweli viongozi wa Yanga na Simba walinifuata wakinihitaji ila niliamua kwenda nje kwanza kwa sababu niliamini ni sehemu nzuri kwangu,” anasema
“Wakati najiunga na Lupopo nilipitia kipindi kigumu sana kwa sababu ya changamoto ya lugha, wenzangu hawajui Kiingereza wala Kiswahili zaidi ya kuongea Kifaransa tu hivyo ilinichukua miezi mitatu hadi minne ili kuelewana nao japo kidogo.”
Wakati Ligi Kuu Bara ikiwa imeisha huku mjadala mkubwa ukibaki kwa nini viungo wameonekana kufanya vizuri zaidi tofauti na washambuliaji, nyota huyo ametoa maoni yake huku akiweka wazi amefurahishwa na jinsi wachezaji wazawa walivyopambana.
“Nawapongeza, Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa (Azam FC) na Waziri Junior wa KMC kwa sababu wamepambana sana, binafsi naamini kama tungekuwa tunawapa promo zaidi wachezaji wetu wazawa wangefika mbali ila shida yetu ni ileile ya kuthamini wa nje.”
Mpole aliongeza, sababu ya washambuliaji kutofanya vizuri msimu uliopita tofauti na viungo huenda imechangiwa na ubora wa mabeki.
“Sijafuatilia sana Ligi ya hapa ila huenda hao washambuliaji walikuwa wanatoa nafasi za kufunga kwa viungo ndio maana wameonekana bora, jambo kubwa kama nilivyosema awali tupende na kuthamini vya kwetu, naamini tuna uwezo mkubwa sana.”
NJE YA SIMBA, YANGA SIO MCHEZO
Mpole anasema, sio rahisi kuibuka mfungaji bora ukiwa timu nje ya Yanga na Simba kwa sababu ya ukubwa wa wachezaji bora waliopo wanaoweza kukutengenezea nafasi japo kama mchezaji unayejua thamani yao utapambana bila kuangalia ni wapi ulipo.
“Kwa mfano mimi wakati nipo Geita Gold, hakuna aliyetarajia kama ningeibuka mfungaji bora hasa ukiangalia jinsi ambavyo nilipambana na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele japo niliamini katika upambanaji na wala sio vinginevyo.”
Nyota huyo aliwahi kuhusishwa kuogopa kupanda ndege wakati akiichezea Geita Gold na hata michezo ya timu hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika ya ugenini alikuwa hasafiri; “Watanzania tunapenda sana kuongea mambo ya uongo kwa sababu unajiuliza mimi naogopa vipi kupanda ndege? mashabiki zangu wanapaswa kutambua wakati nipo Lupopo mechi nyingi tumekuwa tukisafiri kwa usafiri huo sasa nilishangaa kuzushiwa hilo.”
AITAHADHARISHA COASTAL UNION
Mpole ameipongeza timu ya Coastal Union kwa kumaliza nafasi ya nne. “Watambue wanaenda kukutana na timu kubwa zaidi yao hivyo wanatakiwa kujipanga kuanzia maandalizi mazuri kwa maana ya kufanya usajili wa wachezaji bora ambao watawasaidia, wameonyesha inawezekana na wanatakiwa kuipambania nchi kimataifa.”
Nyota huyo amesikitishwa na kitendo cha timu aliyoichezea ya Geita Gold kushuka daraja baada ya kuandamwa na matokeo mabaya tangu mwanzoni huku akiwataka viongozi kujipanga upya na kuangalia ni wapi walipoteleza ili warudi wakiwa imara.
“Inasikitisha kwa sababu kushuka sio ishu ila ni jinsi gani utaipandisha hapo ndipo kuna kazi, kikubwa waangalie namna nzuri ya kuirudisha kwani naamini kama wataweka nguvu zaidi na wakaendeleza umoja na mshikamano wataipandisha tena.”