Akizungumza katika bunge la Ujerumani, Bundestag, Jumanne (11.06.2024) rais Zelensky amewaambia wabunge wa Ujerumani kwamba sasa wanaweza kuelewa kwa nini WaUkraine wanapambana sana dhidi ya juhud za Urusi kuwagawanya, na kuigawa Ukraine.
“Mnayajua haya kutokana na uzoefu wenu wenyewe na ndio maana mnaweza kutuelewa sisi WaUkraine. Mnaweza kuelewa kwa nini tunapigana kwa nguvu nyingi dhidi ya juhudi za Urusi kutugawa na kuigawa Ukraine na kwa nini tunafanya kila linalowezekana kuepusha ukuta kati ya maeneo ya nchi yetu,” alisema Zelensky.
Zelensky ametahadharisha juu ya kuongezeka kwa kauli za kuiunga mkono Urusi barani Ulaya, baada ya vyama vya mrengo wa kulia, baadhi yao vikimuunga mkono rais wa Urusi Vladimir Putin, kupata matokeo mazuri katika uchaguzi wa bunge la Ulaya. Zelensky amesema kauli hizo ni hatari kwa nchi za Ulaya.
Vyama vya mrengo wa kulia na vya msimamo mkali wa mrengo wa kushoto katika bunge la Ujerumani vimeisusia hotuba ya Zelensky bungeni. Sahra Wagenknecht, mkuu wa muungano wa siasa kali za mrengo wa kushoto BSW hakuwepo bungeni, huku wakuu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Chama Mbadala kwa Ujerumani, AfD, wakisema katika taarifa kwamba wanakataa kusikiliza mzungumzaji aliyevalia mavazi ya kujificha uhalisia wake.
Zelensky amesema anatarajia wakimbizi raia wa Ukraine watajerea nyumbani lakini baada ya mapigano kufika mwisho. Rais huyo amesisitiza kuwa haingii akilini kuwahimiza wakimbizi wa Ukraine warejee nyumbani sasa kwa kauli mbiu na kampeni, akisema bila shaka mchakato mzima wa kuijenga mpya nchi hiyo utafanyika baada ya vita.
Soma pia: Scholz arejelea uungwaji wake mkono Ukraine
Zelensky amesema kutakuwa na ari kubwa miongoni mwa raia wa Ukraine waliokimbilia nchi za nje kutaka kurejea na kuijenga upya nchi yao mara tu kutakapokuwa na amani.
Rais Zelensky amedokeza kuwa kutakuwa na ajira nyingi mara tu hilo litakapofanyika, akitambua kwamba tayari kuna mahitaji makubwa ya wafanyakazi wenye ujuzi nchini Ukraine.
Scholz asema Ujerumani itaendelea kuiunga mkono Ukraine
Kwa upande wake kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameelezea matumaini yake kwa uangalifu kuhusu mkutano wa amani kwa ajili ya Ukraine utakaofanyika nchini Uswiwi baadaye mwezi huu, akisema wanajadili kanuni kwa ajili ya amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine.
“Haya si mazungumzo kuhusu mwisho wa vita, kwa sababu rais wa Urusi, Vladimir Putin itabidi aoneshe kwamba yuko tayari kuifikisha mwisho kampeni yake ya kikatili na kuwaondoa wanajeshi wake. Pengine njia inaweza kupatikana kuiwezesha Urusi siku moja ikae kwenye meza ya mazungumzo. Wakati muafaka ukifika, hilo litaamuliwa na Ukraine.”
Kansela Scholzi amesisitiza kwamba ni WaUkraine hawatalazimishwa na washirika wao kuingia kwenye makubaliano. Scholz amesema ilimradi Putin anaendelea na malengo yake ya vita, ujumbe wao utabaki ule kwamba hawatabanduka katika kuiunga mkono Ukraine.
(dpa, afp)