Wajumbe hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi wamefanya ziara mikoa ya Singida, Manyara, Kilimanjaro, Arusha na Tanga kuanzia Mei 29 na kuhitimishwa Juni 8, 2024.
Lengo lilikuwa kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25, kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kuangazia maandalizi ya chaguzi zijazo za serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025.
Dk Nchimbi aliongozana na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, Katibu wa Siasa na Uhusiano ya Kimataifa, Rabia Hamid Abdallah na Katibu wa Idara ya Oganaizesheni, Issa Ussi Gavu.
Katika ziara hiyo, kero zilizoibuliwa zaidi ni migogoro ya ardhi, ubovu wa barabara, masuala ya kilimo, ukamilishaji wa maboma ya afya, elimu, matatizo ya maji na usalama wa raia.
Pia, mauaji kwenye hifadhi, migogoro sekta ya madini, tatizo la umeme pamoja na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Mawaziri waliopewa maelekezo kwa nyakati tofauti na miongoni mwao kupigiwa simu moja kwa moja kutokana na kero hizo kuibuliwa na wizara zao kwenye mabano ni; Mohamed Mchengerwa (Tamisemi), Hussein Bashe (Kilimo), Jerry Silaa (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Angellah Kairuki wa Maliasili na Utalii.
Wengine ni, Jumaa Aweso (Maji), Profesa Adolf Mkenda (Elimu, Sayansi na Teknolojia), Ummy Mwalimu (Afya), Anthony Mavunde (Madini), Innocent Bashungwa (Ujenzi), Hamad Masauni (Mambo ya Ndani) pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko.
Mbali na mawaziri hao, maelekezo mengine yalitolewa kwa wakuu wa mikoa (RC) kwa kusaidiana na wasaidizi wao, wakiwemo wakuu wa wilaya (DC), wakurugenzi, makatibu tawala wa mikoa na wilaya kushuka hadi ngazi za chini kusikiliza kero za wananchi.
Ma-RC hao na mikoa yao kwenye mabano ni; Halima Dendego (Singida), Qeen Sendiga (Manyara), Paul Makonda (Arusha), Nurdin Babu (Kilimanjaro) na Balozi Baltida Burian.
Mchengerwa ndiye aliongoza kupigiwa simu na Dk Nchimbi kutoa ufafanuzi katika mkutano wa hadhara. Alipigiwa mara tatu, huku Aweso akipigiwa mara mbili na Bashe mara moja.
Wengine walipewa maelekezo yao juu kwa juu kwa mtendaji mkuu huyo wa chama tawala kuwataka watekeleze kwa wakati, huku akisisitiza katika moja ya mikutano: “Nitafuatilia kuona kama Serikali inatekeleza maelelezo ya chama.”
Dk Nchimbi alisema Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25 inapaswa kutekelezwa kwa ukamilifu kabla ya chaguzi zijazo pamoja na kero za wananchi zinapatiwa majawabu.
Katika maeneo mbalimbali aliyopita na ujumbe wake, Dk Nchimbi alisisitiza umuhimu wa viongozi wa chama au Serikali wasioguswa na matatizo ya wananchi hawatoshi kwenye nafasi hizo.
Juni 2, 2024 katika eneo la Mijingu, Mkoa wa Manyara, akiwa njiani kutoka Manyara kwenda Arusha, alisema: “CCM kitaendelea kuzisimamia Serikali zake kuona kwamba zinawahudumia wananchi kwa upendo na kwa juhudi na wakati wote hatutasita kuhangaika na kero za wananchi.”
Alhamisi, Juni 6, 2024, Mbunge wa Mwanga (CCM), Joseph Tadayo aliibua changamoto ya Hospitali ya Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro kuhitaji Sh300 milioni ili kuikamilisha na huduma ziweze kutolewa kwa ufanisi.
Kutokana na kero hiyo, Dk Nchimbi aliamua kumpigia simu Mchengerwa, ambaye alisema Serikali inaendelea na ukarabati wa hospitali kongwe 38 nchini na hadi sasa hospitali mpya 128 zimejengwa.
Waziri Mchengerwa alisema mara baada ya mkutano wa Bunge la Bajeti kumalizika atafanya ziara maeneo yote ambayo Dk Nchimbi amepita akiwa na timu yake ili kufuatilia kwa kina changamoto zilizoibuliwa na kuchukua hatua, ikiwemo kutoa fedha.
Pia, Mchengerwa alipigiwa simu Mei 30, 2024 wakati msafara wa Dk Nchimbi uliposimama eneo la Itaja, Singida na wananchi wakaibua changamoto ya ujenzi wa Kituo cha Afya na waziri huyo kuahidi kutuma timu ya wataalamu.
Katika hilo, Dk Nchimbi alitaka ujenzi uanze kabla ya Agosti 2024 na yeye atafika kuweka jiwe la msingi mwezi huo.
Mchengerwa alipigiwa simu pia Mei 29, 2024 wakati msafara huo ulipokuwa Jimbo la Singida Magharibi ambapo mbunge wake, Elibariki Kingu aliibua kero ya ufinyu wa madarasa.
Waziri huyo ameahidi kupeleka fedha ili kujengwe vyumba vya madarasa, huku timu ya wataalamu wakisema ataituma kwenda kuangazia tatizo hilo la wingi wa wanafunzi.
Aidha, sekta ya afya zinaingiliana kati ya Tamisemi ya Mchengerwa na Ummy wa Wizara ya Afya.
Wote wanapaswa kushiriki kuweka mambo sawa kwenye sekta hiyo.
Mchengerwa na mwenzake Silaa wamepewa jukumu la kukutana haraka kuangalia jinsi ya kumaliza mkwamo wa ujenzi wa Soko la Manyema, mkoani Kilimanjaro.
Soko la Manyema ambalo hutumika kuuza samaki wabichi lilikuwa eneo la wazi na kinachohitajika kwa sasa ni kubadilishwa kwa matumizi kutoka eneo la wazi na kuwa eneo la soko.
Kwa sasa Manispaa wameomba kibali cha kubadilisha matumizi ya eneo hilo na baada ya kibali hicho, ujenzi wa soko hilo utaanza na ndicho Mchengerwa na Silaa wanapaswa kukutana.
Waziri Silaa yeye anapaswa kuongeza kasi ya kushughulikia migogoro ya ardhi ambayo katika kila mkutano wa hadhara ama msafara uliposimama kusalimia ziliibuka, zipo zilizo mahakamani.
CCM kimempongeza kwa jitihada anazozifanya tangu aanze kuongoza wizara hiyo na kumtaka kuendelea na kasi hiyo.
Suala la ubovu wa barabara zipo ambazo zipo chini ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) za Mchengerwa na zilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) za Waziri Bashungwa ambazo zote zinapaswa kukamilika.
Kero ya barabara iliibuliwa maeneo mbalimbali na Ijumaa ya Juni 7, 2024, Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Timoth Mzava alisema alitaka kutounga mkono bajeti ya ujenzi ili barabara za maeneo yake zitekelezwe na kumwomba Dk Nchimbi aweke mkono wake ambaye amesema atafanya hivyo.
Waziri Mavunde anapaswa kushughulikia tatizo la uchorongaji kwenye mgodi wa Mirerani.
Pia, uwepo wa maduka ya kuuzia madini ya Tanzanite mkoani Arusha ambayo sasa yanauziwa Mkoa wa Manyara yanapochimbwa.
Agizo hilo lilitokana na Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo kumwomba Dk Nchimbi kuliangalia suala hilo, kwani kuhamishiwa Manyara limeondoa zaidi ya ajira 3,000 za vijana.
Akiwa Manyoni, Mkoa wa Singida, kuliibuka kero ya kukatika mara kwa mara kwa umeme na kuomba wafungiwe kituo kidogo cha kupoza umeme na Dk Nchimbi alimtaka Dk Biteko kushughulikia suala hilo haraka, akisisitiza atambana hadi tatizo hilo limalizike.
Maelekezo hayo yalitokana na kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata kwamba pamoja na mambo mengine mengi yaliyofanyika mkoani humo, suala la umeme wa uhakika linahitajika.
Suala la ujenzi wa makazi ya askari polisi liliibuka Makuyuni, Monduli mkoani Arusha na kusema atalifikisha kwa wahusika.
Masauni ndiye mwenye dhamana na Jeshi la Polisi. Pia, ulinzi wa wananchi wanaotoa taarifa za ubadhirifu walindwe lilijitokeza Himo, Moshi mkoani Kilimanjaro.
Katika eneo hilo, kuna mwananchi ameibua tuhuma za ubadhirifu na anatishiwa usalama wake.
Dk Nchimbi alitaka raia huyo mwema na mwenye mapenzi na Taifa lake, kutosumbuliwa kwa namna yoyote.
Waziri Kairuki yeye anapaswa kusimamia taasisi zake zinazosimamia hifadhi zisitumie nguvu dhidi ya wananchi.
Mauaji na kujeruhiwa wananchi ni matukio ambayo yamekuwa yakitokea mara kadhaa na kuibua mjadala.
Hili lilitokana na kilio kilichowasilishwa kwake na Mbunge wa Vunjo (CCM), Dk Charles Kimei aliyesema kuna changamoto kadhaa, zikiwemo mauaji yanayofanywa na Askari wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa).
“Tunaunga mkono sheria zinazohifadhi misitu yetu kwa kuilinda kwa siku zijazo, lakini wakumbuke ubinadamu ni kitu cha kwanza, lazima wajali maisha ya wananchi wetu, kutumia silaha ni jambo la hovyo kidogo na Serikali naielekeza kutumia busara tunaposhughulikia kesi zinazohusu wananchi,” anasema Dk Nchimbi.
Amesema ndiyo maana hata sheria zinasema kutumia nguvu inapohitajika na sio kila mara unatumia nguvu.
Mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ni Profesa Mkenda ambaye ametakiwa hadi kufikia mwisho wa Juni 2024 wanafunzi wote wawe wamepata.
Ni baada ya wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Arumeru, Arusha kuwasilisha kero hiyo.
Katika majibu yake, Profesa Mkenda amesema hili atalifanyia kazi ndani ya muda uliotolewa.
Pia, Profesa Mkenda anapaswa kuhakikisha anaondoa ubovu wa miundombinu ya Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), Kilimanjaro kuhakikisha anasimamia ukarabati.
Ni kero iliyoibuliwa katika mkutano wa hadhara uliofanyikia Stendi Kuu ya Mabasi, Moshi.
Waziri Bashe, yeye ana jukumu la ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji Itaja, mkoani Singida na soko la vitinguu eneo hilo ambapo ametakiwa kusimamia hilo linafanyika.
Maagizo hayo yalitolewa Mei 30, 2024 wakati msafara wa Dk Nchimbi uliposimama eneo hilo akiwa njiani kwenda Manyara.
Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Ramadhan Ighondo alisema licha ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, wananchi hao kwa sehemu kubwa ni wakulima na wanaomba ujenzi wa soko la mazao.
Baada ya kuibiliwa kwa kero hiyo, Dk Nchimbi alimpigia simu Waziri Bashe ambaye alipopokea, pamoja na mambo mengine alisema Serikali inakwenda kuongeza kodi kwenye mafuta ya kula yanayotoka nje ya nchi katika Bajeti ya mwaka 2024/25 itakayosomwa Alhamisi, Juni 13, 2024 ili kuwalinda wakulima wa zao la alizeti.
Suala la ujenzi wa soko, Bashe alisema liandaliwe eneo na liwe na hati na mchakato wa ujenzi utaanza. Katika hilo, Dk Nchimbi amemwambia Bashe anataka soko hilo ujenzi wake ukamilike kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa 2025 na Waziri huyo alijibu: “Nimepokea.”
Akigusia kilimo cha umwagiliaji, Waziri Bashe amesema kuna zaidi ya Sh10 bilioni zimetengwa kwenye bajeti ijayo ili kujenga Bwawa la Msangi ambalo litakuwa mkombozi kwa wananchi na kuendeleza kilimo bila kutegemea mvua.
“Tayari mkandarasi amepatikana na yupo eneo la mradi. Nikuhakikishie katibu mkuu na wananchi wa Singida kwa ndugu yangu Ighondo, mradi utakamilika kwa wakati,” amesema Bashe.
Makalla akizungumzia mafanikio ya ziara hiyo, anasema kila walipopita wameshuhudia utekelezaji mkubwa wa ilani hiyo, jambo linalowapa matumaini uchaguzi wa serikali za mitaa watautumia kama kipimo cha ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
“Kila tulipopita wananchi wameongeza imani na CCM, tunawaomba utakapofika uchaguzi wa serikali za mitaa muwachague wagombea wetu na tuwatumie salamu ndugu zetu kwenye uchaguzi mkuu ujao,” amesema Makalla.