Aliyehukumiwa kifungo miaka 30 jela kwa unyang’anyi aachiwa huru

Arusha. Mahakama ya Rufani Tanzania  imemwachia huru, Grace Omary aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela alichohukumiwa kwa kosa la kumpora mwanamke mwenzake fedha taslimu Sh300,000 kwa kutumia silaha baada ya kushinda rufaa yake.

Grace ambaye alijiwakilisha mwenyewe kortini, alihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Wilaya ya Tarime, akakata rufaa Mahakama Kuu lakini akakwaa kisiki ndipo akaamua kukata rufaa mahakama ya Rufani Tanzania.

Katika rufaa yake hiyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Ktira Temba, akimwakilisha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), aliunga mkono rufaa hiyo akianisha sababu ya kufanya hivyo ni dosari katika utambuzi wa mrufani eneo la tukio.

Kulingana na maelezo ya kosa, ilidaiwa mahakamani kuwa usiku wa Julai 20, 2017 katika Mtaa wa Kyebikiri, Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara, mrufani akiwa na watu wengine wawili, walimvamia Rehema Masero na kumpora fedha hizo.

Shahidi wa kwanza (Rehema), alidai akiwa amelala, aliamshwa kutoka usingizini na mwanamke aliyekuwa akipiga kelele kuomba msaada na kugonga mlango.

Alidai aliwasha taa ya jua, akafungua dirisha na kumuona mwanamke huyo akiwa amelala chini mbele ya mlango wa nyumba na alipofungua mlango mwanamke huyo alimshika shingoni, akaanguka chini.

Alidai kuwa watu wawili walitokea na kumkata kwa panga usoni na mkono wa kushoto, wakimlazimisha awape pesa na kuwa aliwaelekeza alipokuwa ameficha Sh300,000 chini ya godoro ambazo walizichukua na kukimbia.

Baada ya watu hao kukimbia Rehema alidai kupiga kelele ambapo majirani zake akiwemo shahidi wa tatu katika kesi hiyo walimpeleka mrufani (Grace) eneo la tukio.

Aliendelea kudai alipomuona mrufani, alimtambua kuwa ni mmoja wa majambazi watatu waliokuwa wamemnyang’anya na kudai mrufani alipohojiwa alikiri kuwa miongoni mwa majambazi na kuwataja wengine ni Juma na Mwita.

Shahidi wa tatu Steven Benatus, alidai mahakamani kuwa aliposikia kelele kutoka kwa Rehema alikimbilia huko na akiwa njiani alikutana na mrufani akiwa anatoka kwa mlalamikaji huyo na alipomuuliza nini kimetokea, mrufani alimjibu kuna mke anapigana na mumewe.

Shahidi huyo alidai kutokuamini alichoambiwa na mrufani huyo na kuamua kumkamata na kumrudisha nyumbani kwa Rehema ambaye alimtambua kama mmoja wa majambazi.

Shahidi wa pili wa mashtaka katika kesi hiyo alikuwa Christina Managa, akitoa ushahidi wake alidai kumkuta jirani yake (Rehema) akiwa chini anavuja damu kutokana na majeraha ya kukatwa kichwa na mikono yote miwili.

Alidai kushuhudia mrufani aliyefikishwa katika eneo la tukio na kutambuliwa na shahidi wa kwanza (Rehema), kwama mmoja wa majambazi waliomuibia.

Shahidi wa nne ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Masiaga Chacha, alidai Julai 20,2017, Rehema alipatiwa matibabu baada ya kuwa na majeraha kichwani na mkono wa kushoto.

Katika ushahidi wake mfupi alioutoa chini ya kiapo, Grace alikana kutenda kosa hilo akiiambia Mahakama ya Wilaya kuwa alikamatwa Julai 29, 2017 saa tano usiku na wanaume wawili waliompeleka kituo cha polisi na kuwa baada ya wiki mbili alifikishwa katika mahakama hiyo na kufunguliwa shtaka la wizi wa kutumia silaha.

Kutokana na ushahidi wa upande wa mashtaka, mahakama ya wilaya iliona kesi dhidi ya mrufani ilikuwa imethibitishwa bila shaka yoyote na ilibainika mrufani alikamatwa na shahidi wa tatu wakati akikimbia kutoka eneo la uhalifu.

Aidha, iliangalia kuwa mrufani alitambuliwa na shahidi wa kwanza na alikiri kuwa miongoni mwa majambazi waliompora pesa zake na kumtia hatiani kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Baada ya kuhuhumiwa adhabu hiyo, mrufani alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma ila ilitupiliwa mbali, kisha akakata rufaa Mahakama ya Rufani.

Katika mahakama ya rufani, mrufani huyo alikuwa na hoja nne ambazo ni kutokutambuliwa vyema katika eneo la uhalifu, kesi haikuchunguzwa kama inavyotakiwa na sheria, hakuandika maelezo ya onyo na kesi haikuthibitishwa kwa kiwango kinachohitajika.

 Wakili wa Serikali, Ktira Temba,  alianza kwa kuieleza mahakama kuwa mjibu rufaa haipingi rufaa hiyo, na kudai hoja ya pili na tatu hazina msingi, huku hoja ya kwanza kuhusu utambuzi wa mrufani akiona inastahili na kwa msingi huo kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa kama ilivyolalamikiwa katika msingi wa 4 wa rufaa hiyo.

Alieleza ushahidi wa utambuzi wa mrufani katika kesi iliyopo, shahidi wa kwanza kudai mrufani alikuwa eneo la uhalifu na kuwa ukali wa mwanga wa taa  inayodaiwa kuwa ni sola haujawekwa wazi na haijafahamika iwapo taa hiyo ilikuwa nje ya nyumba au la.

 Pia, alisema kuwa shahidi wa kwanza hakumjua mrufani hapo awali na muda wa shahidi huyo alikuwa na mrufani chini ya uangalizi haukuelezwa, hivyo kupinga ushahidi wa kumtambua mrufani eneo la tukio haukuwa wa kuaminika.

Wakili Temba alieleza mahakama hata ushahidi wa kimazingira kutoka kwa shahidi wa tatu kwamba mrufani alikamatwa wakati akikimbia kutoka eneo la uhalifu ni wa mashaka na hauwezi kutegemewa kusitisha hukumu hiyo.

Alihitimisha kwa kueleza kuwa kwa kuzingatia ukweli kwamba mrufani hakutambuliwa vyema katika eneo la uhalifu, basi kesi dhidi yake hakuthibitishwa bila shaka yoyote na kuiomba mahakama kuruhusu rufaa hiyo kwa kufuta hukumu na kutengua adhabu iliyotolewa kwa mrufani.

 Kwa sababu hiyo, Wakili  Temba aliitaka mahakama kuruhusu rufaa hiyo kwa kufuta hukumu na kutengua adhabu iliyotolewa kwa mrufani.

Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, walioketi Musoma, Jaji Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Abraham Mwampashi na Zainab Muruke, walitoa maamuzi hayo baada ya kupitia hoja za pande zote mbili ikiwemo sababu nne za rufaa hiyo.

Katika hukumu yao iliyopatikana katika mtandao wa Mahakama Kuu wa TanzLII, baada ya kutolewa jana Juni 12, 2024 majaji hao wanaeleza kuwa baada ya kupitia hoja za pande zote mbili umebaini kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa bila shaka yoyote.

“Haijathibitishwa kuwa mrufani ni miongoni mwa majambazi watatu waliompora Rehema Sh laki tatu. Tunaruhusu rufaa, kufuta hukumu na kuweka kando adhabu iliyotolewa kwa mrufani. Mlalamikaji anapaswa kuachiliwa mara moja isipokuwa kama ameshikiliwa kwa sababu nyingine yoyote halali,” imeeleza hukumu hiyo.

Majaji hao baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kufuatilia mwenendo wa shauri la awali, uamuzi wao katika rufaa hiyo umeangalia kama mrufani alitambuliwa eneo la uhalifu na shahidi wa kwanza kama ilivyoelezwa katika mahakama hizo mbili za chini au lah.

Majaji hao wameeleza kuwa sababu zingine hazikuwa na msingi  na kuwa baada ya kuchunguza ushahidi ulio kwenye rekodi, wamefikia uamuzi kwa  kuzingatia ushahidi uliotajwa na mazingira ya kesi hiyo kulikuwa na na kutokuelewana.

Wameeleza kulikuwa na kutokuelewa  kwa ushahidi pamoja na sheria ya ushahidi wa utambuzi na mahakama mbili za chini.

“Kama alivyosema Temba, ni msimamo thabiti wa sheria kwamba ushahidi wa utambuzi wa macho ni wa aina dhaifu na usioaminika. Ili mahakama ichukue hatua kwa ushahidi wa utambuzi wa kuona, ni lazima ijiridhishe utambuzi ulikuwa sahihi ,”wameeleza

Kuhusu ushahidi wa shahidi wa tatu wakati akikimbilia kwa shahidi wa kwanza alikutana na mrufani ambaye alikuwa akitokea upande wa nyumba ya shahidi wa tatu, ikabidi amshike baada ya kutoamini kisa chake cha kuwa kuna mke na mume wanapigana, huacha mashaka.

“Ni maoni yetu kwamba kutoka upande wa nyumba ya shahidi wa kwanza  na kutoroka au kukimbia kutoka kwa nyumba ya mwathirika ni maneno mawili tofauti yenye maana tofauti, kwa kuwa shahidi wa tatu hakushuhudia kwamba alipokutana na mrufani, alikuwa akitoroka au kukimbia,” wamesema.

Walieleza kuhusu madai ya mrufani kukiri kuwa miongoni mwa majambazi walioiba kwa shahidi wa kwanza, baada ya kugundua kuwa ushahidi wa utambuzi wa mrufani haukuthibitishwa, madai hayo yanakuwa hayana msingi.

“Pia tunakubaliana na Temba kwamba, kwa mazingira ya kesi hii, inatia shaka sana kwamba, mrufani alikiri kama inavyodaiwa na shahidi wa kwanza kwa sababu si shahidi wa pili au wa tatu aliyeshuhudia kwamba mrufani alihojiwa na akakiri hivyo,” wamesema.

Related Posts