Wakati mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 yanasomwa leo, moja ya matarajio ni ya wadau ni kuunda sheria ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu nchini.
Pia, inatarajiwa Serikali itakuja na mkakati wa kupunguza utitiri wa kodi kama zilivyolalamikiwa na wabunge.
Wabunge kadhaa, ikiwamo Kamati ya Bunge ya Bajeti wanatarajia ushauri wao wa kuanzishwa sheria ya kupungua matumizi ya fedha taslimu utakuwemo kwenye hotuba ya bajeti.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Twaha Mpembenwe, kwenye hotuba yake alisema Kamati ilibaini kuwa moja ya changamoto katika ukusanyaji wa kodi ni matumizi ya fedha taslimu.
“Serikali imekuwa ikishindwa kufuatilia miamala ya biashara kwa sababu ya malipo kufanyika kwa fedha taslimu.
“Kamati inaishauri Serikali kufanya mabadiliko katika Sheria ya Mifumo ya Malipo Sura ya 437 na Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura 438 na kuanzisha sharti la kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki wakati wa kufanya manunuzi ya huduma na bidhaa,” alisema.
Kamati iliishauri Serikali iendelee kutoa elimu kwa wananchi na kuhimiza watoa huduma za kifedha kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kufungua akaunti na kuweka fedha zao kwenye mabenki na kuwahamasisha kuacha kutumia fedha taslimu.
Pia, alisema kamati ilibaini kuwa takwimu za mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi, zimekuwa zikitofautiana kati ya zile zinazotolewa na mabenki, zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na zinazotolewa na wizara husika.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Mbinga Mjini, Jonas Mbunda, alimshauri Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kuwasilisha sheria itakayowezesha kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika huduma na manunuzi.
Alisema kuendelea kutumia mfumo wa fedha taslimu kunaifanya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa na mapato madogo ya kikodi ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Alisema ukilinganisha pato la Taifa la mapato ya kodi, Tanzania inakusanya asilimia 11.8 ambayo ni ya chini, ikilinganishwa na nchi za Uganda asilimia 13.1, Rwanda asilimia 16.6, Kenya asilimia 18.1 na Burundi asilimia 13.6, kwamba Tanzania iko chini.
“Wazo langu, ili tuweze kukusanya mapato ya kutosha inatakiwa tuimarishe mifumo ya Tehama ya ukusanyaji wa kodi, inatakiwa iimarishwe na kuhakikisha inasomana ili kama kuna tatizo la kupata mapato ya kutosha liweze kushughulikiwa mapema,” alisema.
Pia, alisema sekta isiyo rasmi inafikia asilimia 60 na kwamba Serikali ikipeleka nguvu huko, kuna uhakika wa kupata mapato ya kutosha kupitia mfumo wa malipo yasiyo ya taslimu.
Alimuomba Waziri wa Fedha kuja na mpango wa matumizi ya ‘cashless economy’ na kwamba kwa upande wa vijijini anaweza kuweka utaratibu wa kupunguza kiwango cha matumizi ya fedha taslimu.
Hilo pia lilizungumziwa na Mbunge wa Makete, Festo Sanga alisema kuwa kamati imeshauri iletewe sheria kuhimiza matumizi ya siyo ya taslim ili kupata bidhaa na kupata huduma.
“Watanzania wengi wana intaneti, kwa mujibu wa ripoti ya Nape (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye) nusu ya Watanzania wana uwezo wa kutumia mtandao wa intaneti.
“Lakini kwa kutumia ‘cashless economy’, tunaweza kufanikiwa mambo mengi sana, moja ni kudhibiti masuala ya rushwa, kubwa zaidi ni ukusanyaji wa kodi.
“Hili jambo litafanikiwa kwanza kwa kufanya mabadiliko ya sheria,” alisema.
Sanga alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatakiwa itoe nafuu kwa watu wanaotumia ‘cashless economy’ kwa kuwapunguzia kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Alisema TRA inaweza ikatoa nafuu ya asilimia 15 au 16 kwa wanaotumia ‘cashless economy’ na wanaolipa taslimu wakatozwa VAT ya asilimia 18 au zaidi.
Pia aliitaka Serikali kuzungumza na mabenki wapunguze gharama za kutoa fedha kwenye akaunti benki kwenda kwenye simu.
“Lazima tuwaondoe watu kukaa na fedha taslimu, kwa mtu kuwa na ‘mabulungutu’ ya fedha mkononi au nyumbani kwake, wakati katika hali ya kawaida anaweka maisha yake hatarini na kuhatarisha uchumi wa nchi,” alisema.
Sanga pia aliitaka Serikali kuwahakikishia watumiaji wa mtandao usalama wa fedha zao na uhakika wa mtandao kwa wakati wote badala ya mtandao kuwa chini au kukosekana kwa siku kadhaa.
Alitoa mfano wa Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani, kwamba baada ya kufunga mfumo wa malipo mtandaoni yameongeza mapato kutoka wastani wa Sh3 milioni hadi Sh6 milioni kwa mwezi hadi kati ya Sh30 milioni hadi Sh40 milioni kwa mwezi.
Mbunge wa Kalambo, Josephat Kandege aliishauri Serikali kuiondoa Tanzania kwenye matumizi ya noti na sarafu na kwenda kwenye ‘cashless economy’, kwamba ni rahisi kutuma pesa na kufanya malipo.
“Taarifa za malipo ya Serikali zitakuja kwenye simu na malipo utafanya kwenye simu, pia itazuia ukwepaji kodi na kila mtu atalipa kodi. Inawezekana vijijini ikaonekana itakuwaje, naamini Waziri wa Fedha kwenye Bajeti ya Serikali atasema kuna kiwango kitaruhusiwa kutumia fedha taslimu, lakini viwango vingine iwe ni cashless,” alisema.
Mbunge wa kuteuliwa, Shamvi Vuai Nahodha alisema ameongea na wafanyabiashara na wawekezaji ambao wamemweleza tatizo la Tanzania ni utitiri wa kodi na taasisi nyingine kutoza kodi zinazofanana.
Alisema mamlaka mbalimbali za Serikali zinashindana kutoza kodi na wakati mwingine mamlaka mbili zinatoza kodi ya aina moja.
“Mfano, pale bandarini Camartech anaangalia ubora wa vifaa vya kilimo, TBS (Shirika la Viwango Tanzania) anaifanya kazi hiyohiyo, matokeo yake gharama ya uzalishaji, gharama ya utoaji huduma Tanzania zinapanda sana.
“Sekta ya utalii ni sekta mojawapo ya ambazo zinaathiriwa na utitiri wa kodi. Machi tulifanya ziara nchini Kenya, tulikaa kwenye hoteli moja ya hadhi ya kitalii ya juu sana, kwa usiku mmoja tulilipa Dola za Marekani 55, hoteli hiyohiyo Tanzania unalipa zaidi ya dola 120,” alisema.
Alisema Serikali ilileta utaratibu wa kutoza wafanyabiashara wadogo (wamachinga) Sh20,000 kwa mwaka mzima.
“Jambo hili liliwapunguza wamachinga matatizo makubwa ya kulipa gharama mbalimbali. Kwa bahati mbaya jambo hili sijui limemalizikia wapi,” alihoji.
Pia, alihoji kuhusu hoja iliyowahi kuwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk Nchemba ya kubana matumizi ya magari na mafuta.
“Sisi tulilifurahia sana jambo hilo, lakini mpaka sasa waziri amekaa kimya, hajasema lolote kuhusu jambo hilo, pia, waziri alituahidi hapa shughuli zote za Serikali zitafanywa kwa mtandao, baada ya hapo waziri haelezi jambo lolote. Tumesikia wabunge walisema hapa baadhi ya mifumo serikalini haizungumzi,” alisema.
Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei aliiomba Serikali ikamilishe suala la sera ya kodi ili iweze kuingiza masuala yanayohusu kalenda ya kodi, inayohusu zaidi upande wa forodha pamoja na ushuru wa kawaida na tozo.
Juni 14, 2022, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23, Dk Nchemba alieleza mikakati ya kubana matumizi ya Serikali, ikiwemo ununuzi na matumizi ya magari, hatua ambazo zingeokoa zaidi ya Sh500 bilioni.
Alisema kwa wakati huo Serikali ilikuwa na magari, 15,742, pikipiki 14,047 na mitambo 373 na inatumia Sh558.45 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari, mafuta ya uendeshaji, vipuri na matengenezo ambapo kwa wakati huo ilikuwa ni zaidi ya Sh500 bilioni.
“Tutaondoa utaratibu uliozoeleka wa dereva kupitisha gari chini na bosi anapanda ndege mpaka Mwanza au Mbeya kutoka Dar es Salaam na kurudi hivyohivyo.
Alisema kuna utafiti wa siri ulifanywa kwa siku moja yalibainika magari ya Serikali yaliyotoka Dodoma kwenda Dar es Salaam yalikuwa 132 na yaliyokuwa yakitoka Dar es Salaam yakipishana kuja Dodoma yalikuwa 76 na mengine nane yalikuwa yamepinduka.
Alisema kwa utaratibu huo mpya, gharama za matumizi ya magari Serikalini zitakuwa zimeokolewa Sh500 bilioni.