Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amependekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220 ili kutoza Sh 382 kwa kila kilo ya gesi asilia inayotumika kwenye magari. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Amesema lengo la hatua hiyo ni kuongeza mapato yatakayotumika katika kufanya matengenezo ya barabara pamoja na kuleta usawa kwa kuwa magari yanayotumia mafuta tayari yanachangia mapato kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Amesema mapato yatakayotokana na chanzo hiki yatapelekwa Mfuko wa Barabara. Hatua hiyo inatarajia kuongeza Mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh 9.5 bilioni.
Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/2025, pia amependekeza amesema kuweka utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya barabara katika kipindi ambacho kutakuwa na punguzo la bei ya mafuta ya petroli sokoni ambapo badala ya bei hizo kushuka fedha hizo zitaelekewa kwenye Mfuko wa Barabara.
“Utaratibu huu utatekelezwa na Kamati Maalum itakayoundwa na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati kwa kushirikiana na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha kwa lengo la kupendekeza kiasi kitakachotengwa kwa kuzingatia wastani wa bei iliyopo sokoni.
“Aidha, mapato yatakayotokana na utaratibu huu yatapelekwa Mfuko wa Barabara. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali yatakayotumika katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara nchini,” amesema.