INEC yaeleza mchango wa Vyombo vya Habari na Mchakato wa Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacob Mwambegele, ameeleza kuwa Tume inatambua na kuheshimu mchango wa vyombo vya habari, hasa vya kijamii na kijitali, katika kuwafikia vijana ambao ni walengwa muhimu wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Juni 13, 2024, katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Jaji Mwambegele alibainisha kuwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura utaanza rasmi Julai 1, 2024, mkoani Kigoma, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, atakuwa mgeni rasmi.

Katika hotuba yake, Jaji Mwambegele alisema, “Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba vyombo vya habari vikuu bado vinawafikia watu wengi na vina umuhimu mkubwa katika kuwahabarisha na kuelimisha wananchi,” amesema.

Aliongeza kuwa uwepo wa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kwenye mkutano huo utasaidia kueneza taarifa muhimu kwa wadau wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla, hasa katika kipindi hiki cha uboreshaji wa daftari.

“Tunawasihi muendelee kutuunganisha na wadau. Tume itaendelea kuweka milango wazi kwa ajili ya kutoa taarifa za mara kwa mara,” alisema Jaji Mwambegele. Alifafanua kuwa Tume itakuwa na kituo cha huduma kwa wateja ambacho kitatoa majibu kwa maswali mbalimbali yanayohusiana na uboreshaji wa daftari.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhan Kailima akizungumza wakati wa Semina kwa waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga, Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhani, akiwakilisha mada kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, alisema kuwa zoezi hilo litahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi ifikapo tarehe ya uchaguzi Mkuu mwaka 2025. Pia litatoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye daftari na ambao wamehama kuhamisha taarifa zao, pamoja na kurekebisha taarifa nyingine kama majina.

Kuhusu idadi ya wapiga kura wanaotarajiwa, Kailima alisema, “Wapiga kura wapya wanaotarajiwa kuandikishwa ni 5,586,433, huku idadi ya wapiga kura baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/20 ikiwa ni 29,754,699,” alisema Kailima.

Aidha, alisema kuwa wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao, na wapiga kura 594,494 wanatarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo. Baada ya uboreshaji huu, inatarajiwa kuwa daftari litakuwa na jumla ya wapiga kura 34,746,638.

“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo Watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa wakati wa uboreshaji wa daftari mwaka 2019/20 lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” alieleza Kailima.

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa Tume imekamilisha maandalizi yote muhimu, ikiwemo vituo vya kuandikishia wapiga kura ambavyo vipo 40,126 nchi nzima, Tanzania Bara na Zanzibar.

Related Posts