Jukumu la kutunza mazingira wajibu wa kila mtu

Dar es Salaam. “Safari kuelekea mustakabali wenye urafiki na mazingira,” hii ni mada itakayojadiliwa kesho kwenye Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Mada hii imekuja kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali za mazingira, hasa mabadiliko ya tabianchi.

Lengo ni kuleta suluhu ya pamoja na endelevu kwa mustakabali wa nchi.

Tunafahamu, uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea maliasili kama misitu, bahari, maziwa, mito, ardhi oevu, wanyamapori, ardhi, gesi asilia na madini ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini.

Hata hivyo, matumizi yasiyo endelevu ya maliasili yamechangia uharibifu wa mazingira ambao umekuwa na athari kiuchumi, ikiwamo kupungua kwa pato la Taifa.

Akihutubia mkutano wa mabadiliko ya tabianchi (COP 28) uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania inapoteza asilimia mbili hadi tatu ya pato la Taifa kila mwaka.

Kutokana na uhalisia huu, Serikali ilikuja na Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2032) utakaozingatia masuala hayo yote na kutoa mwongozo kuhusu usimamizi wa mazingira.

Lengo kuu la Mpango Kabambe wa Taifa ni kutoa mwongozo wa hatua za kuchukuliwa kutatua changamoto za mazingira nchini kwa kuzingatia sehemu husika na hatua mahsusi zinazopaswa kuchukuliwa.

Mpango huu ulitaja changamoto 12 za mazingira zinazoikabili nchi yetu na kuweka mikakati ya kuzitatua.

Changamoto hizo ni uharibifu wa ardhi, uharibifu wa vyanzo vya maji, athari za mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, ukataji ovyo wa miti na uharibifu wa misitu, upotevu wa makazi ya wanyamapori na bioanuai, uharibifu wa mfumo-ikolojia ya pwani na baharini, uharibifu wa ardhi oevu, usimamizi hafifu wa taka, kuenea kwa viumbe vamizi na changamoto za mazingira katika miji.

Kwenye matumizi ya ardhi takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 60 ya wananchi ni wakulima.

Pia, kuna wafugaji, hasa katika mikoa ya kati na kusini mwa Tanzania. Makundi haya yote yanategemea ardhi; na katika matumizi ya nishati takwimu zinaonyesha karibu asilimia 90 ya Watanzania wanategemea kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati.

Pia, changamoto hizo zinahusishwa na  mfumo wa usimamizi wa mazingira.

Ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira, Serikali kwa kushirikiana na wadau, imechukua hatua kadhaa, ikiwamo kutunga sera na sheria pamoja na kutekeleza programu na miradi ya hifadhi ya mazingira.

Licha ya juhudi hizo, nchi inaendelea kukabiliwa na changamoto za mazingira. Malengo mahsusi ya mpango ni kuainisha hali ilivyo ya changamoto za mazingira, ikiwamo visababishi, athari zake na hatua zilizoendelea kuchukuliwa na vikwazo.

Pia, kutoa mwelekeo wa kimkakati wa mabadiliko yanayohitajika kuleta matokeo chanya, kuainisha maeneo ya vipaumbele na kuainisha hatua mahsusi zinazopaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na changamoto za mazingira husika. Mpango unataja majukumu ya wadau wote wa mazingira kuanzia taasisi za umma na binafsi pamoja na mwananchi mmoja mmoja.

Utunzaji mazingira unaanza na wewe

Mazingira ni jumla ya vitu vyote vyenye uhai na visivyo na uhai vinavyomzunguka mwanadamu. Kwa maana hiyo mwanadamu amepewa haki ya kuvitawala vitu vyote vinavyomzunguka.

Licha ya uhuru aliopewa mwanadamu wa kuvitawala vitu vyote, utashi wake umeonekana ukijenga au kubomoa sehemu nyingine, hivyo kuathiri mfumo wake wa maisha kwa jumla.

Mwanadamu amekuwa akiishi katika matabaka ya aina mbalimbali, yupo mwenye hali nzuri ya maisha, ngumu ya maisha, msomi na asiyesoma, huku matabaka yakigawanyika kulingana na jiografia ya mahali husika.

Mwanadamu huyu katika harakati zake za kujitafutia unafuu wa maisha amekuwa akiharibu mazingira kwa kujua na wakati mwingine kutokujua, madhara anayoyatengeneza kutokana na shughuli zake humuathiri yeye na jamii inayomzunguka.

Mwanadamu amekuwa akikata miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama nishati ya kupikia na biashara ya mkaa, kujenga nyumba, kuanikia mazao kama tumbaku bila kujua kuwa shughuli zake hizo zinasababisha ukame, mmomonyoko wa ardhi kutokana na ardhi kutokuwa imara, mafuriko yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Mwanadamu amekuwa akifanya kilimo pembezoni na maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji, kemikali anazotumia kama mbolea na viuatilifu vikali vinaleta madhara kwa sababu vinatiririshwa kwenye maji ambayo hutumiwa na mwanadamu.

Kemikali hizo zinaweza kuleta shida kiafya na kuharibu ikolojia ya eneo husika.

Mwanadamu amekuwa akifanya uvuvi haramu kwenye vyanzo vya maji kama mito, maziwa na bahari, lengo likiwa kujipatia kipato na vitoweo bila kujali athari zinazojitokeza, zinazomlenga hata yeye, ikiwamo kupotea kwa mazalia ya samaki na uchumi kuyumba.

Mwanadamu huyu amekuwa akichimba madini kwa kutumia mashine kubwa zinazosababisha mtikisiko wa ardhi, hivyo kukosekana kwa uimara wa ardhi.

Pia, hutumia kemikali kali kwenye mabwawa, ikiwamo ya zebaki ambayo kwa namna moja isipotumika kwa uangalifu huleta madhara kwa watumiaji na uharibifu wa mazingira.

Mwanadamu amekuwa akifanya uzalishaji wa bidhaa kwa viwanda vidogo na vikubwa, ndani ya hivyo viwanda kumekuwapo na mitambo ya umeme inayozalisha moshi unaotambaa angani.

Pia, ununuzi wa magari ambayo yameshatumika na hayana hadhi ya kutembea barabarani yanayotoa moshi kwa kiasi kikubwa unaozalisha hali joto na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.

Kuna maeneo ambayo kutokana na jiografia yake kama mikondo ya maji hayatakiwi kuwekwa makazi ya watu, lakini ukosefu wa elimu na hali ya watu kutaka kuishi maeneo ya mjini hulazimisha kujenga katika sehemu hizo.

Inapotokea mvua imenyesha kwa kiwango kikubwa maji hushindwa kupita, hivyo kusababisha mafuriko yanayoleta hasara ya samani za ndani na wakati mwingine vifo.

Related Posts