Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema hakuna kifungu chochote cha sheria kinachotaka watumishi wake kujiuzulu kwenye nafasi zao kupisha mchakato wa kupatikana wajumbe wapya.
Amesema kuna uhalali wa kisheria unaowafanya watumishi hao waendelee kuwapo kwenye nafasi hizo.
Kauli ya INEC, inajibu msimamo wa Chama cha ACT-Wazalendo unaotaka watumishi wa tume hiyo akiwemo mwenyekiti, makamu wake na wajumbe kujiuzulu kupisha mchakato wa kupatikana kwa wajumbe wapya.
Msingi wa msimamo wa chama hicho ni mabadiliko ya sheria ya INEC inayosema nafasi hizo za ujumbe wa tume, zinapaswa kuombwa na kushindaniwa.
Kwa sababu hiyo, chama hicho kilisusia kushiriki uchaguzi mdogo wa Kwahani, kushinikiza kujiuzulu kwa wajumbe hao.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima amesema hayo leo Juni 13, 2024 kwenye mkutano wa tume na wanahabari kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura.
Amesema uhalali wa nafasi za wajumbe unatokana na kifungu cha 27 cha Sheria ya INEC ya mwaka 2024.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, “mara baada ya kuanza kutumika kwa sheria hii, mtu yeyote ambaye ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au Mjumbe wa Tume ataendelea kushika madaraka hayo hadi pale ujumbe wake utakapokoma.”
Amesisitiza yeyote anayetaka wajumbe hao wajiuzulu, anatakiwa kuja na sheria inayohalalisha viongozi hao kujiuzulu kwa sasa.
“Mnapaswa muwaulize hao wanaolalamika kwamba, kuna sheria gani inayotaka watumishi hao wajiuzulu,” amesema.
Kuhusu tume kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kailima amesema hawana wajibu wa kisheria wa kutekeleza jukumu hilo.
Ameeleza wapo aliowaita wapotoshaji, wanaodai Katiba ya nchi inaitaka INEC isimamie uchaguzi huo, akifafanua ni tofauti na uhalisia.
Kailima amesema kilichotamkwa katika Katiba ni tume kusimamia uchaguzi wa Serikali ya mitaa kwa mujibu wa sheria itakayotungwa na Bunge, ambayo kwa sasa bado haijatungwa.
Kutokuwepo kwa sheria hiyo, amesema kunaikosesha INEC wajibu wa kusimamia uchaguzi huo, badala yake unaendelea kusimamiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele ameeleza umuhimu wa vyombo vya habari kuhamasisha wananchi kushiriki katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura.
“Vyombo vya habari vina mchango muhimu katika kuhamasisha jamii kwa sababu vina nguvu inayoviwezesha kufika pasipofikika katika mazingira ya kawaida,” amesema.