Dar/Dodoma. Baada ya kilio kuhusu kikokotoo cha mafao ya wastaafu kusikika baadhi wa wabunge, wamepongeza hatua hiyo wakisema ni nzuri japokuwa walitarajia zaidi.
Kauli hizo za wabunge zinafuatia hatua ya Serikali kuongeza fao la mkupuo watakalolipwa wastaafu kwa asilimia mbili kwa baadhi yao na wengine asilimia saba.
Ongezeko la fao hilo la mkupuo linajibu vilio vya wastaafu, ambao awali walilalamikia asilimia 33 waliokuwa wanalipwa, kuwa zisingewasaidia kuzikabili gharama za maisha wakati wa ustaafu.
Kilio cha wastaafu kilibebwa pia na wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa, waliodai hatua ya Serikali kuwalipa wastaafu kiasi hicho ni kukosa shukurani kwa waliolitumikia Taifa kwa miaka lukuki.
Sambamba na wadau hao, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), lililalamikia hilo na kupendekeza mabadiliko ya kanuni zinazokokotoa mafao ya wastaafu.
“Kwa kuwa mifuko inaonyesha kuimarika Serikali ione haja ya kuboresha kanuni hizo bila kuathiri mifuko hiyo,” alisema Katibu Mkuu wa Tucta, Henry Mkunda alipohutubia katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei 1, mwaka huu.
Mabadiliko ya ukokotoaji wa mafao hayo ya wastaafu, yametangazwa bungeni jijini Dodoma leo Juni 13, 2024 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipowasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/25.
Katika mabadiliko hayo, Dk Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuongezwa malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 iliyopo sasa hadi asilimia 40 kwa wale waliokuwa wanalipwa asilimia 50.
Mara baada ya kuahirishwa kwa Bunge hadi Jumanne, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya ambaye amekuwa miongoni mwa wabunge vinara kupigia kelele kitototoo, amesema anaamini mifuko ya hifadhi ya jamii ingekuwa na uwezo wa kulipa hadi asilimia 60 katika mafao ya mkupuo.
“Imekuwa hivi kwa sababu mifuko hii ni hoehae lakini waliosababisha hivi ni wao wenyewe na anayepata taabu ni mtumishi wa umma. Sasa rai yangu wamesema wamefikisha asilimia 40 na wamesema kuwa wataongezea kwa kipindi cha muda mfupi hadi watakapoona kuwa iko sawa.
“Kikubwa ninachoweza kusema nipongeze kwa hiyo hatua lakini kiukweli bado kwa sababu kabla ya sheria kubadilishwa ilikuwa ni asilimia 50,” amesema Bulaya.
Ametaka kilio cha wafanyakazi kiendelee kufanyiwa kazi ili wanapomaliza utumishi wao basi wapate kitu wanachostahili.
“Nchi nyingine zinaondoka na asilimia 60 hadi asilimia 70, kwa hiyo sisi mifuko yetu kuwa hoehae na iliyosababisha ni Serikali yenyewe. Kisiwe kigezo cha kuwaminya wale wanaokatwa kila mwezi ili mwisho wa siku wapate mafao yao yatakayoweza kuwaandalia maisha mazuri ya kustaafu,” amesema.
Mtazamo wa Bulaya unafafana na wa Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda aliyesema suala la kikokotoo alitamani wastaafu wagepewa kiasi chote cha asilimia 50 kama ilivyokuwa awali.
Hata hivvyo, amesema kiasi cha asilimia 40 ambacho Serikali imekitoa ni hatua kubwa, na kwa upande wake ameona Serikali imefanya vizuri kwao.
Mbunge wa Nkenge (CCM) Florent Kyombo amesema Rais Samia Suluh Hassan amepunguza makali yaliyokuwa kwa wastaafu kwa kubadilisha kikokotoo.
Amemshukuru Rais kwa kusikiliza kilio cha wafanyakazi na kwamba anaamini hata mapokeo kwa wastaafu walioko mitaani watakuwa wamepokea kwa moyo wa shukrani kwa kuwa Rais amesekia kilio chao.