Maumivu yaja magari yanayotumia gesi

Dar es Salaam. Serikali imeongeza Sh382 katika kilo moja ya gesi inayotumika katika magari na sasa bei itakuwa Sh1,932 kutoka Sh1,550.

Hayo ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa leo Juni 13, 2024 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipowasilisha hotuba ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma ya Sh49.3 trilioni.

Akizungumzia Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220, Dk Mwigulu amesema lengo la hatua hiyo ni kuongeza mapato yatakayotumika katika kufanya matengenezo ya barabara na kuleta usawa kwa kuwa magari yanayotumia mafuta tayari yanachangia mapato kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.

“Mapato yatakayotokana na chanzo hiki yatapelekwa Mfuko wa Barabara. Hatua hii inatarajia kuongeza Mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh9.5 bilioni,” amesema. 

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi kuhusu hatua hiyo, wamesema itadumaza jitihada za kuhakikisha watu wengi wanatumia gesi asilia, huku wakihoji kigezo alichotumia waziri kuongeza kiwango hicho. 

“Kilo moja ya gesi kwa sasa ni Sh1,550, kwa ongezeko hilo bei itapanda. Magari yaliyopo sasa nchini yaliyofungwa gesi si zaidi ya 5,000, idadi ni ndogo kiasi cha kuanza kuweka tozo kwenye eneo hilo,” amesema Alex Wiliam, dereva teksi mtandao. 

Amesema kilichokuwa kinapaswa kufanyika ni kuhakikisha wanashawishi wawekezaji wanajenga vituo na idadi, ikishaongezeka basi Serikali ingekuja na kusudio la kuongeza hizo tozo. 

“Sijajua amekujaje na mtazamo huo, kwa hali ya kawaida nilikuwa nategemea bei ingepunguzwa zaidi ili kuchochea watumiaji waongezeke lakini kwa sura hiyo, hamasa inaenda kushuka,” amesema. 

Msemaji wa Kampuni ya kuunganisha mifumo ya gesi kwenye magari kutoka Kampuni ya NK CNG Auto Ltd, Amani Jacob amesema mapendekezo hayo iwapo yatapitishwa yatawarudisha nyuma waliokuwa wanahitaji huduma hiyo na wanaofanya biashara ya kufunga mitungi.

“Wateja watapungua na biashara itadorora, hamasa ilishaanza kuwa kubwa. Sasa mapendekezo haya ni kuwakosea Watanzania na jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema. 

Aman alishauri umuhimu wa kutokuingiza siasa kwenye mambo ya msingi kwani athari zake ni kubwa na kuwa kama wadau, walikuwa wanatarajia kasi ya kujenga vituo iongezeke. 

“Serikali ina mkono mrefu, tulitamani ihamasishe kwanza kujenga vituo na kuna dhana imesambaa mitaani vituo haviongezeki kutokana na siasa kwamba watu wakubwa wana vituo vyao vya mafuta, wakiongeza vituo vya gesi wanaharibu biashara zao,” amesema. 

Naye Salmon Samson ambaye ni dereva bajaji amesema kuna umuhimu wa viongozi kuwashirikisha wadau badala ya kuongeza tozo zinazoenda kuwaumiza wananchi. 

Maumivu mengine yanakuja kwa wanaofikiria kununua magari ya umeme, eneo ambalo Waziri Mwigulu amependekeza kulijumuisha kwenye wigo wa ulipaji wa ada ya usajili wa magari. 

“Lengo la hatua hii ni kuzingatia kanuni za usawa za utozaji wa kodi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia,” amesema. 

Pia, Dk Mwigulu amependekeza kufanyika marekebisho kwenye Sheria ya Reli ya mwaka 2017 kwa kuongeza kiwango cha Tozo ya Maendeleo ya Reli (Railway Development Levy) kinachotozwa kwa bidhaa zote zinazoingia na kutumika nchini kutoka asilimia 1.5 ya thamani ya mzigo (CIF) hadi asilimia 2 ya thamani ya mzigo. 

Amesema asilimia 50 ya mapato yatakayotokana na chanzo hicho, yatapelekwa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Reli na asilimia 50 itapelekwa kwenye Mfuko wa Barabara.

“Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayotumika katika kuboresha na kujenga miundombinu ya reli na barabara zilizoathiriwa na mvua za El-Nino. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh216.898 bilioni,” amesema.

Mbali na maumivu hayo, wazalishaji na waunganishaji wa simu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kufuta ushuru wa forodha kwenye malighafi zinazotumika katika uzalishaji au uunganishaji wa simu za mkononi.

“Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji na waunganishaji wa simu ndani ya Jumuiya ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa gharama nafuu, kuongeza ajira pamoja na kuhamasisha uwekezaji,” alisema.

Akizungumza na watendaji wa wizara yake, Januari 2021, aliyekuwa Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Dk Faustine Ndungulile amesema Serikali ilikuwa inakamilisha mchakato wa kujenga kiwanda cha simu za kisasa jijini Mwanza.

Machi 19, 2024 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alitembelea kiwanda cha Tanztech jijini Arusha cha kuunganisha vifaa vya kielektroniki kama simu janja, vishikwambi, kompyuta, na vifaa vingine vya kielektroniki.

Katika hatua nyingine, Waziri Mwigulu amependekeza kufanyika marekebisho katika Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, Sura 289 ili kuelekeza asilimia 20 ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye kodi ya majengo na kodi ya pango la ardhi ipelekwe moja kwa moja kwenye akaunti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (halmashauri) husika. 

Kwa utaratibu huo, mapato hayo ya halmashauri yalikuwa yanaingia Mfuko Mkuu wa Serikali na kisha halmashauri kuomba kurejeshewa asilimia 20 ya mapato hayo.

“Lengo la hatua hii ni kuwezesha Mamlaka ya Serikali za Mitaa kugharamia masuala ya ufuatiliaji na ukusanyaji wa kodi ya majengo na kodi ya pango la ardhi kwa ufanisi na kwa wakati,” amesema.

Awali, kodi hiyo ilikuwa ikikusanywa na halmashauri, lakini mwaka 2015/16, Serikali kuu ilichukua jukumu la ukusanyaji wa kodi ya majengo na mabango kutoka serikali za mitaa kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na baadaye kurejesha mapato hayo katika halmashauri husika. 

Mwaka huohuo Serikali ilishusha makadirio ya makusanyo ya kodi hiyo kutoka Sh58 bilioni zilizokuwa zimekadiriwa na serikali za mitaa na kuwa Sh47.7 bilioni. 

Hata hivyo, Juni 5, 2018, Kamati ya Bunge ya Bajeti iliishauri Serikali kurudisha ukusanyaji wa kodi ya majengo na mabango kwa halmashauri badala ya kuendelea kuwa chini ya TRA. 

Hatua hiyo pia imependekezwa kwenye Sheria ya Korosho, Namba 18 ambapo Dk Mwigulu ametaka kufanyika kwa marekebisho kwenye Sheria ya Korosho ili mapato yatokanayo na tozo ya kusafirisha korosho ghafi nje ya nchi yapelekwe Bodi ya Korosho kwa asilimia 100 kwa kipindi cha miaka mitano. 

“Lengo la hatua hii ni kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na kusaidia upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya ruzuku na utafiti pamoja na kuongeza mchango wa zao hilo katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Suala la tozo ya mauzo ya korosho lilizua mjadala bungeni Juni 2018 baada ya Serikali kupendekeza kuzichukua zote kwa aislimia 100, tofauti na awali ilipokuwa ikichukua asilimia 35.

Miongoni mwa wabunge waliochangia suala hilo bungeni Juni 28, 2018, ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Kabwe Zitto akisema kitendo cha Serikali kutaka kuchukua asilimia  65 za ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi si sahihi kwa sababu fedha hizo ni za wakulima.

Zitto alisema uamuzi wa Serikali kutaka kuanzisha Akaunti Jumuifu ya Hazina (TSA) ni uvunjifu wa Katiba na sheria za ukaguzi. 

Mbali na kodi hiyo, Dk Mwigulu amependekeza marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kwa kuruhusu michango ya asilimia 15 inayolipwa na taasisi za Serikali kwenda Mfuko Mkuu wa Serikali, kuwa miongoni mwa sehemu ya gharama za taasisi kwenye ukokotoaji wa kodi ya mapato. 

Lengo la hatua hii ni kupunguza changamoto zilizopo katika ukokotoaji wa kodi hiyo kwa kuwa fedha hizo huingizwa Mfuko Mkuu wa Serikali. 

“Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa Shilingi milioni 1,000,” alisema. 

Katika hatua nyingine, Serikali imependekeza kufanyika kwa marekebisho kwenye Sheria ya Sukari, Namba 6 kama ili kuiwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuwa na uwezo wa kununua kuratibu na kuhifadhi pengo la sukari kwenye hifadhi ya chakula ya Taifa. 

Lengo la hatua hii ni kuwezesha upatikanaji wa sukari nchini na kuondoa uhodhi kwa baadhi ya wenye viwanda, bila kuathiri dhamira ya Serikali ya kulinda viwanda vya ndani. 

Hatua hii inafikia ikiwa ni siku chache tangu Tanzania kujinasua katika uhaba wa sukari uliokuwa unaishumbua nchi jambo ambalo lilikuwa likitajwa kuchangiwa na mvua kubwa iliyoathiri uzalishaji.

Hali hiyo ilifanya bei ya sukari kupaa hadi kufikia Sh6,000 katika baadhi ya maeneo huku baadhi ya wafanyabiashara wakilazimika kuacha kuiuza kwa muda.

Kufuatia uwepo wa hali hiyo, Serikali kupitia Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) ilitangaza bei elekezi ambapo kilo moja kwa wanunuzi wa rejareja ilitakiwa kuuzwa kati ya Sh2,700 hadi Sh3,200. 

Akizungumza hivi karibuni bungeni Dodoma, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema hatakubali kuona uhaba wa sukari ukijirudia, huku akikosoa baadhi ya viwanda vya sukari kushindwa kuagiza sukari na kusababisha uhaba huo. 

Akiwasilisha hotuba ya bajeti jana Bungeni jijini Dodoma, Dk Mwigulu alisema mapendekezo yake yanalenga kufanya marekebisho kwenye kanuni ya NFRA kwa kuijumuisha sukari kuwa sehemu ya usalama wa chakula. 

“Napendekeza kutoza Sh50 kwa kilo ya mabaki yanayotakana na uzalishaji wa sukari. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayoiwezesha Bodi ya Sukari kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuendeleza mafunzo na kukuza ujuzi katika sekta ya sukari,” amesema Dk Mwigulu na kuongeza. 

“Pia itaiwezesha bodi hiyo kusimamia uzalishaji wa sukari nchini kupitia upanuzi wa viwanda vilivyopo na kuhamasisha uwekezaji mpya,” alisema.

Related Posts