Mbunge akerwa majibu ya Serikali kujirudia yaleyale

Dodoma. Mbunge wa Kibiti, (CCM), Twaha Mpembenwe amekerwa na majibu ya Serikali yanayofanana kwa miaka minne mfululizo kuhusu ujenzi wa Barabara ya Kibiti, Dimani hadi Mloka.

Mpembenwe ameeleza hayo leo Alhamisi Juni 13, 2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma.

“Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 nimeuliza swali hili majibu ni haya haya, mwaka 2022 nimeuliza swali hili majibu ni haya haya, 2023 nimeuliza swali ni haya haya, mwaka 2024 nimeuliza swali hili na majibu yanajirudia hivi hivi,” amesema Mpembenwe.

Amehoji Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Kibiti, Dimani hadi Mloka hasa ukizingatia kuwa iko katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Je, mheshimiwa waziri uko tayari kuongozana na mimi twende kwa wapiga kura wangu, kule watu wa Kibiti, Dimani na Mloka uende ukawathibitishie kauli ya Serikali,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenye amesema yuko tayari na watapanga na mbunge huyo waende katika wilaya ama jimbo lake waone na aweze kuwaeleza wananchi mpango wa Serikali wa kujenga barabara hiyo.

“Hii barabara ni kweli iko katika Ilani na mwaka ujao tunategemea kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Na anafahamu hii barabara ndiyo inayotumika kwa sasa na wenzetu wa Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania), kwenda mradi wa Nyerere kupitisha vifaa vyote na ndio wanaoifanyia ukarabati,” amesema.

Amesema wakimaliza, azma ya Serikali ya kujenga kwa kiwango cha lami wataikamilisha na kuijenga ili wananchi waweze kufika kwa urahisi katika bwawa la Mwalimu Nyerere.

Katika swali la msingi, Mpembenwe amehoji ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Kibiti, Dimani hadi Mloka kwa kiwango cha lami.

Akijibu swali hilo, Kasekenya amesema barabara ya Kibiti – Dimani hadi Mloka yenye urefu wa kilometa 100.18 imeingizwa kwenye mpango wa mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

“Kazi hii ikikamilika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami,” amesema Kasekenya.

Related Posts