Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni anaingia kwenye mkutano wa kilele wa G7 akiwa ameimarishwa na matokeo mazuri katika uchaguzi wa Ulaya Jumapili iliyopita.
Italia ndiyo mwenyeji wa mkutano huo wa “Grande Sette”, kama kundi la G7 linavyojulikana kwa Kiitaliano. Meloni mwenyewe alisaidia kuunda maelezo mengi mwenyewe wakati wa kuandaa “mkutano wake,” kama anavyouita.
Mbali na Italia, G7 inajumuisha mataifa ya Marekani, Kanada, Japan, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya.
Rais wa Marekani aliwasili Italia jana jioni kushiriki mkutano huo utakaotawala na ajenda za kuisaidia Ukraine katika vita dhidi ya Urusi na juhudi za kutafuta mkataba wa kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza.
Ikulu ya Marekani imesema Rais Biden na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine watatia saini mkataba wa usalama kati ya nchi hizo mbili wakati viongozi hao watakapokutana pembezoni na mkutano huo wa kilele wa G7.
Mataifa hayo saba pia yatajadili utaratibu wa kutumia zaidi ya dola bilioni 260 za mali ya Urusi iliyozuiwa nje ya nchi hiyo tangu kuzuka kwa vita Februari 2022 kwa ajili ya kuisaidia Ukraine.
Tayari mkataba wa awali wa kutumia dola bilioni 50 za mali hizo za Urusi kuisaidia Ukraine umeafikiwa saa chache kabla ya kuanza kwa mkutano wa G7.
Ahadi zaidi za kuisaidia Ukraine kutolewa wakati wa mkutano wa G7
Suala la Ukraine liko juu katika ajenda ya mataifa saba ya Magharibi yanayotoa msaada muhimu wa kifedha na silaha kwa Kiev. Rais wa Ukraine anatarajiwa kushiriki katika mijadala hiyo mjini Puglia. Anahitaji silaha za masafa marefu zaidi, risasi na mifumo zaidi ya ulinzi wa anga.
Kansela Olaf Scholz tayari ameahidi kushughulikia upatikanaji wa mifumo zaidi ya ulinzi wa anga kutoka mataifa ya G7 na kwingineko. Kufikia sasa, baadhi ya mataifa ya Ulaya yalio na mifumo ya ulinzi wa makombora ya Patriot, kwa mfano, yamekuwa yakisita kutoao mifumo hiyo kwa Ukraine.
Mataifa ya G7 hayakubaliani juu ya kupeleka askari wa Magharibi nchini Ukraine. Ingawa Ufaransa na Uingereza ziko tayari kutuma wakufunzi na washauri, Ujerumani, Marekani na Italia zinapinga vikali hatua hii.
Olaf Scholz anataka kufikia ahadi madhubuti za ujenzi mpya wa Ukraine baada ya vita. Mataifa saba ya mkutano huo na Umoja wa Ulaya wanataka kukubaliana kuipatia Ukraine dola bilioni 50 za ziada.
Pesa hizo zitachukuliwa kama mkopo wa pamoja, ambao baadaye utalipwa polepole na mapato yatokanayo na mali za serikali ya Urusi zilizozuwiwa. Njia ya kumaliza vita pia inajadiliwa.
Hatimaye, baadhi ya wakuu wa nchi na serikali wa G7 watasafiri siku ya Jumamosi hadi Uswisi kwa mkutano wa kimataifa wa amani ulioandaliwa na Ukraine. Lakini Urusi haishiriki.
Italia imenuwia kuliweka bara la Afrika miongoni mwa ajenda za mkutano wa G7
Giorgia Meloni, mwenyekiti wa sasa wa G7, anataka kuzingatia ushirikiano bora na Afrika katika malighafi na usambazaji wa nishati, mifumo ya usambazaji na usimamizi wa uhamiaji.
Wageni 12 kutoka mataifa ya Afrika na Indo-Pacific wamealikwa kuzungumzia uwekezaji zaidi barani Afrika na uzalishaji wa pamoja wa nishati rafiki kwa mazingira barani Afrika kwa ajili ya Ulaya.
Tayari kumekuwa na mipango mingi ya Afrika ya aina hii ndani ya G7. Kilichokosekana ni ahadi madhubuti za kifedha na ushirikiano kwa usawa, lilikosoa shirika hisani la Oxfam kabla ya mkutano huo.
Kwa kutumia asilimia tatu tu ya matumizi yao ya ulinzi ya kila mwaka, Oxfam inasema mataifa ya G7 yanaweza kupambana kikamilifu na njaa barani Afrika.
Tobias Hauschild wa Oxfam Ujerumani alisema kabla ya mkutano huo, kwamba serikali za G7 zinaweza kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika silaha, lakini linapokuja suala la kukomesha njaa, zinafilisika ghafla.
Shirika la misaada ya maendeleo la ONE linalalamika kwamba dhamira ya kifedha ya nchi za Magharibi kwa Afrika imeshuka katika miaka ya hivi karibuni. Deni, kwa upande mwingine, linaongezeka kwa kasi.
Mataifa ya Umoja wa Ulaya yanazidi kuunganisha misaada yao kwa mataifa ya Afrika na fidia kwa udhibiti wa uhamiaji. EU inajaribu kukamilisha makubaliano ya uhamiaji na Libya, Tunisia, Jordan na Misri ili kuwazuia wakimbizi na wahamiaji katika nchi hizi za usafirishaji ikiwezekana. Mashirika ya misaada yanakosoa mbinu hii kwa sababu Ulaya inataka kukwepa wajibu wake.
G7 pia itaunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kusitisha vita kati ya Hamas na Israel, lililowasilishwa na Marekani.