Mpango kukabili ajira kwa watoto wazinduliwa

Mwanza. Serikali imezindua mpango mkakati wa kitaifa wa miaka mitano wa kutokomeza utumikishwaji wa mtoto wa 2024/2025 utakaotekelezwa mpaka 2028/2029.

Mpango huo umezinduliwa leo Juni 12, 2024 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Patrobas Katambi.

Katambi amezindua mpango huo  kwenye  maadhimisho ya kitaifa ya kupinga utumikishwaji wa ajira kwa watoto yaliyofanyika kitaifa wilayani Meatu mkoani Simiyu.

Katambi akizungumza katika maadhimisho hayo amesema Serikali imezindua mpango huo ikiwa ni moja ya utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa Shirika la Kazi Duniani  (ILO) namba 138 ambao unaeleza umri wa mtoto kuajiriwa na ule namba 182 unaohusu kazi hatarishi kwa mtoto.

“Serikali inazindua mpango mkakati huu kwa lengo la kutokomeza kabisa vitendo vya utumikishaji wa watoto ambao utaenda sambamba na utoaji elimu, ukusanyaji taarifa za familia na maeneo matukio yao yanapofanyika ili kuhakikisha hadi ifikapo mwaka 2029 matukio haya yawe yamepungua kwa kiwango kikubwa katika jamii,” amesema.

Hata hivyo, ametoa wito kwa viongozi wa Serikali kuhakikisha wanatekeleza mpango huo pamoja na sera na sheria zinazolenga kutokomeza vitendo hivyo ili kufikia lengo la Taifa.

“Jamii pia  ina wajibu wa kutekeleza sera na sheria za watoto kuanzia ngazi ya familia, jamii, taasisi za dini na elimu kwa kuondoa na kuacha kuwatumikisha watoto,” amesema Katambi.

Kwa upande wa Ofisa Ustawi wa Jamii wa Shirika la Kutetea Wafanyakazi wa Nyumbani (WoteSawa), Renaida Mambo amesema tangu mwaka 2018 mpaka sasa wamefanikiwa kuwaokoa watoto 130 waliokuwa wakitumikishwa kazi za ndani huku kwa mwaka 2023 pekee, watoto 12 wameokolewa mkoani Simiyu.

Mratibu wa Miradi Kitaifa, Glory Blasio akimwakilisha Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Tanzania, Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda ameipongeza Serikali kwa kuonyesha nia thabiti ya kukomesha ajira kwa watoto kwa kuzindua mradi huo.

“Pamoja na kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali bado hatujafikia azimio la kutokomeza utumikishwaji kwa asilimia 100. Kwa taswira ya kidunia watoto takribani milioni 160 bado wanatumikishwa kati ya hao milioni 72 wanatoka Afrika na kibaya zaidi asilimia 50 wanatumikishwa katika aina mbaya zaidi za utumikishwaji zinazoathiri afya, usalama na kuwaweka katika hatari ya kutostawi wakiwa watu wazima,” amesema Blasio

Kaimu wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Fauzia Ngatumbura amesema mkoa huo unaendelea kutoa elimu kwa jamii namna ya kukabiliana na tatizo hilo ili kujenga Taifa la kesho.

Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Gobogo, Anord Emmanuel amesema watoto wenzao wengi wanashindwa kutimiza ndoto ya kupata elimu, kutokana na wazazi wengi kuwatumikisha kazi hivyo kushindwa kupata muda wa kusoma.

Related Posts