Unguja. Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikitaja vipaumbele vitano katika bajeti ya mwaka 2024/25, uchumi kwa mwaka 2024 unakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 7.2 kutoka ukuaji wa asilimia 7.1 mwaka 2023.
Akisoma hotuba ya bajeti ya Serikali Juni 13, 2024, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema mapato ya Serikali kwa mwaka 2024/25 yanakadiriwa kufikia Sh5.182 trilioni ikiwa ni ongezeko la Sh2.342 trilioni sawa na asilimia 54.81 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24 ya Sh2.840 trilioni.
Waziri Dk Saada amesema matarajio ya ukuaji huo utatokana na ongezeka la watalii watakaotembelea Zanzibar kwa asilimia 30 kutoka watalii 638,498 mwaka 2023 hadi watalii 829,929 kwa mwaka 2024 kwa wageni wa kimataifa na kuongezeka kwa watalii wa ndani kwa asilimia 64.5 kutoka watalii 164,084 mwaka 2023 hadi kufikia watalii 270,000.
Pia kuendelea kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo na miradi ya ujenzi wa miundombinu itakayochangia ukuaji wa uchumi na huduma za jamii, ikiwamo miundombinu ya afya, elimu, maji safi na salama.
“Kwa Mwaka wa fedha 2024/25 kiwango cha utegemezi wa bajeti ya Serikali kinakadiriwa kufikia asilimia 6.3 kulingana na matarajio ya kupokea Sh322.95 bilioni ikiwa ni misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo,” amesema.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali inapendekeza kutoa unafuu wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa uingizaji au usambazaji wa vifaa vinavyotumiwa na watu wenye mahitaji maalumu ili kupunguza gharama za ununuzi wa vifaa hivyo, vikiwemo vitimwendo, viungo bandia, visaidizi vya kuona na kusomea, fimbo nyeupe na mashine za kutolea hati nundu.
Mbali na hilo, amesema kwa muda mrefu usambazaji wa boti umekuwa ukitozwa VAT hali inayosababisha kuongeza gharama za uwekezaji katika sekta ya uvuvi nchini.
“Hivyo, Serikali inapendekeza kutoa unafuu wa VAT kwa usambazaji wa boti zinazotengenezwa nchini,” amesema.
Amesema Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zimeanza kusajili na kuziingiza katika mfumo wa Kodi ya VAT kampuni zinazotoa huduma katika mitandao ya kijamii.
Amesema kampuni hizo zimesajiliwa katika mfumo maalumu wa kodi wenye uwezo wa kutambua muamala ulipofanyika katika pande zote za Muungano.
Kwa sasa mfumo huo unatoza kiwango cha kodi cha asilimia 18 wakati mfumo wa kodi wa VAT Zanzibar unatoza kiwango cha asimilia 15.
Amesema inapendekezwa kutoza kiwango cha asimilia 18 ya VAT kwa kampuni zinazotoa huduma katika mitandao ya kijamii ili kuondoa changamoto za utozaji wa kodi, na kulinda mapato ya Serikali.
Amesema hatua hiyo inatarajiwa kuongeza pato la Serikali kwa Sh3.75 bilioni.
Kama ilivyo kwa kampuni za biashara mtandaoni, Serikali inapendekeza kuoanisha kiwango cha utozaji wa kodi ya VAT kuwa asilimia 18 kwa huduma za bima nchini badala ya asilimia 15 iliyopo sasa hivi.
“Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mapato kwa Sh3.57 bilioni,” amesema.
Katika kuhamasisha matumizi ya gesi kwa wananchi na kupunguza madhara na athari za mabadiliko ya tabianchi, inapendekezwa kutoa msamaha wa ushuru wa bidhaa kwa uingizaji wa gesi nchini.
Serikali inapendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha Sh300 kwa kilo moja ya kuku au samaki wakati wa uingizaji ili kuhamasisha uwekezaji wa uzalishaji wa bidhaa hizo jambo litakaloongeza ajira na kuwa na ushindani wa soko la ndani.
Hatua hiyo amesema inatarajiwa kuongeza pato la Serikali kwa Sh3 bilioni.
Waziri Saada amesema Serikali inapendekeza kuongeza kiwango cha kutoza ushuru wa bidhaa za vinywaji vikali ikiwemo bia.
Ushuru wa bidhaa kwa mvinyo itatoka Sh2,466 hadi Sh4,386 kwa lita moja, ushuru wa bidhaa kwa vinywaji vingine vikali utapanda kutoka asilimia 35 hadi 70. Hatua hiyo itaongeza pato la Serikali kwa Sh1 bilioni.
Waziri Saada amesema kumekuwa na wimbi la kuongezeka kwa matumizi ya shisha na sigara za kielektroniki, hususan kwa vijana na watoto wadogo ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Kutokana na hilo, amesema Serikali inapendekeza kuongeza kiwango cha kutoza ushuru wa bidhaa kutoka asilimia 35 hadi asilimia 120.
Said Ali Issa, mtaalamu wa masuala ya uchumi amesema bajeti imejikita kuongeza ushuru lakini haijaonyesha vyanzo vya mapato.
“Nimesikia bajeti lakini ndio mfumo uleule wa kila wakati hatuoni vyanzo vipya zaidi tunaona kuongeza ushuru kwenye baadhi ya bidhaa, kwa hiyo inafanya kuendelea kuwa tegemezi ya bajeti za nje,” amesema.
Muhidini Mwinyishekha amesema wananchi wengi wanatamani kuona gharama za maisha zikipungua, hivyo kuwa na bajeti ambayo haitakuwa imewalenga itakuwa kazi ngumu.
Mfanyabiashara Khadija Yussuf amepongeza kuongeza kiwango cha Sh300 kwa kilo ya kuku na samaki wanaotoka nje akisema hatua hiyo itasaidia wafanyabiashara wa ndani kuongeza wigo wa biashara zao.