Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amevitaka vyombo vya dola na mamlaka husika kuwaonya na kuwachukulia hatua baadhi ya wanasiasa wanaotoa kauli zinazoashiria kuhatarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 13, 2024 wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma, akisema katika kuendeleza ustawi wa Watanzania na kukuza uchumi wa Taifa, umoja na kitaifa, amani na mshikamano suala la undugu ni muhimu.
Amefafanua Serikali inatambua Muungano ndiyo utaifa, bila Tanzania Bara hakuna Taifa linaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo ndio utambulisho.
Hata hivyo, Dk Mwigulu amesema hivi sasa kumezuka baadhi ya wanasiasa (hakuwataja majina), kwa sababu za kufilisika kisiasa na kutotambua unyeti wa suala hilo ambapo wamekuwa wakitoa lugha zinazopandikiza chuki dhidi ya Watanzania.
“Sote tumeshuhudia lugha za kibaguzi zikitolewa na baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa zinazohatarisha Muungano wetu. Kauli hizi zikiachwa bila kukemewa na kila mmoja wetu zina uelekeo wa kuvunja Muungano wetu na zinatishia kuvunja utaifa wetu na undugu wetu.
“Tutamaliza kubaguana kwa misingi ya Muungano na baada ya hapo tutahamia kubaguana kikabila, tutachomeana vibanda, tutanyang’anyana viwanja, tutafukuziana mifugo, tutavunja utaifa wetu,” amesema Dk Mwigulu.
Bila kuwataja wanasiasa hao, Dk Mwigulu amewataka Watanzania kuzikataa agenda za viongozi wabaguzi waliofilisika kisera, akidai hawana agenda inayoweza kuwapa uhalali kwa Watanzania mpaka watoe lugha za kibaguzi.
Ameongeza kuwa lugha hizo ni za hovyo kabisa na za aibu kutolewa na viongozi wa vyama vya siasa. Amesema vyama vya siasa vimesajiliwa kwa sharti la lazima la kuungwa mkono na pande mbili za Muungano.
“Wanasiasa wanaotafuta uhalali wa kisiasa kwa misingi ya ukabila au Utanganyika au Uzanzibar, ni wanasiasa waliofilisika kisera, hawafai, na jambo hili ni la hatari kwa Taifa letu,” amesisitiza.
“Jambo hili halikubaliki hata kidogo na wala halina afya kwa vyombo na mamlaka zote zinazohusika zitoe onyo na kuchukua hatua kali ili haya mambo yasijirudie,” amesema Dk Mwigulu.