Dar es Salaam. Taarifa ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2024/2025 inaonesha kasi ya kiwango cha mikopo chechefu kutoka asilimia 5.5 Aprili 2023 hadi asilimia 4.3 katika kipindi kinachoishia mwezi Aprili, 2024.
Kupungua kwa mikopo chechefu kulitokana na hatua mbalimbali zilizoendelea kuchukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania zikiwemo kuongeza ufuatiliaji wa utoaji mikopo na kuwaondoa wafanyakazi wa benki wasio waaminifu na kuzitaka benki na taasisi za fedha kuimarisha taratibu za utoaji na ufuatiliaji wa mikopo.
Hatua nyingine ni kuzielekeza benki kutumia ripoti za mikopo kutoka kwa kampuni za kuchakata na kutunza kumbukumbu za mikopo, utekelezaji wa kanuni za kuwalinda watumiaji wa huduma za benki kwa kuhakikisha utunzaji wa haki na usawa kwa wakopaji.
Hayo yameelezwa katika taarifa hiyo iliyowasilishwa leo bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Taarifa hiyo inaonesha pia idadi ya taasisi zilizotumia kanzidata ya wakopaji iliongezeka na kufikia 185 Aprili 2024 ikilinganishwa na taasisi 182 Aprili 2023 huku idadi ya wakopaji waliosajiliwa kwenye kanzidata ya wakopaji iliongezeka na kufikia 8,958,203 ikilinganishwa na wakopaji 5,650,384 Aprili 2023.
Mbali na kupungua kwa mikopo chechefu taarifa hiyo inaonesha mikopo ya sekta binafsi imeendelea kuwa imara katika kipindi kinachoishia mwezi Aprili, 2024, hadi kufikia ukuaji wa Sh33.7 trilioni sawa na asilimia 17.6, kutoka ukuaji wa Sh28.7 trilioni, katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Profesa Mkumbo amesema ukuaji huo ulitokana na maboresho katika mazingira ya biashara na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini.
Aidha, mikopo kwa sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 60.6, kutokana na matokeo ya hatua za kisera zilizolenga kushusha viwango vya riba pamoja na juhudi za Serikali kuongeza bajeti katika sekta ya kilimo.
“Mikopo katika sekta ya viwanda na uzalishaji ulikua kwa asilimia 29.1, uchimbaji madini (asilimia 18.1), na mikopo kwa shughuli binafsi asilimia 16.7. Katika kipindi hicho, sehemu kubwa ya mikopo iliendelea kuelekezwa katika shughuli binafsi (biashara ndogo na za kati), sawa na asilimia 37.0 ya mikopo yote, ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 12.8, kilimo asilimia 11.6 na viwanda asilimia 10.2.
“Ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi, hususan katika sekta za kilimo, viwanda na uzalishaji, na uchimbaji madini, linaashiria uimarishaji wa mazingira ya biashara na ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Hatua za kisera zilizolenga kupunguza viwango vya riba na kuongeza bajeti katika sekta muhimu kama kilimo zimeonekana kuwa na matokeo chanya katika kuchochea ukuaji huu.” imeeleza taarifa hiyo.