Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inafanya tathmini ya mashamba na viwanda vilivyobinafsishwa na vitakavyobainika kuwa havifanyi kazi vitarejeshwa kwa umma.
Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 13, 2024 wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Thimotheo Mzava.
Amesema kwa nyakati tofauti wameshuhudia kusimama kwa ghafla kwa uchakataji na usindikaji wa mazao kwa viwanda ambavyo vilikuwa vya umma vikabinafsishwa na kutolea mfano viwanda vya chai.
“Pamoja na kuwa na sababu na visingizio vingi lakini sababu kubwa inaonyesha sababu kubwa ni uwekezaji na uendeshaji usioridhisha. Mheshimiwa Waziri Mkuu nataka kujua Serikali haioni umuhimu wa kufanya tahmini ya kina kwa viwanda na mashamba yaliyobinafsishwa ili tuweze kuokoa uchumi na kuwasaidia wananchi wetu,” amehoji.
Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema baada ya kubinafsisha wamegundua watu waliowapa mali hizo mashamba na viwanda wapo ambao hawafuati masuala waliyokubaliana nayo.
Amesema kazi ambayo inafanywa na Wizara ya Kilimo ni kufanya upembuzi kwa maana ya tathmini ya watu wote waliopewa mashamba hayo kwa masharti waliokubaliana viendelee lakini wako walioshindwa kabisa.
“Tathimini hii inayofanywa na Wizara ya Kilimo inapelekea kuja kufanya maamuzi ya wale wote waliopewa viwanda na mashamba haya lakini hawajaendeleza hadi leo,” amesema.
Amesema mara kadhaa Kamati za Kudumu za Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Mifugo na Kilimo imepita maeneo mengi na kugundua migogoro kati ya wananchi na wawekezaji ambao hawajaitumia ardhi kwa muda mrefu.
Amesema tathmini hiyo itasababisha Serikali kutoa maamuzi ya kurudisha ili waweze kuyaendeleza kama sekta ya umma ama kutoa kwa mwekezaji mwingine ambaye anahitaji kuwekeza ili aweze kuendeleza.
“Nami natambua kuwa mheshimiwa Mzava kule kwake anakiwanda cha chai eneo la Mponde, nimeenda mara kadhaa kuona uwekezaji ule wa sekta binafsi ambaye tumebinafsisha lakini ameshindwa kabisa. Tumekirudisha na tumeipa taasisi yetu ya PSSSF (Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma) na NSSF (Shirika la Hifadhi ya Jamii.
Hatua hizo zinapelekea kufanya maamuzi na maamuzi yake ni kuzinyanganya na tutawapa wengine wanaoweza kuendeleza mashamba haya.”
Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Chakoma amesema Serikali imekuwa ikiwekeza asilimia moja ya bajeti ya sekta elimu katika masuala ya ubunifu na teknolojia.
“Serikali ina mkakati gani zaidi katika kuongeza na kuimarisha ubunifu, sayansi na teknolojia ili kuimarisha sekta nzima ya elimu,” amesema.
Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema Serikali kuna utaratibu wa kuwakusanya pamoja wabunifu katika masuala ya sayansi na teknolojia.
“Jukumu hili la Serikali linao uwekezaji na sasa kinachofanyika chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni kuhakikisha kuwa uwekezaji huu tunaupanua tunaongeza kama ni asilimia moja. Tunaamini kwenye uwekezaji wetu huo katika eneo hilo tutaongeza kwa sababu tumeona kuna faida,” amesema.
Amesema Serikali imeanza kuwahudumia wabunifu ambao pia wanafanya shughuli zao kwa kuanza na utafiti. Hivyo wameimarisha kitengo cha utafiti kinachosababisha watu kutafiti kwenye maeneo mbalimbali na baadaye kubuni jambo ambalo linawaletea faida katika majukumu yao.
Majaliwa amesema mkakati uliopo hivi sasa ni kuhamasisha ubunifu kwenye sayansi na teknolojia kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu mpaka wale walioko uraiani.
Amesema Serikali inaendelea kuongeza bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambako ndiko wanasimamia masuala ya sayansi, ubunifu na teknolojia ili kuwezesha sekta hiyo iweze kukua.