TETESI ZA USAJILI BONGO: Thabang Sesinyi kupishana na Okrah

COASTAL Union imeanza mazungumzo ya kumsajili winga wa Jwaneng Galaxy ya Botswana, Thabang Sesinyi ili kuongeza nguvu msimu ujao hasa kwa Kombe la Shirikisho Afrika.

Sesinyi ni pendekezo ya Kocha Mkuu, David Ouma anayemhitaji mchezaji anayemudu wingi zote mbili ili aweze kuwasaidia CAF.

BECHEM United ya Ghana imepanga kumrejesha nyumbani winga wa Yanga, Augustine Okrah aliyeonekana kutokuwa katika mipango ya kocha Miguel Gamondi. Imeripotiwa Waghana wamefungua milango kwa winga huyo aliyefanya vizuri akiwa na timu hiyo kabla ya kurejea Tanzania wakati wa dirisha dogo, awali aliichezea Simba.

INADAIWA Yanga imeanza mazungumzo na Singida Black Stars kwa ajili ya kumpata kipa wa timu hiyo, Khomeiny Aboubakar. Khomeiny amekuwa na msimu mzuri na kikosi hicho, anatajwa kama mbadala wa Metacha Mnata anayeondoka baada ya kuhudumu kwa miezi sita ya mkopo na Yanga inamtaka iwapo itamkosa Yona Amos Prisons.

AZAM FC inadaiwa ipo katika mazungumzo na nyota wa zamani wa timu hiyo, Wazir Junior kuona kama watafikia makubaliano ya kupata saini kwa ajili ya msimu ujao, japo inaelezwa kiu aliyonayo ni kucheza nje. Waziri amekuwa na msimu mzuri akiwa ndiye straika mzawa pekee aliyefunga mabao mengi (12).

MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars, Ismail Mgunda yupo katika mazungumzo na Simba ili kujiunga na kikosi hicho msimu ujao. Mgunda aliyemaliza na mabao sita ya Ligi Kuu, amefuatwa na viongozi wa Simba ili akaichezee, ikielezwa mazungumzo yanaendelea Singida ikiwa tayari kumuachia.

BAADA ya Simba Queens kumtoa kwa mkopo wa miezi sita aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Joelle Bukuru kwenda Fountain Gate Princess iko kwenye mpango wa kumrejesha kikosini hapo. Inaelezwa Simba imefikia maamuzi ya kumrudisha mrundi huyo aliyedumu Simba kwa takribani misimu mitano kikosini hapo tangu aliposajiliwa 2019.

YANGA Princess imeanza mazungumzo na Zesco Ndola Girls ya Zambia juu ya kumsajili moja kwa moja winga wa timu hiyo, Mary Mbewe. Kiraka huyo alisajiliwa Yanga kwa mkopo wa miezi sita kupitia dirisha dogo lililofungwa  anuari mwaka huu na viongozi wa timu hiyo wamenogewa na huduma ya mchezaji huyo wakitaka kumunuanua moja kwa moja.

Related Posts