Vijana 30,000 waguswa tamasha Twenz’etu kwa Yesu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Zaidi ya vijana 30,000 wamebadili maisha yao kupitia tamasha linaloandaliwa kila mwaka na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Tamasha hilo lijulikanalo kama ‘Twenz’etu kwa Yesu’ lilianza mwaka 2014 limekuwa likiwakutanisha vijana wa dini na madhehebu mbalimbali kutoka Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Naibu Katibu Mkuu KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Wilbroad Mastahi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tamasha la Twenz’etu kwa Yesu, Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Upendo Media, Neng’ida Johanes.

Akizungumza leo Juni 13, 2024 Naibu Katibu Mkuu KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Wilbroad Mastahi, amesema tamasha la mwaka huu litafanyika Juni 15, katika viwanja vya Tanganyika Packers vilivyopo Kawe, Dar es Salaam.

Amesema lengo la tamasha hilo ni kuwabadilisha vijana kuwa na mtazamo chanya katika kumjua Mungu katika uchumi na uzalendo kwa taifa na kuwasisitiza wazazi na walezi kuendelea kuwaunga mkono waweze kushiriki.

“Nia ya kanisa ni kusaidia vijana, kupitia tamasha hili watapokea ujumbe wa neno la Mungu utakaowasaidia kufanya maamuzi yenye tija kwa taifa na tunaona wengi wana shauku ya kujua habari za Mungu na wengi ni wahitaji ndiyo maana kila mwaka tunaendelea kuandaa,” amesema Mchungaji Mastahi.

Amesema kwa mwaka huu tamasha hilo pia litafanyika katika Mkoa wa Mbeya uwanja wa Sokoine (Juni 29) na Shinyanga (Agosti 10) uwanja wa Kambarage.

“Tunasema tamasha la Twenz’etu kwa Yesu linakua kwa sababu tunaona maelfu ya vijana wa dini na madhehebu mbalimbali wakishiriki kila mwaka na wapo wengi wanaotoka katika mikoa ya jirani,” amesema.

Kwa mujibu wa Mchungaji Mastahi, mnenaji katika tamasha hilo atakuwa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kati (Singida), Dk. Syprian Hilint.

Related Posts