Dar es Salaam. Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema miongoni mwa maeneo yatakayopewa kipaumbele katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 ni pamoja na kukamilisha miradi ya kielelezo na kimkakati.
Maeneo mengine ni pamoja na kuimarisha rasilimali watu hasa sekta za huduma za jamii, kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji katika sekta binafsi.
Dk Mwigulu ameeleza hayo leo Alhamisi Juni 13, 2024 wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025 bungeni jijini Dodoma.
“Maeneo mengine ya muhimu katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25 ni kugharamia mishahara ya watumishi wa umma; deni la Serikali, uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024 na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
“Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na maandalizi ya michuano ya mpira wa miguu ya mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja,” amesema Dk Mwigulu.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 imelenga kutekeleza vipaumbele vilivyozingatia maeneo yaliyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya ‘kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25.
“Maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa katika mpango ni pamoja na kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza biashara na uwekezaji kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu,” amesema Dk Mwigulu.