Wadau wafunguka matamanio yao bajeti ya Serikali 2024/25

Dar es Salaam. Wasomi, wataalamu wa uchumi na wananchi wanatamani kuona bajeti ya Serikali ya Tanzania mwaka 2024/25 ikijikita zaidi katika kuongeza wigo wa kodi, uchaguzi wa Serikali za mitaa na kukuza sekta ya kilimo na afya.

Bajeti hiyo itasomwa Alhamisi ya Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.

Wadau hao wameyasema hayo leo Jumatano Juni 12, 2024 katika mjadala wa Mwananchi X Space zamani (twitter) uliokuwa na mada isemayo ‘Kuelekea bajeti ya Serikali 2024/25 yepi matarajio yako? Ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Philbert Komu amesema matarajio yake ni kuona bajeti itakayohusisha uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu akisema ni bajeti muhimu hasa katika kuangalia falsafa za Rais Samia Suluhu Hassan za 4R ya namna ya kuendesha chaguzi.

Tangu ashike madaraka Machi 19, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitumia falsafa ya R nne maana yake ni maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebulding).

“Tunatarajia mageuzi makubwa hasa katika uendeshaji chaguzi hasa za Serikali za mitaa kwa sababu ndiyo zitaleta hamasa kwa watu kushiriki uchaguzi mwakani. Bajeti iweke mwanga wa uchaguzi mwakani na ijikite kuwezesha uchaguzi huu unaotangulia wa Serikali za mitaa,” amesema Dk Komu.

Dk Komu amesema mambo mengine anayoyatarajia ni kusikia miongoni mwa vipaumbele vilivyotolewa katika bajeti kama kuwezesha Tume Huru ya Uchaguzi, demokrasia vikichukua nafasi katika bajeti hiyo.

Awali, akichokoza mada hiyo, Mhariri wa Uchumi wa Gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu amesema bajeti hiyo ni maalumu wakati huu ambao Taifa linaendelea kujifunza kutoka katika changamoto mbalimbali za mabadiliko tabianchi, mvua nyingi zilizoharibu miundombinu, ongezeko la gharama la uchukuzi na usafirishaji wa mizigo kutoka mataifa mbalimbali kuja nchini.

“Wananchi wengi wanaamini kodi ikipungua watapa unafuu, lakini wazalishaji wa ndani wanatamani Serikali iweke ulinzi katika bidhaa zao za ndani, lakini wananchi wangependa kuona gharama za mawasiliano zikipungua maana zipo juu.”

“Watu wanatarajia Serikali ingeshughulikia tatizo la mawasiliano ili kufanya shughuli za kiuchumi. Pia wana matarajio kwamba nishati hasa mitungi ya gesi ikishuka, wangependa kusikia baadhi ya bidhaa zikishushwa bei ili kuleta unafuu katika maisha yao ya kila siku kutokana na changamoto wanazokuta nazo,” amesema Bahemu.

Rais wa zamani wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Elisha Osati amesema anatarajia kuona bajeti hiyo ikijibu kitendawili cha namna Watanzania wote watakavyoweza kuingia katika matumizi ya bima ya afya.

“Kwa sisi madaktari inaumiza kuwa na mgonjwa mbele yako unaona kabisa huyu mgonjwa alipaswa kuhudumiwa namna hii lakini hawezi kulipa gharama za matibabu hii inaumiza sana,” amesema.

Mbali na hilo, Dk Osati amesema angependa kuona bajeti hiyo ikienda kutatua changamoto mbalimbali akisema jitihada kubwa zimefanyika katika ujenzi wa hospitali za wilaya na kikanda na lakini bado kuna majengo mengi ni maboma.

“Baadhi ya hospitali zinafanya kazi lakini ujenzi haujaisha, wafanyakazi hawajapelekwa kulingana na mahitaji  na upatikanaji wa vifaatiba na dawa bado hautoshelezi.”

“Hospitali za rufaa upatikanaji wa dawa kwa sasa ni asilimia 76 hadi 78, upungufu bado upo, mwananchi anataka akienda hospitali anachoangalia amepata dawa na huduma, ametibiwa, natamani kuona mwananchi anapata huduma kwa bei nafuu kwa muda mfupi na iliyo bora,” amesema Dk Osati.

Mmoja wa wachangiaji katika mjadala huo, Clay Mwaifwani amesema anatamani kuona bajeti hiyo ikionyesha mwanga wa kuwa na watu wengi wanaoweza kulipa kodi.

“Bajeti ya Serikali itatuongoza katika njia hiyo, kwa sasa mzigo mkubwa upo kwa watu ambao vipato vyao vinaweza kufikiwa moja kwa moja ikiwemo wafanyakazi, lakini pia bajeti iongeze wigo wa ulinzi wa mazingira ili kuondoka na uharibifu wa miundombinu inayojitokeza kutokana na mvua na mabadiliko tabianchi,” amesema Mwaifwani.

Mkurugenzi wa Malembo Farm, Lucas Malembo amesema anatamani kuona asilimia 10 ya bajeti ya Serikali ikielekezwa katika sekta ya kilimo akisema bajeti nyingi zimekuwa zikishindwa kufikia lengo hilo licha ya kuwapo kwa ongezeko katika bajeti sekta hiyo.

“Suala la tija linapaswa kuangaliwa bado tuko katika kiwango kidogo ukilinganisha na mataifa yanayotuzunguka, mahindi yanachukua asilimia 70 ya nafaka zote zinazozalishwa nchini na wakulima zaidi ya milioni 10 wanasadikiwa kuzalisha zao hilo lakini tija ni ndogo,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa Chama cha ACT- Wazalendo, Abdul Nondo amesema angependa kuona vyuo vyote vya kati vinafutiwa ada ili elimu ya Tanzania iwe ya kuongeza ujuzi.

“Tunapotoa kipaumbele kwenye vyuo vya kati tuhakikishe vyote vinafutiwa ada siyo vyuo kadhaa vinafutiwa na vingine ada inabaki, lakini utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu bado kuna changamoto

“Matarajio yetu ni kuona bajeti ya kesho inajibu ili wanafunzi waliofika vyuo vya kati  waweze kufika vyuo vikuu na kunufaika na mikopo hiyo,”amesema Nondo.

Hata hivyo, Said Rashid amedai bajeti nyingi zipo katika makaratasi na si utekelezaji:“Mfano katika afya, zahanati imejengwa kwa nguvu za wananchi lakini hata bajeti ya kupeleka umeme, jenereta au sola hakuna.”

“Zahanati inaweza kuendeshwa kibubu, wizara inapeleka friji na dawa lakini unajiuliza hizi dawa zinafanyaje kazi,” amedai.

Related Posts