Wanaume vinara idadi ya watafuta kazi ikiongezeka

Dar es Salaam. Serikali kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira ilisajili watu wanaotafuta kazi 17,107 katika mwaka 2023 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 62.3 la watafuta kazi waliokuwapo mwaka uliotangulia.

Hiyo ni baada ya watafuta kazi 10,540 kusajiliwa mwaka 2022 na kupatiwa ushauri nasaha kuhusu uchaguzi wa kazi na mafunzo ya kushindania fursa za ajira.

Hayo yameelezwa katika kitabu cha Hali ya Uchumi 2023 kilichosomwa leo Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo katika watafuta kazi waliosajiliwa mwaka 2023 wanaume walikuwa 8,902 na wanawake 8,205.

“Katika kipindi hicho, watu 10,847 ambapo wanaume 6,025 na wanawake 4,822 walipata mafunzo ya kushindania fursa za ajira ikilinganishwa na watafuta kazi 5,161 waliopata mafunzo husika mwaka 2022,” amesema Profesa Mkumbo.

Profesa Mkumbo amesema mafunzo hayo yalitolewa kwa ajili ya kuwajengea uwezo watafuta kazi kushindania fursa za ajira ndani na nje ya nchi pamoja na kujenga maadili ya kazi yanayohitajika na waajiri mbalimbali.

“Vilevile, vijana 311 waliunganishwa na fursa za kazi kwa waajiri mbalimbali nchini ikilinganishwa na vijana 909 waliounganishwa na kazi mwaka 2022,” amesema Profesa Mkumbo.

Wakati watafuta kazi hao wakisajiliwa mwaka 2023, vijana 2,895  ambao ni wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo waliunganishwa kwa waajiri kufanya mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa kipindi cha miezi 12.

Mafunzo hayo yalilenga kuwapatia uzoefu wa kazi na kujenga stadi muhimu za kuongeza tija na ufanisi kazini ikilinganishwa na vijana 3,231 mwaka 2022.

“Katika mwaka 2023, kitengo cha huduma za Ajira kiliunganisha Watanzania 2,529 kwenye fursa za kazi nje ya nchi,” amesema Profesa Mkumbo.

Kufuatia hali hiyo imeelezwa kuwa Serikali iliendelea kutekeleza Programu ya Taifa ya ukuzaji ujuzi kwa vijana kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

“Katika kipindi hicho, vijana 10,220 walipata mafunzo ya ujuzi unaohitajika katika soko la ajira ili waweze kuajiriwa na kujiajiri ikilinganishwa na vijana 21,586 waliopata mafunzo mwaka 2022,” amesema.

Kati ya hao, vijana 4,273 walipata mafunzo ya uanagenzi (ufundi stadi vyuoni, uchumi wa buluu, unenepeshaji wa mifugo na Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora – BBT).

Pia wafanyakazi 1,593 wa sekta ndogo ya utalii na ukarimu pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati walipata mafunzo ya kukuza ujuzi na wahitimu 4,354 walipata mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi.

Related Posts