Mtwara. Wamekwaa kisiki. Haya ndiyo maneno unayoweza kuelezea namna vinara wa wawili wa kimataifa wa usafirishaji wa dawa za kulevya, walivyokwaa kisiki kortini kupinga hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya Sh14.2 bilioni.
Hukumu hiyo imetolewa Juni 11, 2024 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania iliyoketi Mtwara, Rehema Kerefu, Sam Rumanyika na Agnes Mgeyekwa ambao walizitupa sababu zote 11 za rufaa walizokuwa wamewasilisha.
Wauza unga hao, Athman Nyamvi au Ismail Adam na Ahmad Mohamed au Hemed Said, walikamatwa Januari 12, 2012 katika Kijiji cha Mchinga II kilichopo Wilaya ya Lindi, wakisafirisha kilo 110 za dawa za kulevya aina ya Heroin zenye thamani ya Sh496.9 milioni.
Katika shtaka la pili, wawili hao walikamatwa na gramu 200,531 sawa na kilo 2,000 za mchanganyiko wa dawa za kulevya aina ya Heroin na Cocaine zenye thamani ya Sh9 bilioni, zilizoingizwa nchini kutokea nchini Afrika Kusini.
Itakumbukwa, mbali ya wauza unga hao, alikuwapo kinara wa biashara hiyo, Ally Hatibu maarufu Shikuba, ambaye hata hivyo alifutiwa mashtaka hapa nchini na baadaye kusafirishwa kwenda Marekani alikokuwa akihitajiwa.
Hata hivyo, Agosti 2019, Shikuba na Watanzania wengine wanane walitiwa hatiani kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin nchini Marekani na kuhukumiwa vifungo tofauti jela huku Shikuba yeye akihukumiwa kwenda jela miezi 99.
Athman Nyamvi na Ahmad Mohamed ambao kesi yao iliendelea hapa Tanzania mbele ya Jaji Isaya Arufani wa mahakama Kuu kanda ya Mtwara baada ya kusikiliza mashahidi 10 wa Jamhuri, aliwatia hatiani kwa makosa yote mawili.
Kwa kosa la kwanza na la pili la kusafirisha kilo zaidi ya kilo 2,110 za dawa za kulevya Heroin na Cocaine, Jaji Arufani aliwahukumu kutumikia kifungo cha miaka 20, lakini kwa kosa la kwanza akawahukumu pia kulipa faini ya Sh745.4 milioni.
Katika kosa la pili la kusafirisha kilo 2,000 za dawa za kulevya mchanganyiko wa Heroin na Cocaine zilizokuwa na thamani ya Sh9.0 bilioni, Jaji huyo akawahukumu wauza unga hao kulipa faini ya Sh13.5 bilioni kwa kosa la kusafirisha dawa hizo.
Hata hivyo, wakitetewa na mawakili Majura Magafu na Hudson Ndusyepo, walikata rufaa mahakama ya Rufani Tanzania kupinga hukumu hiyo, awali wakiwa na sababu 10 za rufaa na baadae wakaongeza sababu nyingine 11 za Rufaa.
Rufaa ilipoanza kusikilizwa, wakili Magafu akaachana na sababu zote za nyongeza isipokuwa sababu ya nne ambayo ilisema maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Ahmad Mohamed, yalikiuka kifungu cha 50 na 51 na CPA cha mwaka 2002.
Namna ‘wazungu wa unga’ walivyodakwa
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Salimin Shelimoh kutoka Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya (ADU), alipokea taarifa fiche kuwa kuna shehena ya dawa za kulevya itapakuliwa Kunduchi jijini Dar ikitokea Afrika Kusini kwa meli.
Kulingana na taarifa hizo, shehena hiyo ingepokelewa na kinara wa biashara ya dawa za kulevya Ally Hatibu maarufu kama Shikuba ambapo makachero wa Jeshi la Polisi walifanya upelelezi na kujipanga kwa ajili ya kuwakamata washukiwa.
Hata hivyo, ilikuja kubainika baadaye kuwa kituo cha kushukia shehena hiyo kilikuwa siyo tena Kunduchi bali ni Kijiji cha Mchinga kilichopo Pwani ya Lindi, na ingesafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa gari Toyota Land Cruiser T921 BPY.
Kwa kufanyia kazi taarifa hiyo mpya, makachero hao walisafiri hadi Lindi na kuungana na makachero wengine wawili wa Lindi ili kuwaongezea nguvu ambapo ni katika kamatakamata hiyo huko Lindi walimtia nguvuni Shikuba.
Ilielezwa kuwa baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam kutoka Afrika Kusini, mrufani wa kwanza, Athman Nyamvi, alimchukua rafiki yake wa kike na kwenda naye Lindi na kupangisha chumba namba 104 katika hoteli ya kitalii ya Lindi Oceanic Hotel.
Januari 10,2012, mrufani wa pili, Ahmad Mohamed alifika hotelini hapo akiwa na gari lakini alipowaona polisi wanaelekea upande wake, aliliacha gari na kuamua kutembea kwa miguu lakini kabla hajafika mbali alidondoka na kukamatwa.
Katika mahojiano ya awali, aliwaeleza makachero hao kuwa kuna dawa za kulevya zimehifadhiwa nyumbani kwa dada aitwaye Pendo Cheusi ambaye ni mama yake mzazi anayeishi Mchinga II, ingawa mama yake huyo alikuwa hafahamu chochote.
Pia akawaeleza kuwa mrufani wa kwanza, Athman Nyamvi alikuwa na rafiki yake wa kike chumba namba 104 katika Hoteli ya Lindi Oceanic ambapo polisi walikwenda na kufanikiwa kuwakamata kumkamata pamoja na vitu mbalimbali.
Vitu hivyo ni pamoja na simu tano ambapo tatu zilikuwa zikilimiliwa na mrufani wa kwanza, na mbili za mpenzi wake, tiketi ya ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara, fedha aina ya Rand 50 za Afrika Kusini na Dola 12,000 za Marekani.
Mrufani wa kwanza na mpenzi wake waliwekwa mahabusu kituo kikuu cha Polisi Lindi huku mrufani wa Pili akiwaongoza polisi hadi nyumbani kwa mama yake ambako kulikutwa kasha lenye paketi 210 zikiwa na dawa hizo za kulevya.
Washitakiwa hao walikanusha tuhuma na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya huku mrufani wa pili akikana maelezo yake ya onyo aliyoandika polisi akisema aliyaandika baada ya kuteswa na polisi ili akiri kutenda kosa hilo.
Pamoja na utetezi wao huo, baada ya Jaji kusikiliza Ushahidi wa pande zote mbili, aliwatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela kwa kila kosa na kulipa faini ya Sh745,490,250 kwa kosa la kwanza na Sh13,535,869,500 kwa kosa la pili.
Walivyokata rufaa, ilivyotupwa
Hawakuridhika na hukumu hiyo iliyotolewa Novemba 29,2021 na Jaji Arufani, wakaamua kukata rufaa kupinga hukumu hiyo wakiegemea sababu 11 ambazo ni pamoja na upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha shitaka hilo.
Sababu nyingine ni pamoja na maelezo ya kosa hayakueleza kosa wanaloshitakiwa nalo na mashahidi namba 4, 7 na 10 hawakuondoa dosari hiyo na sababu nyingine ni kuwa dosari hiyo katika hati ya mashtaka ilienda hadi kwenye mzizi wa kesi.
Pia, wakajenga hoja kuwa upekuzi, ukamataji na uhesabuji na ufungaji wa dawa hizo za kulevya haukuwa sahihi kisheria kwani haukuwahusisha warufani hao na kwamba mnyororo wa uhamishaji vielelezo kutoka eneo moja ulivunjika.
Mbali na hoja hizo, lakini walisema Ushahidi wa shahidi namba 4,6,7 na 10 ulikuwa ni wa maofisa wa Polisi ambao sheria inataka uungwe mkono na mashahidi huru na pia Jaji alichambua vibaya Ushahidi na kufikia hitimisho baya.
Majaji baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, walikubaliana na hoja za Wakili wa Serikali Mkuu, Wilbroad Ndunguru aliyesaidiana na mawakili waandamizi wa Serikali, Credo Rujgaju na Faraja George, waliojenga hoja kupinga hoja za warufani.
Mawakili hao wa Serikali walichambua Ushahidi na kueleza kuwa upande wa mashitaka hayo uliweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya warufani kwa viwango vinavyokubalika na bila kuacha mashaka, hoja ambayo ilikubaliwa na majaji.