Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa mwelekeo wa mpango wa maendeleo 2024/25 ikijielekeza katika miradi mikubwa mitano ya kimkakati.
Akisoma mwelekeo wa mpango huo leo Alhamisi Juni 13, 2024 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema miradi ya kimkakati imepangwa kwa kuzingatia umuhimu na faida zitakazopatikana.
Mipango hiyo ni kutumia fursa za uchumi wa buluu, mazingira wezeshi na uimarishaji wa miundombinu, mageuzi ya kiuchumi, kukuza rasilimali watu, huduma za kijamii, kuimarisha utawala na uhimili wa kiuchumi.
Amesema utekezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kugharimu Sh2.087 trilioni sawa na asilimia 63.98 ya bajeti ya maendeleo ya Sh3.263 trilioni.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta ya uchumi wa buluu katika ukuaji wa Taifa na masilahi ya wananchi kiujumla, Serikali itaendelea kutilia mkazo katika utekelezaji wa sera na mikakati ya kuendeleza utalii wa baharini na visiwani kwa kushajihisha miradi ya uwekezaji katika visiwa,” amesema.
Pia amesema kuendeleza ujenzi wa hoteli za nyota tano, kuweka miundombinu ya kufanikisha michezo ya bahari pamoja na kuanza maandalizi ya usafiri wa baharini (sea taxis).
Pia, itaimarisha uvuvi na Rasilimali za Bahari kwa kuimarisha mazingira ya bahari, kusimamia upatikanaji wa meli za uvuvi, kujenga uwezo wa usimamizi wa rasilimali za bahari, kuimarishwa kwa upatikanaji wa mazao ya baharini ikiwemo ukulima wa mwani, kusimamia upatikanaji wa mifumo ya kuhifadhia mazao ya baharini sambamba na kuendelea na ujenzi wa majiko na masoko ya samaki ya kisasa.
Vilevile, katika eneo hili miundombinu ya bandari itaendelezwa ambapo Serikali imedhamiria kuanza ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, kusimamia na kuratibu ujenzi wa jengo la abiria la Mpigaduri na bandari ya mizigo ya Fumba.
Kwa umuhimu wa kipekee Serikali itaendelea kuiimarisha sekta ya mafuta na gesi asilia kwa kuimarisha Kampuni ya Mafuta ya Zanzibar (ZPDC) pamoja na kusimamia uwekezaji wa miundombinu ya uhifadhi wa mafuta na gesi Mangapwani. Sh453.03 bilioni zinatarajiwa kutumika kutekeleza shughuli hizo.
Amesema Serikali itaendelea na kasi yake ya kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, nchi kavu na majini. Kwa mwaka 2024/2025, Serikali itaendelea na ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Pemba, ujenzi wa jengo la abiria Terminal II la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), ujenzi wa barabara mbalimbali Unguja na Pemba zenye urefu wa kilomita 782.9 zikiwemo barabara kuu, mijini, vijijini na za ndani.
Waziri Saada amesema katika kuhakikisha Taifa linakuwa na uchumi wa kidijitali miundombinu ya uchumi huo itaendelea kuimarishwa sambamba na mifumo ya usimamizi wa fedha na uendeshaji wa shughuli za Serikali.
“Serikali itaendelea kuimarisha biashara na viwanda kwa kuweka miundombinu kwa ajili ya ujenzi wa maeneo ya viwanda na kuyaimarisha maeneo huru ya kiuchumi ili kuweza kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Sh65.32 bilioni zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa shughuli hizo,” amesema.
Amesema upatikanaji wa huduma bora na sahihi za kijamii ni miongoni mwa viashiria muhimu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa, hivyo kwa mwaka 2024/2025, kwa upande wa sekta ya afya Serikali itaendelea na uimarishaji wa miundombinu ya afya kwa kuendelea na ukarabati na utanuzi wa Hospitali ya Rufaa ya MnaziMmoja,
Ujenzi wa nyumba za madaktari, Hospitali ya Binguni na ukarabati wa vituo vya afya.
Kwa upande wa sekta ya elimu Serikali itaendelea kutekeleza mageuzi ya sekta hiyo kwa kujenga mabweni, madarasa 1,000, kukarabati shule na kutanua Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza).
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama ili kuhakikisha nchi inaendelea kubakia katika hali ya utulivu na amani.
“Katika eneo hili Serikali imekusudia kuweka mazingira mazuri ya kutoa na kupokea huduma kwa kuendelea na ujenzi na ukarabati wa Ofisi za Serikali, kuanza ujenzi wa mji wa Serikali, pamoja na ofisi za wakuu wa mikoa, wilaya na ofisi za masheha,” amesema.
Pia, amesema jitihada za kuimarisha utawala bora kupitia upatikanaji wa haki za raia na usawa zinaendelea kupewa kipaumbele ambapo Serikali kwa sasa inaendelea na ujenzi na ukarabati wa mahakama za wilaya na mikoa Unguja na Pemba sambamba na uwekaji wa mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa kesi. Sh83.62 bilioni zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kutekeleza shughuli hizo.
Amesema Serikali imetilia mkazo wa malengo matano kati ya 17 yakiwamo kuondoa umasikini kila mahali, kukomesha njaa kwa kufikia usalama wa chakula na kuboresha lishe na kukuza kilimo endelevu na lengo na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake.
Pia kukuza jamii zenye amani na umoja kwa maendeleo endelevu, kutoa upatikanaji wa haki kwa wote na kujenga taasisi zenye ufanisi, uwajibikaji na umoja katika ngazi zote, kukuza ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu.
Kamati ya bajeti ya Baraza la Wawakilishi iliisisitiza Serikali kuyafanyia kazi kwa upekee maeneo ambayo wakati wa mijadala ya bajeti za wizara yalionekana kuwagusa wawakilishi wengi na wengine kuchangia kwa hisia na msisitizo mkubwa.
Mwenyekiti wa kamati ya bajeti, Baraza la Wawakilishi, Mwanaasha Khamis Juma amesema kamati imeona ni vyema kuyapa uzito maeneo hayo kwa kuyakumbushia pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali ili iweze kuyafanyia kazi kwa weledi na haraka,hatimaye kufikia malengo ya kupata ufanisi katika utekelezaji wa bajeti na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ametaja baadhi ya maeneo hayo ni ofisi ya Makamu wa Pili kuendelea kusimamia mfumuko wa bei na kuhakikisha inaweka mikakati thabiti ili kuudhibiti ikiwemo kufanya mabadiliko katika sekta ya kilimo na kuelekea katika kilimo cha kisasa.
Katika ofisi ya Makamu wa Kwanza jambo lililogusa hisia ni uharibifu wa mazingira na changamoto za uchimbaji mchanga holela na kuwapatia mikopo watu wenye ulemavu.
Kwa upande wa masoko ya Jumbi, Chuini na Mwanakwerekwe, wajumbe walisisitiza juu ya umuhimu wa Serikali kufanya ufunguzi wa masoko hayo kwa haraka pamoja na kuzingatia uendeshaji wake, utaratibu wa kuyafanyia ukarabati kwa muda utakaohitajika pamoja na kuangaliwa utaratibu ulio wazi katika ugawaji wa sehemu za kufanya biashara kwa wananchi wanaohitaji.
“Katika wizara ya ujenzi wajumbe wengi walichangia kukamilisha ujenzi wa barabara hususani kisiwani Pemba na uwanja wa ndege wa Pemba ili kukifungua kisiwa hicho.
Pia suala la kuimarisha na kuvitangaza vivutio vya utalii ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea Zanzibar limesisitizwa na wajumbe walipokuwa wakichangia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale.
Ili kuimarisha utalii Zanzibar, Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara, usafiri, na huduma za afya.
Katika Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji lililosisitizwa ni makusanyo ya kutoka Serikali za Mitaa kwa ajili ya kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Kamati inashauri kusimamia taratibu za kutoa fedha hizo kwa makundi yaliyokusudiwa, kuwajengea uwezo wa namna ya kuzitumia na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kuzirudisha kwa wakati ili ziwanufaishe na wengine.
Wizara ya Elimu na Mafunzo, wajumbe walichangia kwa wingi kuhusu mtaala mpya wa elimu kwa ngazi ya elimu ya maandalizi na msingi, hivyo kutakiwa vitabu ambavyo vipo katika hatua ya uchapaji kuhakikisha vinapatikana haraka wanafunzi wavitumie.
Ujenzi holela, migogoro ya ardhi vilijadiliwa na wajumbe wengi hivyo kamati kuishauri Serikali kuhakikisha inaandaa utaratibu mzuri kupunguza changamoto hiyo.
Katika Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo michango ya wajumbe wengi iligusia suala la Serikali kuwekeza fedha nyingi katika kilimo cha umwagiliaji Unguja na Pemba.
Katika Wizara ya Afya ilisisitiza suala la kuwepo kwa uhaba wa wakunga katika vituo vya afya na hospitali hali ambayo husababisha waliopo kuzidiwa, hivyo Serikali imeshauriwa kuongeza ajira za wakunga.
Katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wajumbe wengi walisisitiza suala la vitendo vya udhalilishaji huku wakisikitishwa na namna kesi zake zinavyoendeshwa.
Ukosefu boti kubwa za kisasa ni mjadala uliotawala katika Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi wengi wakisema zingewasaidia wavuvi wadogo kuendesha shughuli zao.
Serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto hii kwa kuwekeza katika ununuzi na usambazaji wa boti hizo.
Kutopatikana kwa huduma ya maji kwa wananchi katika maeneo mengi ilikuwa hoja kubwa katika bajeti ya Wizara ya Maji, Nishati na Madini hivyo Serikali kutakiwa kuimarisha miundombinu hiyo.
Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ilisisitiza juu ya suala la kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kupata vifungashio bora vya kuweka bidhaa zao.
Kuimarisha mifumo itakayosaidia taasisi za ukusanyaji wa kodi kukusanya mapato yatokanayo na sekta ya utalii kwa ufanisi na kuhakiki kampuni zinazoleta watalii zinaangaliwa upya.