Bunge jipya lililoapishwa nchini Afrika Kusini limekwishaanza mchakato wa kupiga kura ya siri kumchagua rais mpya atayeliongoza taifa hilo.
Mchakato huo unafanyika huku taarifa zikitangazwa kwamba chama cha African National Congress ANC kimefikia makubaliano ya kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa na vyama vingine vitatu, ikiwemo wapinzani wao wakubwa wanaogemea zaidi sera za kibiashara cha Demokratic Alliance DA.
Soma pia: Chama cha Zuma cha pinga kikao cha bunge cha kumchagua rais
Shirika la habari la taifa SABC limetangaza kwamba serikali hiyo itajumuisha chama cha ANC, DA, Inkatha Freedom na kile cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Patriotic Alliance.
Ripoti zilizochapishwa muda mfupi uliopita kwenye tovuti ya kituo cha habari cha Times zinasema Ramaphosa anategemewa kushinda muhula mwingine chini ya makubaliano yaliyokwishafikiwa na vyama vingine vitatu ambavyo vimeshasema vitamuunga mkono kwenye mchakato huu wa uchaguzi.
Chama cha DA kumuunga mkono Ramaphosa
John Steenhuisen ni kiongozi wa chama cha DA amethibitisha kwamba kambi yake inamuunga mkono Ramaphosa kama walivyokubaliana katika mpango wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Mgombea wa urais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa atatoka kwenye chama kikubwa zaidi miongoni mwa vyama vilivyoungana na kwa maana hiyo ni Rais Cyril Ramaphosa.”
Kiongozi huyo wa DA amefafanuwa kwamba akishachaguliwa Ramaphosa kuendelea kuiongoza Afrika Kusini atakuwa na jukumu la kuteuwa baraza jipya la mawaziri kutoka vyama vyote vinavyounda serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa,kwa kushauriana na viongozi wote wa vyama hivyo.
Soma pia: Chama cha MK chajaribu kuzuia vikao vya kwanza vya bunge
Jana usiku chama cha African National Congress kupitia katibu mkuu wake Fikile Mbalula, kilitangaza kufikia makubaliano ya kushirikiana na DA na vyama vingine viwili vidogo lakini bado kilikuwa kinafanyia kazi mpango kamili wa makubaliano yaliyofikiwa.
Leo bunge lilipokutana kiongozi wa DA John Steenhuisen akatoa taarifa akisema chama chake na kile cha Wazulu chenye sera za kizalendo cha IFP wataunga mkono serikali ya muungano walioamuwa kuuita serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Serikali ya Umoja wa kitaifa
Na muda mfupi uliopita, Katibu mkuu wa ANC Mbalula ameweka wazi kwamba vyama vvya kisiasa vilivyo vingi nchini humo vimekubali juu ya kuwepo serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini akaongeza kusema kwamba muundo wa serikali ya Umoja huo wa Kitaifa utajulikana zaidi wakati Rais Cyril Ramaphosa atakapotangaza.
Hata hivyo chama cha EFF kinachoongozwa na Julius Malema, kimeshasema hakitoiunga mkono serikali inayokuja na hasa kwakuwa kimekataa kujiunga na muungano huo unaowajumuisha wenye mrengo wa kulia au wazungu.
Ingawa pia kiongozi wa DA Steenhuisen amesema mchakato wa kisiasa hautoishia hapa tu akiamini kwamba safari haitokuwa rahisi huko mbele.
Steenhuisen anasema muda wa wiki mbili uliowekwa na katiba wa kuunda serikali haukuwapa nafasi ya kutosha kutafakari kwa kina mambo mengi.