Asilimia 30 bajeti ya Serikali itategemea mikopo, misaada

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitarajia kupata na kutumia Sh49.3 trilioni katika mwaka wa fedha 2024/2025, jambo ambalo wengi wanaweza kujiuliza fedha hizo zitatoka wapi?

Mwananchi imefanya uchambuzi wa bajeti kwa kuangalia vyanzo vya mapato katika bajeti hiyo, kitabu kilichosomwa bungeni jana Juni 13, 2024 kinaonyesha sehemu kubwa ya mapato yatatokana na mapato ya ndani ya Serikali kuu ambayo itakusanya Sh33.25 trilioni (za mapato ya kodi na yasiyo ya kikodi).

Eneo lingine ambalo Serikali inatarajia kukusanya mapato kwa kiwango kikubwa ni mikopo ya kibiashara ndani na nje ya nchi kwa kiasi cha Sh9.6 trilioni, huku misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ikichangia Sh5.1 trilioni.

Kwa maana hiyo ni kuwa pamoja na kutegemea mifuko ya walipakodi kwa zaidi ya theluthi mbili (Sh33.25 trilioni), takribani theluthi moja itakayobakia Serikali itategemea kukopa na misaada ili kutekeleza bajeti yake ambayo kwa ujumla itakuwa Sh14.7 trilioni.

Katika bajeti hiyo ambayo miongoni mwa vipaumbele vyake ni uchaguzi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, mapato ya halmashauri yanatarajia kuchangia Sh1.3 trilioni.

Akiwasilisha bajeti bungeni jana, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 unaweza kuathiriwa na vihatarishi mbalimbali vinavyohusisha mabadiliko ya sera za uchumi, fedha, bajeti, siasa na mahusiano ya kidiplomasia.

“Utekelezaji wa bajeti unaweza kuathiriwa na masuala mtambuka, hususani mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili, magonjwa ya mlipuko na athari za vita baina ya mataifa. Vihatarishi katika bajeti ya mwaka 2024/25 ni pamoja na kudorora kwa uchumi wa dunia,” alisema.

Alitaja mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma, mabadiliko ya riba katika masoko ya fedha ndani na nje ya nchi, mabadiliko ya viwango vya kubadilisha fedha, madeni, siasa na mahusiano ya kidiplomasia, na mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili na magonjwa ya mlipuko.

Dk Mwigulu alisema endapo vihatarishi hivyo vitatokea, athari zinazoweza kujitokeza ni kutofikiwa kwa lengo la ukusanyaji wa mapato, kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi, kuongezeka kwa gharama za bidhaa, malighafi, huduma na utekelezaji wa miradi, kuongezeka kwa gharama za kuhudumia deni la Serikali na kuongezeka kwa gharama za mikopo ya kibiashara katika masoko ya fedha.

Alisema athari nyingine ni kupungua kwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti, kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo, uharibifu wa miundombinu na kuongezeka kwa madai na madeni ya wazabuni na watoa huduma.

Related Posts