KIUNGO mkabaji wa Yanga, Khalid Aucho amesema anautumia muda wake wa mapumziko kuhakikisha anarejea kwenye utimamu wa mwili, ili msimu ujao awe fiti na kufanya makubwa Ligi Kuu Bara.
Msimu ulioisha Aucho aliumia goti mechi ya ugenini ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly ya Misri, ambapo alifanyiwa upasuaji mdogo wa goti, kitu kulichomfanya akae nje ya uwanja, ili kuuguza majeraha yake.
“Kipindi Ligi Kuu inachezwa sikupata muda wa kupumzika vizuri, ndio maana nipo makini nisiuchoshe mwili wangu na kuiruhusu akili kuingiza vitu vipya, ili nikirejea kwenye majukumu nakuwa nguvu mpya.
Aliongeza; “Ukiona kiwango cha mchezaji kipo juu, huyo anakuwa yupo vizuri kwenye akili yake, anakuwa fiti kimwili, kwani soka halina njia za mkato wala kubahatisha.”
“Ndio maana nikiwa mapumziko napenda kutumia muda mwingi nikiwa na ndugu, jamaa na marafiki, kubadilishana nao mawazo ya kimaisha, hivyo naepuka kuyapa nafasi masuala ya soka, ili nisije nikarejea kazini nikiwa sina ari ya kufanya nzuri,”alisema
Aucho alisema msimu ulioisha haukuwa mzuri kwake, kutokana na kupitia changamoto za majeraha, hivyo anatamani ujao uwe wa kung’ara katika karia yake.
“Ingawa furaha yangu ilikuwa ni kuona Yanga inanyakua mataji na hilo lilifanikiwa, kama mchezaji nilitamani huduma yangu iwe bora, bahati mbaya nikaumia nikashindwa kutimiza ndoto zangu, lakini msimu ujao nina imani utakuwa bora kwangu,” alisema Aucho aliyewahi kucheza Kenya (Gor Mahia na Tusker), Scotland, Sauzi, Serbia, India na Misri kwa miaka tofauti na kwa mafanikio.