Unguja. Siku moja baada ya kusomwa bajeti ya Serikali imeelezwa kuwa kuna wanaocheka, kulia na ina utegemezi kwa kiasi kikubwa.
Wakiichambua bajeti hiyo wachambuzi wa siasa, uchumi na wataalamu wa maeneo yaliyoguswa, wamesema licha ya Serikali kuonyesha vipaumbele vitano vya kimkakati na kutanua wigo wa mapato, wamesema wadau wa maendeleo ikitokea wakasitisha misaada Serikali itashindwa kufanya mambo yake kama ilivyopangwa.
Katika bajeti iliyowasilishwa kwenye Baraza la Wawakilishi Juni 13, 2024 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya Serikali imepanga kutumia Sh5.182 trilioni kati ya hiyo Sh4.961 trilioni ni makusanyo ya Serikali Kuu na misaada kutoka kwa washirika ni Sh1.516 trilioni.
Ali Makame, mchambuzi wa siasa amesema bado bajeti ni tegemezi na iwapo ikitokea wahisani wakasitisha misaada inaweza kufanya Serikali ikashindwa kutekeleza mipango kama ilivyopangwa.
“Jambo ambalo limeshtua ni kusema kutakuwa na udhibiti wa gesi ya LPG na kila lita moja watatoza Sh50, ukiangalia na jitihada zinazofanywa kuhamasisha matumizi ya gesi inaweza kuleta shida kidogo,” amesema.
Amesema licha ya kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mitungi ya gesi lakini kinachotakiwa ni gesi yenyewe kwa sababu mtungi mtu anaweza kumaliza hata miaka mitano bila kununua.
Dk Mkuya alisema kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 Mamlaka ya Kudhibiti Huduma za Maji na Nishati (Zura), itaanza kuweka bei elekezi kwa usambazaji wa gesi nchini kama ilivyo kwa mafuta.
Serikali inapendekeza kutoza Sh50 kwa kilo moja ya gesi kama ada ya udhibiti wa uingizaji nchini.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Othman Maulid amesema inasikitisha wakulima wa kawaida hawajapata ruzuku ya mbolea na kilimo cha karafuu hakijapata kipaumbele licha ya kuwa ni chanzo cha mapato.
“Katika mazingira hayo tunaweza kusema bajeti ni nzuri kwa namna yake, wapo walioumia na wengine wamenufaika,” amesema.
Amesema wafanyakazi wanafurahi kwa kuwa watapewa posho ya Sh50,000 kwa mwezi, pia zitatolewa ajira zaidi ya 21,000 mwaka huu.
Amepongeza kubadilishwa viwango vya malipo kwa wageni wanaosafiri kwa boti kulipa kwa Dola badala ya Shilingi kutoka Unguja kwenda Dar es Salaam.
Serikali imependekeza kutoza kiwango cha Dola za Marekani mbili badala ya Sh2,000 kwa wageni wanaosafiri kwenda Tanzania Bara na kiwango cha Dola moja badala ya Sh1,000 kwa wageni wanaosafiri ndani ya Zanzibar. Hatua hii inatarajiwa kukusanya Sh1 bilioni.
Akizungumza kuhusu kuondoa ushuru kwa boti ndogo za uvuvi, kiongozi wa wavuvi Mkokotoni, Yahya Rashid Hussein amesema kwao ni kicheko kwani itasaidia kutengeneza au kuingiza boti nyingi nchini zitakazokuza vipato vya wavuvi.
Amesema bado wavuvi wanahangaika na vifaa hususani boti kwa hiyo mkakati huo utasaidia kutimiza malengo yao.
Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Debbe amesema kuondoa kodi kwenye vifaa vya watu wenye ulemavu ni faraja kwa kundi hilo.
“Ukitazama Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, inaonyesha Zanzibar asilimia 10.4 ni watu wenye ulemavu wa aina moja au nyingine kwa hivyo sisi tunafurahi kwa sababu Serikali imeendelea kusimamia jambo hili na kuona ni haki ya msingi,” amesema Debbe.
Amesema vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ni sehemu ya maisha yao kwa hiyo vikitozwa kodi ni kuwanyima haki yao ya msingi.
Ameiomba Serikali kuendelea kutoa kipaumbele kuhakikisha kodi katika vifaa vingine vya kundi hilo inaondoka.
Kiongozi wa moja ya baa mjini Unguja ambaye hakutaka kutajwa jina amesema kukusanya kodi ni jambo jema, lakini Serikali isiangalie vileo kama ndiyo sehemu pekee ya kuongeza mapato.
Amesema kupandisha kodi za vileo kila wakati ni kuiangalia sekta hiyo kwa mtazamo tofauti, kwani nayo ni sehemu ya kukuza uchumi kama zilivyo sekta zingine.
“Hatupingani na kukusanya kodi, lakini utaona kila mara kwenye bajeti hizi maeneo ni yaleyale ya kuongeza kodi kama vile kukomoa, lakini wanasahau kuwa kama bidhaa hizi zina leseni waache zijiendeshe bila kuzibambikia kodi kila mwaka,” amesema.
Wakati akisema hayo, wapo baadhi ya wananchi waliosema Serikali ilipaswa kupiga kabisa marufuku uingizaji wa shisha kwani kuongeza kodi hakusaidii chochote.
“Kwangu nafikiri lengo ni kuongeza kodi ila siyo kupunguza matumizi kama tulivyoelezwa na waziri, ingekuwa nia ni hiyo wangepiga marufuku uingizaji kabisa lakini kwa kuwa imeongezwa watu hawana shida watalipa na ulevi utaendelea kama kawaida,” amesema Nassor Khamis.
Amesema wanaosimamia jambo hilo kama watoto wao ndio wangekuwa wanatumia wangeona uchungu na kupiga marufuku siyo kuongeza kiwango cha kodi ambacho hakitasaidia kupunguza utumiaji.
Amefafanua kuna ongezeko kubwa la matumizi ya shisha tena kwa vijana katika maeneo mbalimbali ya kawaida na starehe.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Omar Mshei aliyesema ni kama Serikali imehalalisha jambo hilo baada ya muda mfupi kutaibuka tatizo kubwa la ulevi wa shisha kwa vijana badala yake ingepiga marufuku kabisa.
“Ukipita maeneo mbalimbali utaona jinsi matumizi ya vitu hivi yanavyoongezeka kwa kasi, mwarobaini wake ni kuzuia badala ya kutaka kuongeza mapato,” amesema.
Kwa mujibu wa bajeti iliyosomwa juzi barazani ushuru wa bidhaa kwa mvinyo itatoka Sh2,466 hadi Sh4,386 kwa lita moja, ushuru wa bidhaa kwa vinywaji vingine vikali utapanda kutoka asilimia 35 hadi 70. Hatua hiyo itaongeza pato la Serikali kwa Sh1 bilioni.
Waziri Mkuya katika hotuba alisema kumekuwa na wimbi kubwa la matumizi ya shisha na sigara za kielektroniki hususan kwa vijana na watoto wadogo ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Hivyo, Serikali inapendekeza kuongeza kiwango cha kutoza ushuru wa bidhaa kutoka asilimia 35 hadi 120.