Biteko ataka mafanikio yaendene na maisha bora ya watu

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amesema mafanikio yanayoelezwa katika sekta za mafuta, umeme na gesi asilia lazima yaendane na kubadilisha maisha ya watu kuwa bora.

Dk Biteko amesema hayo leo Ijumaa Juni 14, 2024  alipozindua taarifa za utendaji katika sekta ndogo za umeme, gesi asilia na mafuta kwa mwaka 2022/2023, huku akitoa maelekezo mahususi kwa wizara na taasisi za Serikali kufanyia kazi taarifa hizo zinazoonyesha mafanikio na changamoto katika sekta ndogo ya nishati.

Ametoa mfano wa mikoa ya Lindi na Mtwara ambako kunatoka gesi asilia kwamba mafanikio yake hayajabadilisha maisha ya wakazi wa maeneo hayo.

Dk Biteko amesititiza wanapotaja mafanikio kwenye sekta ndogo za mafuta, gesi asilia na umeme, lazima kuwe na mafanikio ya kubadili maisha ya watu wa maeneo husika.

Amesema hii ni mara ya kwanza kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutoa taarifa ya utekelezaji tangu kuundwa kwake.

Dk Biteko amesema utoaji wa taarifa hizo ni maelekezo yake kwa Ewura inayosimamia utendaji katika maeneo hayo, kwamba wana wajibu wa kujipima kama utendaji wa sekta hizo uko kwenye njia nzuri ya kunufaisha Taifa na maendeleo ya wananchi.

Ameitaka Ewura kupima uhusiano wa rasilimali zilizopo na mafanikio ya watu akisisitiza kuwa mafanikio ya sekta lazima yaendane na mabadiliko ya maisha ya watu.

Dk Biteko ameagiza kila aina ya fursa iliyoonekana kwenye taarifa hizo ichukuliwe kwa uzito mkubwa na itambuliwe nani ana uwezo wa kuitumia fursa hiyo ndani ya Serikali na katika taasisi binafsi.

“Vilevile nawaagiza Ewura mhakikishe kuwa, tathmini ya mwaka ujao ihusishe utendaji wa nishati safi ya kupikia ili kuweza kujipima kwa usahihi kuhusu utekelezaji wa ajenda hii inayopewa kipaumbele na Rais Samia Suluhu Hassan,” ameagiza.

Agizo jingine ni kuwa, matishio yote ya sekta ya nishati yaliyoainishwa katika ripoti kati ya mwaka 2023 hadi 2025 yawe na suluhisho  ili katika ripoti ijayo changamoto husika zisiwepo, ikiwemo suala la kuongezeka kwa mahitaji ya umeme kila mwaka.

Ametaka mifumo ya uagizaji mafuta iendelee kuboreshwa baada ya kufanyika utafiti wa kina na kueleza  miundombinu ya mafuta bado inahitajika, huku akisisitiza urasimu usiwepo kwenye sekta ya nishati.

Kuhusu sekta ndogo ya umeme amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuiboresha.

Leo Juni 14, ametoa taarifa kuwa mradi wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) umeingiza mtambo wa pili katika gridi ya Taifa kupitia mtambo namba nane, hivyo kufanya mradi huo kuingiza megawati 470 katika gridi.

Dk Biteko amezungumzia suala la gesi asilia kwamba tangu kutolewa leseni ya mwisho wa uchimbaji gesi mwaka 2006, uongozi wa awamu ya sita umetoa leseni ya uchumbaji wa gesi asilia utakaotoa futi za ujazo zenye kutosheleza mahitaji.

Kuhusu mafuta amesema alipoteuliwa kushika wadhifa huo, suala aliloshughulikia kwa ukaribu ni kuhusu uhaba wa mafuta akieleza alilazimika kumuamuru Mkurugenzi Mkuu wa  Ewura, Dk James Andilile afungie baadhi ya kampuni za uagizaji mafuta kwa kusababisha uhaba wa mafuta nchini.

“Sekta binafsi imetutoa kimasomaso, Serikali haiwezi kufanya kila kitu, wamefanya kazi kubwa mno kwenye mafuta, gesi na hata kwenye uzalishaji umeme, wito wangu kwenu msibaki nyuma changamkieni fursa, na kwa taasisi zilizo chini ya wizara msione sekta binafsi kama watu wajanjawajanja, tuwape kipaumbele,” amesema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema taarifa ya Benki ya Dunia kwa nchi za dunia ya tatu zinazofadhiliwa na benki hiyo inaonyesha sekta ya nishati kwa Tanzania inafanya vizuri zaidi katika nchi zote zinazoendelea na barani Afrika.

Amesema kutokana na mafanikio hayo Benki ya Dunia imeahidi kuendelea kutoa Dola 300 milioni za Marekani kwa ajili ya  utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme.

Mramba amesema kilichoipaisha Tanzania kwenye ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia ni miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Andilile amesema uamuzi uliotolewa na Dk Biteko wa kuruhusu matumizi ya fedha za Euro na Dirham ya Uarabuni kununua mafuta ulisaidia kwa kuwa kulikuwa na upungufu wa Dola.

Amesema uamuzi wa Serikali wa kuruhusu deni la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) la Dola 1.9 bilioni kuwa mtaji umesaidia kuongeza ufanisi kwa shirika hilo.

Andilile amesema sekta ya nishati inaendelea kuimarika ikiwemo uwekezaji kwenye miundombinu ya mafuta, uwekezaji wa vituo vya mafuta na maghala umeongezeka.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema jitihada za Rais Samia za kuiimarisha sekta ya nishati na maji zimesaidia hata wananchi wanalipa ankara za maji bila tatizo ikiwamo kushuhudia uimarikaji wa sekta ya umeme.

Related Posts